2017-07-18 15:04:00

Mons. Giacomo Morandi ateuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Kipapa


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Monsinyo Giacomo Morandi, kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na kumpandisha hadhi ya kuwa ni Askofu mkuu. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu mteule Giacomo Morandi, alikuwa ni Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Itakumbukwa kwamba, alizaliwa mjini Modena, Italia, tarehe 24 Agosti 1965. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikuhani, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 11 Aprili 1990.

Kunako mwaka 1992 akatunukiwa Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Biblia kutoka Taasisi ya Kipapa ya Biblia na mwaka 2008 akatunukiwa Shahada ya Uzamivu katika taalimumgu ya Uinjilishaji kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian. Tangu wakati huo ametekeleza dhamana na utume wake kama Padre na Mwalimu katika taasisi mbali mbali huko Modena. Baba Mtakatifu Francisko kunako tarehe 27 Oktoba 2015 akamteuwa kuwa Katibu mkuu Msaidizi wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.