2017-07-19 07:17:00

Kenya: kateni mzizi wa fitina kwa kufanya uchaguzi huru na wa haki!


Viongozi wa kidini nchini Kenya wanaitaka serikali, wanasiasa pamoja na wapambe wao kuhakikisha kwamba, uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika nchini humo tarehe 8 Agosti 2017 unakuwa huru, wa haki pamoja na kuhakikisha kwamba amani inatawala. Viongozi wa kidini katika mkutano wao uliohitimishwa hapo tarehe 13 Julai 2017 Jijini, Nairobi wanakaza kusema, kutoakuaminika kwa mchakato mzima wa uchaguzi ndicho chanzo kikuu cha ghasia,kinzani na hatimaye, mipasuko ya kijamii!

Kumbe, Serikali na wadau mbali mbali hawana budi kuhakikisha kwamba, wanawajengea wananchi wa Kenya mazingira yatakayowaaminisha kwamba, kweli zoezi zima la uchaguzi limefanyika katika mazingira huru na ya haki, ili kukata mzizi wa fitina. Kwa wale viongozi ambao hawataridhika na matokeo ya uchaguzi mkuu, basi wanapaswa kufuata taratibu, sheria na kanuni kwa kutafuta haki yao Mahakamani badala ya kuanzisha vurugu na ghasia, hatari sana kwa misingi ya haki, amani na mafungamano ya kitaifa!

Kwa viongozi, wanasiasa na wapambe watakaosikika wakitumia lugha ya uchochezi inayoashiria uvunjifu wa amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, washughulikiwe haraka iwezekano navyo. Tume huru ya uchaguzi nchini Kenya pamoja na Tume ya Mipaka ya Uchaguzi haina budi kuhakikisha kwamba, mchakato mzima unafanyika kadiri ya sheria za nchi na kwamba, wafanyakazi na wasimamzi wa uchaguzi mkuu wapewe mafunzo ya kutosha ili kuwajengea uwezo wa kutekeleza dhamana hii nyeti katika ujenzi wa demokrasia na utawala bora.

Viongozi wa kidini wanavitaka vyombo vya ulinzi na usalama nchini Kenya kuhakikisha kwamba, wananchi na mali zao wanalindwa vyema kabla, wakati na baada ya zoezi la uchaguzi mkuu, kwani historia inaonesha kwamba, hiki ni kipind tete sana katika mchakato mzima wa ulinzi na usalama wa raia na mali zao. Vyombo vya usalama viwashughulikie barabara watu wanaowajengea wanawake hofu, ili hatimaye, washindwe kutekeleza dhamana na wajibu wao wa kikatiba. Wananchi wawanyime kura viongozi wanaotaka kuingia madarakani kwa mtutu wa bunduki na ncha ya upanga; yaani kwa kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia.

Viongozi wa kisiasa, waheshimu na kuthamini mawazo na watu wanaopingana nao, kwani hii ni sehemu ya ukomavu wa kidemokrasia na kwamba, licha ya malumbano yote haya, lazima mshindi mmoja tu ndiye atakayepatikana. Maisha nchini Kenya yataendelea kama kawaida kwa kushinda au kushindwa katika uchaguzi mkuu, kwani haya ni mambo ya mpito na kamwe yasiwavuruge wananchi wa Kenya. Viongozi wa kidini wana matumaini makubwa kwa vyombo vilivyopewa dhamana ya kuratibu, kusimamia na hatimaye kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu na kwamba, wataitekeleza dhamana hii kwa uadilifu na uwajibikaji mkubwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wengi wa Kenya.

Mwishoni, viongozi wa kidini nchini Kenya wanawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kusali ili kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia haki, amani, umoja, uhuru, ustawi na maendeleo ya kweli kwa wananchi wote wa Kenya. Viongozi wa kidini wanawakumbusha Wakenya wote kwamba, kuvuruga uchaguzi ni dhambi kubwa. Ni matumaini ya viongozi wa kidini nchini Kenya kwamba, mchakato mzima wa uchaguzi mkuu utakuwa huru na wa haki na kwamba, wananchi wataweza kuridhika na matokeo ya uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.