2017-07-18 16:15:00

Kardinali Sandri: Hija ya haki, amani na upatanisho nchini Ukraine


Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki kuanzia tarehe 11 hadi 17 Julai, 2017 amekuwa na ziara ya kikazi nchini Ukraine kama kielelezo cha mshikamano wa upendo na familia ya Mungu nchini humo inayoendelea kuteseka kutokana na madhara ya vita! Jumapili iliyopita, tarehe 16 Julai 2018 ameshiriki katika Liturujia Takatifu katika Madhabahu ya Zarvanytsia na katika mahubiri yake amekazia kwa namna ya pekee: umuhumu wa kukuza na kudumisha amani; imani, matumaini na mapendo miongoni mwa watu wa Mungu nchini Ukraine.

Maandamano makubwa yaliyofanywa na waamini kama sehemu ya hija yao kwenye Madhabahu ya Zarvanytsia ni alama ya imani na matumaini ya watu wa Mungu wanaomkimbilia Mwenyezi Mungu wakiwa na matumaini ya kupata amani katika maisha yao. Hija, kimsingi ni tukio la imani, ambalo waamini wanataka kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu, ili aweze kuwaombea kwa Kristo Yesu ambaye amewaahidia kwamba, atakuwa pamoja nao hadi utimilifu wa nyakati. Kwa njia ya hija ya imani na matumaini, waamini wanapenda kumwomba Bikira Maria aendelee kutekeleza dhamana na utume wake alioachiwa na Kristo Yesu, pale chini ya Msalaba, alipoinama kichwa na kukata roho!

Kardinali Sandri anaendelea kufafanua kwamba, miujiza mbali mbali iliyotendwa na Kristo Yesu kadiri ya Injili ililenga kwa namna ya pekee, kuimarisha imani ya watu waliokuwa wanamzunguka na wala haikuwa ni kwa ajili ya kujitafutia “ujiko”. Kumbe, ili muujiza uweze kutendeka, waamini hawana budi kujiaminisha kwa Kristo Yesu kwa njia ya imani, kama alivyofanya Bikira Maria alipomwamwambia Malaika Gabrieli, nitendewe kama ulivyonena!

Yesu Mwana wa Mungu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu anayo mamlaka ya kuwaondolea watu dhambi na kuwaponya magonjwa yao pamoja na kuwatimizia mahitaji yao msingi; kwani mtu ameumbwa mwili na roho! Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Yesu ameonesha umoja, upendo na mshikamano na binadamu katika mambo yote isipokuwa hakutenda dhambi! Kanisa linaungama na kufundisha kwamba, Kristo Yesu ni mtu kweli na Mungu kweli, aliyezaliwa bila kuumbwa kwake yeye Bikira Maria akawa mwanadamu! Kardinali Sandri anakazia umuhimu wa imani kwa Kristo na Kanisa lake; ili kuweza kujichotea neema na baraka ya toba na wongofu wa ndani, ili kuweza kuondolewa dhambi zao.

Ikumbukwe kwamba, Sakramenti ya Upatanisho ni kiti cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu anayeogelea katika dimbwi la dhambi na mauti! Kumbe, waamini wanahimizwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu katika maisha yao, kama ambavyo wanasali na kuomba katika Sala ya Baba Yetu, muhtasari wa Mafundisho makuu ya Yesu kwa wafuasi wake. Familia ziwe ni chemchemi ya huruma, msamaha, upatanisho na amani ya kweli!

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufuatilia kwa ukaribu sana matukio mbali mbali huko nchini Ukraine na anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa hali na mali. Ameendelea kuombea: haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu nchini Ukraine kama alivyofanya wakati wa kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 150 tangu Yosefati alipotangazwa kuwa Mtakatifu. Kuna matukio mbali mbali ambayo, familia ya Mungu inayaadhimisha kwa ari na moyo mkuu, ikimwomba Mwenyezi Mungu neema na baraka ya kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake.

Kardinali Sandri anawataka waamini wawe kweli ni mashuhuda wa ukweli na upendo; nguvu na uvumilivu katika mateso, dhuluma na nyanyaso wanazokumbana nazo katika historia ya maisha yao. Hata katika mazingira magumu na hatarishi kama haya, waendelee kuonesha umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro kama ambavyo aliwahi kusema, Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea Madhabahu ya Zarvanytsia kunako mwaka 1979. Amewataka vijana wa kizazi kipya nchini Ukraine kumkimbilia na kumsikiliza kwa makini Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa ili aweze kuwafunda mambo msingi katika maisha, ili hatimaye, waweze kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano kati ya watu!

Vijana watambue kwamba, wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwa ni wakamilifu na watakatifu kama alivyo Baba yao wa mbinguni! Wawe ni vyombo vya matumaini na uinjilishaji kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko kwa kutambua kwamba, yote yatapita, lakini upendo wa Mungu wadumu milele. Ibada hii ya Liturujia Takatifu imehudhuriwa pia na Askofu mkuu Claudio Gugerotti, Balozi wa Vatican nchini Ukraine.

Kwa uapande wake, Askofu mkuu Sviatoslav Shevchuk, Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki, Madhehebu ya Kigiriki nchini Ukraine, amempongeza na kumshukuru Kardinali Sandri kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko aliyemwezesha kufanya hija ya haki, amani na upatanisho kwa ajili ya familia ya Mungu nchini Ukraine. Hiki ni kielelezo makini cha uwepo wa Khalifa wa Mtakatifu Petro miongoni mwa watu wanaoteseka na kusumbuka kutokana na changamoto mbali mbali za maisha. Hii ni hija ambazo imekazia umuhimu wa sala, upendo na mshikamano wa kitaifa miongoni mwa familia ya Mungu nchini Ukraine.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.