2017-07-15 14:11:00

Uhuru wa kidini ni kitochu ya haki msingi za binadamu!


Kutambua na kuheshimu haki msingi za binadamu ni hatua muhimu sana ya maendeleo ya binadamu, kwani mizizi ya haki za binadamu inafumbatwa katika hadhi na utu wa binadamu mwenyewe aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hizi ni haki za wote zisizoweza kukiukwa wala kutenguliwa. Ni za binadamu wote bila kujali: wakati, mahali au mhusika. Haki msingi za binadamu zinapaswa kulindwa na kudumishwa na wote. Haki ya kwanza kabisa ni uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi pale anapofariki dunia kadiri ya mpango wa Mungu. Mkazo umewekwa katika haki ya uhuru wa kidini inayofafanuliwa katika uhuru wa kuabudu. Hiki ni kiini cha haki msingi kinachofumbata haki nyingine zote. Kuheshimu na kuthamini haki hii ni alama ya maendeleo halisi ya binadamu katika medani mbali mbali za maisha! Haki inakwenda sanjari na wajibu!

Mama Kanisa anakazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu  wa kuheshimu haki msingi za binadamu kichocheo muhimu sana cha amani na utulivu miongoni mwa binadamu. Kanisa linapenda kusimama kidete kustawisha haki na amani sehemu mbali mbali za dunia kwa njia ya mwanga na chachu ya Injili. Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa hivi karibuni, ameshiriki katika mkutano wa kimataifa kuhusu dini ulioandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa nchini Italia kuhusu umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kulinda na kudumisha uhuru wa kidini unaofafanuliwa katika uhuru wa kuabudu.

Askofu Mkuu Gallagher anasikitika kusema, kwamba, kwa miaka mingi, Wakristo huko Mashariki ya Kati na katika baadhi ya nchi wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu kwa kubaguliwa na kutengwa kana kwamba, wao ni ”watu wa kuja” hata katika nchi yao wenyewe! Dhana na sera za ubaguzi na nyanyaso kwa misingi ya kidini ni hatari sana kwa maendeleo na mafungamano ya kijami sehemu mbali mbali za dunia. Uwezo wa kiuchumi, ujenzi wa miundo mbinu ya sala na Ibada; uhuru wa kidini na kuabudu ni mambo msingi yanayoweza kusaidia kujenga jamii inayomsikwa katika amani, utulivu na udugu.

Askofu Mkuu Gallagher anakaza kusema, Vatican itaendea kusimamia haki msingi za binadamu na uhuru wa kuabudu kwa watu wote bila kujali: dini, rangi au mahali anapotoka mtu! Kwa namna ya pekee, Vatican inapenda kuelekeza jicho lake huko Mashariki ya Kati, kwani huko ndiko chimbuko la Ukristo, chemchemi ya mshikamano wa maisha ya kiroho; lakini pia ni mahali ambapo Wakristo wengi wanateseka, wananyanyaswa na kudhulumiwa, ikilinganishwa na waamini wa dini nyingine katika maeneo haya. Katika mazingira na hali kama hii, uhuru wa kuabudu; amani na usalama vinakuwa mashakani.

Kwa nyakati mbali mbali, viongozi wakuu wa Kanisa Katoliki wamekaza kusema kwamba, Ukristo ni sehemu ya utambulisho wa wananchi wanaoishi huko Mashariki ya Kati. Mashambulizi ya kigaidi, misimamo mikali ya kidni na kiimani; nyanyaso na madhulumu dhidi ya Wakristo yanapania kuharibu utambulisho huu huko Mashariki ya Kati. Lakini, ikumbukwe kwamba, huu ni utambulisho wa watu ambao umejikita katika vinasaba vya maisha yao, changamoto na mwaliko wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu!

Ubaguzi, nyanyaso na dhuluma za kidini ni kwenda kinyume cha haki msingi ya uhuru wa kidini inayotafsiriwa katika uhuru wa kuabudu unaopaswa kulindwa na kudumishwa kwa kuondokana na misimamo mikali ya kidini inayotaka kusimika dini kwa njia ya ghasia na mtutu wa bunduki! Kuna haja ya kudhibiti matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii inayohatarisha mafungamano ya kijamii kwa kuandika maneno yenye uchochezi dhidi ya imani na dini za watu wengine. Ikumbukwe kwamba, uhuru wa kidini ni sehemu ya haki msingi za binadamu, inayopaswa kulindwa, kuheshimiwa na kuendelezwa na wote.

Ni wajibu wa viongozi wa kidini kuwaelimisha wafuasi wao kutambua na kuthamini uhuru wa kidini kama njia ya kukuza na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu. Vita, ghasia na vurugu si sehemu ya maisha ya kidini. Katika mkutano huu wa dini kimataifa, Waziri wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa nchini Italia, Bwana Angelino Alfano amesema kwamba, Serikali ya Italia imeanzisha kitengo maalum cha kuangalia haki ya kuabudu sehemu mbali mbali za dunia. Ni kitengo ambacho kwa kutumia mtandao wa kidiplomasia kitaweza kuhabarisha Serikali ya Italia kuhusu matukio makubwa ya kidini, uvunjifu wa uhuru wa kuabudu na mahali ambapo kuna haja ya kukemea ili kulinda uhuru wa kuabudu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.