2017-07-17 09:23:00

Papa Francisko anawakumbuka na kuwaombea wananchi wa Venezuela


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 16 Julai 2017, aliwashukuru waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, waliofika kuungana naye katika tafakari na sala ya Malaika wa Bwana. Amewakumbuka Wamissionari wa Shirika la Bikira Maria wa Mlima Karmeli wanaoadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria wa Karmeli. Amewataka kujikita zaidi katika safari ya tafakari makini ya Neno la Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko, ametambua uwepo wa Jumuiya ya waamini wa Kanisa Katoliki kutoka Venezuela na kuwakumbusha kwamba, bado anaendelea kusali kwa ajili ya kuombea nchi ya Venezuela ambayo kwa sasa inapitia kipindi kigumu cha historia na maisha yake. Jumapili tarehe 16 Julai 2017 wananchi wamepiga kura ya maoni, kuonesha utashi wao; tukio ambalo linaungwa mkono na Maaskofu Katoliki nchini Venezuela, lakini halitambuliwi kisheria na Serikali ya Rais Nicolàs Maduro.

Lakini, matokeo ya kura hii ya maoni, yanapaswa kuifikirisha sana Serikali ambayo inatarajia pia kuitisha kura ya maoni, hapo tarehe 30 Julai 2017, kura ambayo inataka kubadili Katiba ya nchi kwa kumwongezea madaraka Rais, jambo ambalo Maaskofu wanasema, ni kinyume cha utawala bora! Mambo msingi ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kwa wakati huu ni huduma ya afya, elimu, ustawi na maendeleo ya jamii; ulinzi na usalama kwa raia na mali zao; lakini zaidi: amani na utulivu, kwani kuna watu wanaoendelea kuuwawa kila kukicha, wengine wanapotea katika mazingira ya kutatanisha na kwamba, watoto wanaendelea kufariki dunia kutokana na ukosefu wa chakula, lishe bora na tiba muafaka! Haya ni mambo msingi ambayo yamefafanuliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela katika barua yao ya kichungaji kwa familia ya Mungu nchini Venezuela.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, amewakumbuka kwa namna ya pekee kabisa Masista wa Bikira Maria wa Mateso ”Hijas de la Virgen de los Dolores”, wanaoadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu Shirika hili lilipotambuliwa kuwa na hadhi ya Shirika la Kipapa. Amewakumbuka Masista wa Wafranciskani wa Mtakatifu Yosefu wanaoadhimisha Jubilei ya Miaka 150 tangu kuanzishwa kwa Shirika lao. Mwishoni, amewatakia wote heri na baraka katika maisha yao, akiwaomba kuendelea kumkumbuka katika sala na maisha zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.