2017-07-15 14:43:00

Ukraine: Shuhuda za mateso na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia


Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki akiwa ameambatana na Askofu mkuu Claudio Gugerotti, Balozi wa Vatican nchini Ukraine pamoja na Askofu mkuu Sviatoslav Shevchuk, Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki, Madhehebu ya Kigiriki nchini Ukraine, tarehe 14 Julai 2017 wametembelea miji ya Kramatorsk na Sloviansk; maeneo yaliyokuwa yametekwa nyara na vikosi vya waasi kunako mwaka 2014 na kuzungumza na wananchi wa maeneo haya.

Imekuwa ni fursa ya kusikiliza shuhuda mbali mbali za mateso na mahangaiko ya watu zilizotolewa wakati maeneo haya yalipovamiwa. Kukombolewa kwa miji hii ni heshima kubwa kwa wananchi wa Ukraine ambao bado wanaendelea kuteseka kutoka na vita. Kardinali Sandri amewapongeza na kuwashukuru viongozi wa Kanisa ambao wameendelea kushikamana na watu wao licha ya mateso na magumu waliyokumbana nayo katika huduma kwa familia ya Mungu. Amesikiliza shuhuda mbali mbali kutoka kwa Mapdre waliokuwa kwenye orodha ya kuchapwa viboko na waasi wa Ukraine.

Kuna baadhi ya Mapadre wameamua kwenda kutoa huduma kama Mapadre wa maisha ya kiroho kwa vikosi vya ulinzi na usalama, wakiwa bega kwa bega na waamini wao ambao walilazimika kubeba silaha ili kulinda umoja na mustakabali wa taifa la Ukraine. Kimekuwa ni kipindi cha mateso na mahangaiko makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia. Lakini, waamini wamejitahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano katika huduma makini, maisha ya sala na uekumene wa damu unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto kwa Kristo na Kanisa lake. Mapadre wamekuwa mstari wa mbele kutoa huduma ya kiroho kwa wananchi waliokuwa wanatekwa nyara; wagonjwa na majeruhi waliokuwa wanahitaji msaada. Huduma yote hii imetolewa katika ari na moyo wa upendo na udugu.

Kardinali Leonardo Sandri amewashukuru na kuwapongeza kwa moyo wa umoja, udugu na mapendo kwa familia ya Mungu nchini Ukraine. Anapenda kuonesha uwepo wa karibu wa Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wao. Anawahimiza kuendelea kujenga na kuimarisha madaraja ya watu kukutana na kusaidiana kama ndugu, kwa kubomoa kuta za utengano, vita na ghasia; wakitambua kwamba, wao ni ndugu wamoja, tofauti zao msingi zisiwe ni sababu ya chokochoko za kisiasa na mipasuko ya kijamii. Hapa kuna haja ya kudumisha uhuru wa kuabudu unaofumbatwa katika haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Majadiliano ya kisiasa katika ukweli na uwazi kwa msaada wa Jumuiya ya Kimataifa hayana budi kuendelezwa zaidi, ili kujenga misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa, baada ya “patashika nguo kuchanika”. Amepongeza huduma makini inayotolewa na Kanisa kwenye kambi za wakimbizi na wahamiaji huko Ukraine. Wafanyakazi wa Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini Ukraine, Caritas Ukraine wamekuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kwa njia ya huduma wameonesha utu na heshima yao na kwamba, atakaporejea mjini Vatican atamsimlia Baba Mtakatifu Francisko kile alichoshuhudia kwa kusikia na kujionea mwenyewe. Watu bado wana wasi wasi kuhusu hatima ya maisha yao, lakini Kardinali Sandri amewataka kuwa na ari na moyo mkuu, kwani amani ikishatoweka inakuwa ni vigumu sana kuweza kurejeshwa. Kumbe, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kujikita kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa amani nchini Ukraine.

Hii ndiyo changamoto inayotolewa pia na Baba Mtakatifu Francisko anayewataka viongozi wenye dhamana na hatima ya maisha ya wananchi wa Ukraine kuhakikisha kwamba: haki, amani na maridhiano yanapatikana kwa viongozi  kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki amekutana na kuzungumza pia na Masista wa Shirika la Mtakatifu Yosefu lililoanzishwa nchini Ukraine kunako karne XIX na sasa limeenea hadi Brazi. Canada na Poland. Hawa ni watawa wanaojisadaka kwa ajili ya katekesi makini, malezi na majiundo kwa vijana wa kizazi kipya. Amewashukuru na kuwapongeza watawa vijana ambao wameamua kuacha yote na kumfuasa Kristo Yesu kwa ajili ya huduma kwa familia ya Mungu ndani na nje ya Ukraine.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.