2017-07-17 10:22:00

Ushuhuda wa Mtumishi wa Mungu Giorgio La Pira


Mtumishi wa Mungu Giorgio La Pira, katika maisha na utume wake alijitahidi kuwa ni shuhuda amini wa Kristo na Kanisa lake; akajimwaga bila kujibakiza katika masuala ya kisiasa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Vietnam. Yote haya yaliyatekeleza katika mwanga wa Injili ya Kristo Mfufuka. Alitekeleza dhamana yake kama wakili mwaminifu, kiongozi mwadilifu na mchaji wa Mungu; aliyejitahidi kusimama kidete kulinda na kudumisha amani na kuhakikisha kwamba, watu wanapata ajira kwa kuendeleza shughuli za uzalishaji na utoaji wa huduma.

Mtumishi wa Mungu Giorgio La Pira alijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia watoto maskini, kwani hawa kwake, walikuwa ni matunda ya kazi na maisha yake ya kiroho! Alikuwa ni kiongozi ambaye aliyakita maisha yake katika unabii kwa kusimamia ukweli katika maisha! Haya yameelezwa hivi karibuni na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, wakati wa uzinduzi wa kitabu cha maisha ya mtumishi wa Mungu Giorgio La Pira kama sehemu ya kumbu kubu ya miaka 40 tangu alipofariki dunia.

Kitabu hiki kimeandikwa na Bwana Mario Primicerio kinachoonesha jitihada za mtumishi wa Mungu katika mchakato wa ujenzi wa amani huko nchini Vietnam, bila kusahau mchango wake katika mchakato wa utunzi wa Katiba ya Italia, Makubaliano ya Itifaki ya Helsinki kuhusu usalama, ushirikiano wa Ulaya na Maendeleo endelevu ya binadamu. Amekuwa ni shuhuda amini wa imani katika matendo, hasa wakati wa kipindi cha “Vita Baridi”, akaonesha huruma na upendo kwa waathirika wa vita nchini Vietnam tangu wakati wa ukoloni.

Huu ni ushuhuda wa maisha uliotolewa na Mtumishi wa Mungu La Pira, kwa kukazia umuhimu wa utamaduni wa maisha ya kimonaki yanayojikita katika upendo kwa Mungu anayepaswa kuabudiwa, kusifiwa, kutafakariwa na kupendwa kwa njia binadamu! Alipenda kujihusisha sana na sala kama chakula chake cha kila siku, kilichoimarishwa na adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu kwa kutambua umuhimu na ukuu wa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu katika maisha na utume wa Kanisa hata kwa familia ya Mungu nchini Vietnam.

Katika mazungumzo yake na Professa Ho Chi Minh, Mtumishi wa Mungu Giorgio La Pira anashuhudia kwamba, hii ilikuwa ni changamoto pevu, kwani amani iliyokuwa inatakiwa nchini Vietnam ilikuwa inawagusa hata watu wengi zaidi duniani iliyokuwa inaathiriwa na Vita Baridi! Nguvu ya sala ilitakiwa ili kushinda nguvu hizi za giza. Akajitahidi kutumia karama na uwezo wake wa maisha ya kiroho, kisiasa, kitamaduni na kiakili alizojipatia wakati wa malezi na majiundo yake katika hatua mbali mbali za maisha. 

Waraka wa kitume wa Mtakatifu Yohane XXIII “Mater et Magista” yaani “Kanisa ni Mama na Mwalimu” ulimsaidia kuchota utajiri wa mafundisho ya Kanisa, akashuhudia baadhi ya nchi za Kiafrika na Kiasia zikijipatia uhuru wake kutoka kwa wakoloni. Akaguswa sana na mahitaji msingi ya wananchi wengi kutoka katika nchi changa zaidi duniani waliokuwa na kiu ya maendeleo: kielimu, kiafya na kiuchumi, kama kielelezo makini cha uhuru na kazi kama ambavyo walikuwa wanasema, wanasiasa wa nyakati hizo!

Mtumishi wa Mungu Giorgio La Pira akajiunga na Chama cha Mtakatifu Vincent wa Paulo, ili kuwahudumia maskini, wazee na wagonjwa, kama mahali muafaka pa kukutana na Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Hii inatokana na ukweli kwamba, maskini ni amana na utajiri wa Kanisa na wao ndio walengwa wa kwanza  wa Habari Njema ya Wokovu! Ekaristi Takatifu iliyomegwa na kutolewa kwa waamini ili iweze kuwa ni chakula cha maisha ya kiroho inapatikana tena katika sura na maisha ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kardinali Pietro Parolin anakaza kusema, huu ndio uliokuwa ufahamu wa maana ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu katika maisha na utume wa Mtumishi wa Mungu Giorgio La Pira ambaye kunako mwaka 1942 aliwataka watu waliobahatika kuwa na utajiri wa mali ya dunia kuonesha huruma na upendo kwa maskini kwa kusitisha vita, kwani vita ni chanzo kikuu cha maafa ya binadamu, umaskini, baa la njaa na magonjwa. Mambo haya yanaweza kusimuliwa kwa uchungu na mtu ambaye ameyaonja na kuyagusa katika safari ya maisha yake kama ilivyokuwa kwa Mtumishi wa Mungu Giorgio La Pira.

Kwa mtu anayeteseka kwa baa la njaa, kiu na utupu; anapata furaha ya ajabu moyoni mwake, anapoonja huruma, upendo na ukarimu kutoka kwa jirani zake. Ili kugundua siri na urembo inayofichika moyoni mwa watu, Mtumishi wa Mungu Giorgio la Pira, aliwataka watu kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu duniani! Ni mang’amuzi haya ya mateso na  mahangaiko ya watu wa Mungu yaliyokuwa ni chimbuko la maisha ya kisiasa ya Mtumishi wa Mungu Giorgio La Pira anasema Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican.

Katika malezi na makuzi yake ya kiakili na kisayansi, daima alitamani kupata suluhu ya matatizo na changamoto zilizokuwa zinamwandama mwanadamu kutokana na vita. Alifahamu fika kwamba, vita ni mama wa maafa na majanga yote yanayomwandama mwanadamu! Upendo wa kisiasa unapaswa kufumbatwa katika upendo wa kiakili unaodumishwa kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi, kwani matatizo na changamoto zinazomwandama mwanadamu zinaweza kupatiwa ufumbuzi makini kwa njia ya majadiliano, tafakari na upembuzi yakinifu! Mtumishi wa Mungu Giorgio La Pira alionja mang’amuzi na kweli za Kiinjili, akaishi kama fukara kati ya maskini, ili kuweza kuwa kweli ni shuhuda na chombo cha amani kati ya watu wa Mataifa

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.