2017-07-19 07:59:00

Familia ni shule ya uhai: simameni kidete kupinga utamaduni wa kifo!


Jimbo kuu la Jakarta linaadhimisha miaka 210 tangu kuanzishwa kwa shughuli za uinjilishaji nchini Indonesia kuanzia Batavia, ambalo ni jina la kiholanzi la mji mkuu wa nchi hiyo wakati wa utawala wa kikoloni. Jumuiya za parokia za jimbo kuu la Jakarta zimekuwa zikijikusanya kwa miezi kadhaa sasa kwa ajili ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uinjilishaji jimboni mwao. Kumekuwa pia na nafasi za majadiliano na maundo endelevu kwa vijana kuhusu maisha ya ndoa na familia, ambapo takribani  vijana 3,000 wamekusanyika Kemayoran, katikati ya mji wa Jakarta kwa ajili ya majadiliano na shamra shamra za maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Warsha kuhusu fadhila na tunu msingi za familia, iliandaliwa tarehe 1 Juni 2017 na kamati ya Familia ya Kikatoliki ya Jimbo kuu la Jakarta, warsha iliyoongozwa na kauli mbiu: Familia, shule, uhai. Lengo hasa ni waamini kushirikishana hali halisi, mawazo, na mapendekezo kuhusu namna ya kuishi vema tunu msingi za familia ya kikatoliki na kumshuhudia Kristo katika maisha ya kila siku, kwani ni katika kiini cha maisha ya familia ndipo imani katoliki huchipuka, hukua na kuzaa tunu mpya. Katika warsha hiyo, kumekuwa na wawezeshaji katika fani mbali mbali za maisha, na kumechambuliwa changamoto za maisha ya ndoa na familia katika jamii ya utandawazi na kuona namna sahihi ya kukabiliana na changamoto hizo. Kati ya mada zilizotimua vumbi katika warsha hiyo ni pamoja na mawasiliano ndani ya familia, nafasi ya mume na mke, malezi ya watoto katika mahitaji maalumu, mahusiano ya kimapenzi, utunzaji bora wa uchumi wa familia, utafutaji wa mchumba mkatoliki na changamoto ya ndoa ya pili.

Mada hizi ni za msingi sana kwa jamii ya leo ambapo ubinafsi ndani ya familia unazidi kukua na fadhila za unyenyekevu na ukarimu zinaonekana kukanyagwa na kuharibiwa kwa nyayo zenye machacha sugu. Ni lazima kuziunda upya familia za kikatoliki hasa kwa kujikita katika malezi bora ya watoto kwa kuzingatia tunu msingi za kikristo, kwani ni katika familia ndipo watoto wanajenga utambulisho wao wa kiimani na maadili. Askofu mkuu Ignatius Suharyo wa Jimbo kuu la Jakarta ameongoza Ibada Takatifu ya Misa ikiwa ni kilele cha maadhimisho hayo. Wakati wa mahubiri, kawaalika waamini wa Jakarta kuzidi kukuza ushuhuda wa kuishi tunu msingi za familia za kikatoliki na kuwa chachu kwa majirani zao.

Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.   
All the contents on this site are copyrighted ©.