2017-07-18 15:54:00

CERAO: Vipaumbele: haki, amani na maridhiano kati ya watu!


Familia ya Mungu Barani Afrika haina budi kuendelea kujikita zaidi na zaidi katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ni ujumbe uliotolewa na Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini kwa wajumbe wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya Kati, CERAC, wakati wa mkutano wao wa XI uliohitimishwa hivi karibuni!

Maaskofu katika mkutano huu, wamekazia kwa namna ya pekee, umuhimu wa Kanisa Barani Afrika kuwa ni chemchemi ya upatanisho, haki na amani inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Amani ya kudumu ni changamoto endelevu inayopaswa kuvaliwa njuga na wadau mbali mbali; kwa njia ya toba, msamaha na wongofu wa ndani. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wajitahidi kukuza na kudumisha amani, kwa kujenga na kuimarisha mfumo unaosimikwa katika haki, usawa, demokrasia na utawala bora!

Waamini wakuze ndani mwao Heri za Mlimani, muhtasari wa Mafundisho makuu ya Yesu; kwa kutambua kwamba, upendo katika ukweli ni chemchemi ya amani ya kudumu inayopaswa kumwilishwa katika umoja na mshikamano wa kidugu! Wananchi wamechoshwa na vita, ghasia na mipasuko ya kijamii inayoendelea kuibuka kila kukicha huko Afrika ya Kati. Maaskofu wanaendelea kuwahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho.

Maaskofu wanawataka wale wote wanaoendelea kusababisha vita, chuki na mipasuko miongoni mwa wananchi kuacha mara moja vitendo vya umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia na kuanza kujikita katika mchakato wa: majadiliano unaofumbatwa katika ukweli na uwazi; kwa kudumisha amani inayobubujika kutoka katika toba na msamaha wa kweli, ili hatimaye, kuweza kupata upatanisho wa kitaifa unaokita mizizi yake katika sakafu ya maisha na mioyo ya watu!

Maaskofu kwa namna ya pekee kabisa, wanapenda kuonesha mshikamano wao wa dhati na familia ya Mungu huko Afrika ya Kati ambako bado mtutu wa buduki unaendelea kurindima licha ya mikataba ya amani inayolenga kusitisha mapigano kama haya kutiwa sahihi! Wanawakumbuka na kuwaombea wananchi wa Chad, Cameroon na Congo, Brazzaville ambako bado wanateseka kutokana na mipasuko ya kijamii na kisiasa. Maaskofu wanaitaka Serikali ya Cameroon kuonesha ujasiri kwa kuelezea ukweli bila kificho kuhusu mauaji ya Askofu mkuu Jean Marie Benoit Bala, wa Jimbo kuu la Bafia, aliyeuwawa kikatili tarehe 2 Juni 2017 na mwili wake ukatumbukizwa mtoni, ili kufuta ushahidi. Maaskofu wanasema, kumekuwepo na matukio ya mauaji pamoja na baadhi ya viongozi kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya Kati, CERAC linasema, majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam ni changamani, lina ugumu na changamoto zake, lakini ni jambo linalowezekana, ikiwa kama waamini wa pande zote mbili wanataka kukuza upatanisho, haki na amani; kwa kushirikiana na kushikamana, licha ya tofauti zao msingi, lakini wote wanatambuana kuwa ni watoto wapendwa wa Mwenyezi Mungu. Ubaguzi wa kidini, misimamo mikali na mashambulizi ya kigaidi ni changamoto kubwa katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini.

Mwaliko ni kwa waamini wa dini hizi mbili, kujitaabisha kufahamiana kwa dhati, ili kuheshimiana na kuthaminiana, huku wakitajirishana kwa hali na mali; katika uhuru na ukweli! Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya Kati, CERAC linaundwa  na Mabaraza ya Maaskofu kutoka katika nchi sita nazo ni: Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, Chad, Gabon, Cameroon, Equatorio Guinea pamoja na Congo-Brazzaville. Majadiliano ya kiekumene na kidini Barani Afrika ndiyo kauli mbiu iliyoongoza mkutano wa kumi na moja wa CERAC kwa mwaka 2017. Kwa sasa, Maaskofu wanaendelea kuandaa Waraka wa kichungaji kuhusu majadiliano ya kiekumene na kidini Barani Afrika. Maaskofu watakutana tena kunako mwaka 2020 huko Equatorio Guinea.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.