2017-07-17 10:39:00

Simameni kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliowaandikia washiriki wa kongamano la kimataifa kuhusu utunzaji bora wa mazingira katika majiji na miji mikuu duniani  lililokuwa linafanyika huko Rio de Janeiro, nchini Brazil kuanzia tarehe 13-15 Julai, 2017, anakazia kwa namna ya pekee kabisa: umuhimu wa kuheshimu, kuwajibika na kuhusiana kama mambo msingi yanayoiwezesha jamii kuishi kwa amani na utulivu. Kuheshimiana anasema Baba Mtakatifu ni dhamana ambayo binadamu anapaswa kuimwilisha katika mchakato wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayopaswa kuendelea kumshangaza mwanadamu na kuitumia kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi.

Anawahimiza binadamu kusimama kidete kulinda na kutunza maji ambayo ni muhimu sana kwa uhai na maendeleo ya binadamu. Maji safi na salama ni kielelezo makini cha upendo uliokusudiwa na Mwenyezi Mungu kwa binadamu wote! Hii ni haki msingi  inayopaswa kulindwa na kudumishwa na jamii ya binadamu. Maji yasipoheshimiwa yanageuka kuwa ni chanzo cha magonjwa na maafa makubwa kwa mamilioni ya watu duniani. Kumbe, hapa kuna haja ya kuhakikisha kwamba, watu wanajenga tabia ya kulinda na kuhifadhi mazingira, kwa ajili ya ustawi na mafao ya kizazi cha sasa na kile kijacho!

Baba Mtakatifu kuhusu wajibu anasema, binadamu anapaswa kuwajibika barabara katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Mwanadamu hawezi kuendelea kufumbia macho uharibifu, uchafuzi na uzalishaji wa takataka ambazo zinaendelea kuwa kero kubwa na chanzo cha magonjwa na maafa yanayomwandama binadamu. Zote hizi ni dalili zinazoonesha kwamba, binadamu ameshindwa kuwajibika barabara kwa ajili ya mafao ya wengi. Kuna haja ya kushikamana ili kupambana na mambo yote yanayosababisha uharibifu wa mazingira, ili hatimaye, kuboresha afya ya watu wengi duniani!

Kardinali Lluis Martinez Sistach, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Barcellona, Hispania anasema, kongamano hili la kimataifa imekuwa ni fursa ya kuwakutanaisha wataalam na mabingwa katika masuala ya mazingira hasa kuhusiana na rasilimali maji ambayo ni sehemu ya haki msingi za binadamu; afya inayopaswa kulindwa na kudumishwa kama kichocheo cha ushiriki katika shughuli za maendeleo endelevu ya binadamu pamoja na sayansi jamii, inayopania kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kongamano hili ni mwendelezo wa makongamano kama haya yaliyofanyika mjini Barcellona na Roma kunako mwaka 2014 kwa lengo la kutaka kuboresha hali ya maisha ya binadamu kwenye majiji na miji mkuu duniani.

Maboresho haya yanakwenda sanjari na umuhimu wa kuzingatia kanuni maadili, utu wema; umuhimu wa kutekeleza dhamana na wajibu katika kulinda vyanzo vya maji, ili jamii iweze kupata maji safi na salama, chachu muhimu sana ya kupambana na magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji machafu! Afya ni haki ya binadamu wote, kumbe, utunzaji bora wa mazingira unaofumbatwa katika ukusanyaji na hifadhi ya taka ni muhimu sana, ili kuboresha mazingira wanamoishi binadamu! Leo hii anasema Kardinali Lluis Martinez Sistach kuna watu wamekumbwa na magonjwa makubwa makubwa kutokana na uchafuzi wa mazingira, vyanzo vya maji na makazi ya watu hasa kwenye majiji na miji mikubwa zaidi duniani!

Mada hizi zina umuhimu wa pekee katika kujenga na kudumisha mshikamano wa Jumuiya Kimataifa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na hasa baada ya utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani kujiondoa katika utekelezaji wa Itifaki ya Paris, iliyotiwa mkwaju na nchi 195 duniani! Hapa, Jumuiya ya Kimataifa inalenga kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa duniani chanzo kikuu cha athari za mabadiliko ya tabianchi duniani! Ongezeko la ukame wa kutisha, mafuriko, baa la njaa duniani pamoja na changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni kati ya madhara yanayosababishwa na uchafuzi wa mazingira duniani!

Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa mazingira nyumba ya wote ni dira na mwongozo sahihi wa kimaadili na kiutu; unaokazia umuhimu wa mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa katika kupambana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Masuala ya umuhimu wa maji safi na salama; utunzaji na hifadhi ya takataka pamoja na umuhimu wa kutunza mazingira, ili kuhakikisha kwamba, watu wanavuta hewa safi, zimejadiliwa mintarafu kanuni maadili; kwa kuzingatia ushauri wa kisayansi na kitaalam pamoja na kuangalia uwezekano wa kumwilisha ushauri wa watalaam hawa katika uhalisia wa maisha.

Kardinali Lluis Martinez Sistach anasema, waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si”, ukipewa kipaumbele na kumwilishwa katika uhalisia wa maisha, utasaidia sana kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi. Waraka huu una mtazamo wa kinabii kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wengi zaidi duniani! Viongozi wa kidini wanayo dhamana kubwa katika kuwaelimisha waamini wao kuhusu madhara ya uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote! Mazingira ni sehemu ya kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi binadamu kuitunza na kuiendeleza kwa ajili ya kizazi cha sasa na kile kijacho!

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume, “Laudato si” anakazia umuhimu wa toba na wongofu wa kiekolojia, ili kuunda mfumo mpya wa maisha. Jitihada hizi zinahitaji pia ushirikiano wa kiekumene, kwa ajili ya kujenga na kudumisha uekumene wa huduma kwa waathirika wa majanga asilia sehemu mbali mbali za dunia. Uchafuzi mkubwa wa mazingira unaendelea kuwatumbukiza watu wengi katika umaskini, magonjwa na baa la njaa kama inavyojionesha sehemu mbali mbali za dunia kwa wakati huu!

Maji safi na salama; chakula na lishe bora ni mambo yanayofungamana kwa ajili ya ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu! Leo hii kutokana na ukame wa kutisha na uharibifu wa mazingira, kuna uhaba mkubwa wa maji safi na salama; chakula na lishe bora na matokeo yake kuna watoto wanaopoteza maisha kutokana na utapiamlo wa kutisha. Tatizo la maji safi na salama ambayo ni sehemu ya haki msingi ya binadamu bado ni changamoto kubwa sana Barani Afrika!

Rasilimali maji isipolindwa, ikatunzwa na kuendelezwa, inaweza kuwa ni chanzo kikuu cha mipasuko ya kijamii kwa siku za usoni anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Uzalishaji na utunzaji wa taka ni changamoto kubwa kwa miji na majiji mengi duniani! Kuna uzalishaji wa taka za sumu ambazo ni hatari sana kwa maisha ya watu wengi duniani! Hali hii haiwezi kuendelea kufumbiwa macho, bali Jumuiya ya Kimataifa anasema Kardinali Lluis Martinez Sistach, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Barcellona, Hispania inapaswa kuvaliwa njuga, kwa kuheshimu na kuthamini mazingira nyumba ya wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.