2017-07-19 16:10:00

Askofu Amani: Watawa kiteni Neno la Mungu katika maisha yenu!


Baba Mtakatifu Francisko Jumapili iliyopita, tarehe 16 Julai 2017, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican alisema, Yesu ndiye mpanzi wa mbegu ya Neno la Mungu kazi anayoifanya kwa uvumilivu na ukarimu ili liweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, yaani: toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha kwa wale wote wanaolipokea kwa moyo wa ukarimu na mapendo! Waamini wanapaswa kuwa kweli ni udongo mzuri utakaoweza kuzaa matunda mengi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Ufalme wa Mungu. Roho ya mwamini anayepokea mbegu ya Neno la Mungu, lakini inashindwa kuzama katika undani wa maisha, ni sawa na ile mbegu iliyoangukia kwenye njia, miamba au kwenye miiba.

Hawa ni wale waamini wenye nia na hamu ya kutaka kusali, kupenda na kushuhudia, lakini hawana nguvu ya kuweza kuvumilia, wala ujasiri wa kusonga mbele. Ni waamini wanaompokea Kristo Yesu kadiri ya vionjo vyao, kiasi kwamba, hawawezi kuzaa matunda yanayodumu! Ni watu waliozongwa mno na malimwengu pamoja na uchu wa mali na madaraka; kwa kupenda starehe na anasa za dunia hii, kwa njia hii mbegu ya Neno la Mungu itashindwa kuzaa matunda yanayokusudiwa.

Waamini wanahimizwa kuangalia mioyo yao, ili hatimaye, waweze kutambua ni mambo yepi yanayokwamisha mbegu ya Neno la Mungu kutozaa matunda kwa wakati wake. Ili mbegu ya Neno la Mungu iweze kuchipua na kumea, kuna haja kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanang’oa hiyo miiba na mawe yanayozuiwa mbegu ya Neno la Mungu kuzaa matunda kadiri ya mpango wa Kristo! Wajitahidi kuangalia ikiwa kama nyoyo zao ziko wazi kupokea kwa imani na matumaini mbegu ya Neno la Mungu.

Waamini wawe na ujasiri wa kuondoa vilema vya maisha ya kiroho kwa njia ya: toba na wongofu wa ndani; kwa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika Sakramenti ya Upatanisho; kwa sala na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kamwe waamini wasiwe wepesi wa kuiga mambo ya ulimwengu huu, kwani yatawatumbukiza pabaya na hasa ikiwa kama ni watawa! Waamini wawe na ujasiri wa kulipokea Neno la Mungu na kuliachia nafasi, ili liweze kuzaa matunda ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha, ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya!

Hii ni changamoto ambayo imetolewa Jumapili iliyopita, tarehe 16 Julai 2017 na Askofu Isaac Amani Massawe wa Jimbo Katoliki Moshi ambaye pia ni Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki Mbulu wakati wa Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Kanisa la Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni, Parokia ya Sanu, Jimbo Katoliki Mbulu, kwa ajili ya Masista 14 wa Shirika la Mama wa Mkombozi walioweka nadhiri za kwanza na za daima. Kati yao watawa sita wameweka nadhiri za muda na wengine 8 wameweka nadhiri za daima.

Askofu Isaac Amani Massawe amewataka watawa hawa waliojifunga kwa nadhiri ya: ufukara, utii na usafi kamili, kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni udongo mzuri utakaosaidia kusitawisha mbegu ya Neno la Mungu katika maisha na huduma kwa familia ya Mungu. Watawa pamoja na waamini wote katika ujumla wao, wawe na moyo wa ukarimu kwa kufumbata na kuziishi Amri za Mungu, dira na mwongozo wa maisha adili na ya kiutu!

Wawe na ujasiri wa kuliachia Neno la Mungu liweze kupyaisha maisha yao kwa kuondokana na tabia ya kulalalama daima na kutafuta sababu. Amezitaka familia za Kikristo kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya familia; Kanisa dogo la nyumbani, shule ya utakatifu, haki na amani; pamoja na kuwa ni vitalu vya miito mitakatifu ndani ya Kanisa, ili kweli Kanisa liweze kuwapata Mapadre na Watawa watakatifu, wachapakazi na wachamungu, watakaoshuhudia tunu msingi za maisha ya Kikristo kwa njia ya maisha yenye mvuto na mashiko!

Masista walioweka nadhiri za daima ni Sr. Magdalena Elias Sulle, Sr. Christina Isdori Nade, Sr. Martha  Michael Amsi, Sr. Beatrice  Joseph Orio, Sr. Petronila Pius Momoya , Sr. Geovania Adelard Shirima, Sr. Benedikta Leornard Patrice Na Sr. Magreth John Hose. Masista walioweka nadhiri za kwanza ni Sr. Basilisa Antoni Yustini, Sr Balbina Peter Sumaye,  Sr. Maria Mathew Mefurda, Sr. Adelmas Augustino Shirima, Sr. Anna Philipo Nakei pamoja na Sr. Elizabeth Lucian Humri.

Na Sr. Edith Temu, Jimbo Katoliki Mbulu. 

Na kuhaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.