2017-07-19 15:00:00

Balozi wa Vatican nchini Tanzania awasili! Kumekucha!


Askofu mkuu Marek Solczyński, aliyeteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Tanzania, tayari amewasili nchini humo kuanza kutekeleza majukumu yake rasmi lakini baada ya kuwasilisha hati zake za utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. John Pombe Magufuli. Alipowasili nchini Tanzania amelakiwa na viongozi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania waliongozwa na Askofu mkuu Beatus Kinyaiya, Makamu wa Rais na Naibu Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Padre Daniel Dulle.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko alimteua, mwezi Aprili, 2017 Askofu mkuu Marek Solczyński kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Tanzania, baada ya Askofu mkuu Francisco Padilla kuhamishiwa nchini Kuwait pamoja na kuwa ni Mwakilishi wa Kitume wa Visiwa vya Kiarabu. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Marek Solczyński alikuwa ni Balozi wa Vatican nchini Georgia, Armenia na Azerbaijan. Askofu mkuu Marek Solczyński alizaliwa tarehe 7 Aprili 1961 huko Stawiszyn, nchini Poland. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 28 Mei 1987 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre.

Baada ya kufanya utume wake katika masuala ya kidiplomasia ya Vatican sehemu mbali mbali za dunia na tarehe 26 Novemba 2011, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu mkuu na kumwekwa wakfu tarehe 6 Januari 2012. Askofu mkuu Marek Solczyński ameshiriki kikamilifu katika maandalizi ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Georgia, Armenia na Azerbaijan aliyoitekeleza kunako mwaka 2016.

Wakati huo huo, habari kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania zinasema, Maaskofu wamefanya marekebisho katika Sheria za Baraza kifungu namba 158 na kwa kuongeza nafasi ya Naibu Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Ambaye pamoja na majukumu mengine, atashughulikia masuala ya kiutendaji wa kila siku wa Baraza; kusimamia masuala ya wafanyakazi; nidhamu na atakuwa pia ni mshauri wa masuala ya kisheria na mtekelezaji wa majukumu ya Katibu mkuu anapokuwa nje ya ofisi, au pale Katibu mkuu anaposhindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake kisheria.

Aliyeteuliwa kuchukua na nafasi hii baada ya kutangazwa na Askofu mkuu Beatus Kinyaia, Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ni Padre Daniel Dulle, ambaye hadi kuteuliwa kwake alikuwa ni mshauri wa mambo ya sheria, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na kwamba, ameupokea uteuzi huu kwa moyo wa mkunjufu na shukrani kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Kwa unyenyekevu mkubwa anawaalika wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kumpatia ushirikiano, ili aweze kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini Tanzania. padre Daniel Dulle, kitaaluma ni mwanasheria na anatoka Jimbo Katoliki la Singida.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.