2017-07-17 09:08:00

Papa Francisko: Ng'oeni vilema, ili Neno lipate kuzaa matunda!


Kristo Yesu katika maisha na utume aliwahubiria watu kwa kutumia lugha na mifano ya kawaida iliyozoeleka na watu ili kuweza kufikisha ujumbe wa Neno la Mungu kwa watu wengi zaidi. Alitamani kuona kwamba, Neno la Mungu linagusa nyoyo za watu ikilinganishwa na lugha iliyokuwa inatumiwa na viongozi wa wakati ule, iliyokuwa ngumu na kuwafanya watu kuwakimbia. Lugha nyepesi na iliyokuwa inaeleweka kwa wengi ilitumiwa na Yesu kufafanua kuhusu Ufalme wa Mungu, kama inavyojieleza katika mfano wa mpanzi, unaofafanuliwa kwenye Injili ya Jumapili ya XV ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa. Yesu ndiye mpanzi mwenyewe anayejimwaga miongoni mwa watu kama mbegu njema. Yesu anapandikiza mbegu ya Neno la Mungu kwa uvumilivu na ukarimu mkuu ili liweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, kwa wale wote wanaolipokea kwa moyo wa ukarimu na mapendo!

Hii ni sehemu ya tafakari ya Neno la Mungu iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 16 Julai 2017. Baba Mtakatifu anakaza kusema, mfano wa mpanzi unawahusu waamini wenyewe, wanaopaswa kuwa ni udongo mzuri, kuliko hata mpanzi mwenyewe. Yesu katika maelezo yake anapima kwa uangalifu mkubwa nyoyo za waja wake ambazo ziko tayari kupokea Neno lake la uzima.

Moyo ukiwa ni mzuri, mbegu ya Neno la Mungu itaweza kuzaa matunda mengi. Moyo ukiwa mgumu kama jiwe, haupenyeki kwa udi wala uvumba, inakuwa ni vigumu sana kwa mbegu ya Neno la Mungu kuweza kupenya na hatimaye, kuzaa matunda. Hivi ndivyo inavyotokea kwa mwamini kuweza kulisikia Neno la Mungu, lakini likashindwa kupenyeza katika undani wake na hivyo mbegu ya Neno la Mungu kushindwa kuzaa matunda yanayokusudiwa!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, mfano wa mpanzi unaonesha pia aina mbili za nyoyo za watu katika kupokea mbegu ya Neno la Mungu. Sehemu ya kwanza ni udongo wenye mawe, hata kama mbegu ya Neno la Mungu itaweza kumea, lakini itashindwa kuzamisha mizizi yake. Hivi ndivyo ilivyo roho ya mwamini anayepokea mbegu ya Neno la Mungu, lakini inashindwa kuzama katika undani wa maisha ya mwamini. Huu ni moyo unaokuwa na nia ya kutaka kusali, kupenda na kushuhudia, lakini hauna nguvu ya kuweza kuvumilia, unawahi kuchoka kwa kukosa nguvu ya kusonga mbele. Huu ni moyo usiokuwa na nafasi, ni moyo unaotawaliwa na mawe ya uvivu na upendo usiokuwa na mvuto wala mashiko; ni wale waamini wanaompokea Kristo Yesu kadiri ya vionjo vyao, kiasi kwamba, hawawezi kuzaa matunda yanayodumu, watanyauka na kukauka kama kigae!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, moyo wa mwamini uliozungukwa na miiba, utaifanya mbegu ya Neno la Mungu kushindwa kukua na hatimaye, kuzaa matunda yanayokusudiwa. Hii inatokana na ukweli kwamba, huu ni moyo ambao umezongwa mno na malimwengu pamoja na uchu wa mali za dunia hii. Hivi ni vishawishi ambavyo vinapelekea watu kutawaliwa na uchu wa mali na madaraka; kwa kupenda starehe na anasa za dunia hii, kwa njia hii mbegu ya Neno la Mungu itashindwa kuzaa matunda yanayokusudiwa. Hapa, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuangalia mioyo yao, ili hatimaye, waweze kutambua ni mambo yepi yanayokwamisha mbegu ya Neno la Mungu kutozaa matunda kwa wakati wake? Ili Neno mbegu ya Neno la Mungu iweze kuchipua na kumea, kuna haja kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanang’oa hiyo miiba na mawe yanayozuiwa mbegu ya Neno la Mungu kuzaa matunda mioyoni mwao.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, Neno la Mungu, Jumapili ya XV ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa, linawaalika waamini kujichunguza kutoka katika undani wao; ili kuwa na ujasiri wa kumshukuru Mungu kwa udongo mzuri ambao bado uko ndani mwao unaoweza kuzaa matunda mema na kuendelea kujibidisha kuboresha nyoyo ambazo zinaelemewa na malimwengu. Wajitahidi kuangalia ikiwa kama nyoyo zao ziko wazi kupokea kwa imani na matumaini mbegu ya Neno la Mungu. Wawe na ujasiri wa kuondoa vilema vya maisha ya kiroho kwa njia ya: toba na wongofu wa ndani; kwa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika Sakramenti ya Upatanisho; kwa sala na matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Kwa kutekeleza yote haya, Mpanzi ambaye ni Kristo Yesu, ataweza kufurahi kutekeleza kazi yake ya kusafisha nyoyo za waamini kwa kuondoa mawe na miiba inayozuia mbegu ya Neno la Mungu kuzaa matunda yanayokusudiwa. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumkimbilia Bikira Maria wa Mlima Karmeli, aliyeonesha mfano bora na wakuigwa kwa kulipokea Neno la Mungu na kumwilisha katika uhalisia wa maisha yake, awasaidie kutakasa nyoyo zao, tayari kutoa nafasi ya kuhifadhi uwepo wa Mungu katika maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.