2017-07-15 14:57:00

Papa Francisko: Waonjesheni matumaini ya Kikristo waliokata tamaa!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa ajili ya nia za jumla kwa Mwezi Julai, 2017 anawaomba waamini kuonesha moyo wa upendo na ukarimu; kwa kuwa karibu na kushirikiana na wale wote ambao wanaonekana kana kwamba, wako mbali sana na masuala ya imani ya Kikristo. Ujumbe wa Baba Mtakatifu unasambazwa na mtandao wa utume wa sala, unaonesha kwamba, Baba Mtakatifu ana matumaini makubwa kwa Kanisa kuweza kuwasikiliza kwa makini, wale wote waliovunjika na kupondeka moyo kutokana na sababu mbali mbali.

Waamini waoneshe ukarimu na moyo wa kuwasikiliza kwa makini na hatimaye, kuweza kuwasaidia wale ambao katika safari ya maisha yao ya kiimani wamepoteza ile furaha, inayopata chimbuko lake kutoka kwa Injili ya Kristo! Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, kiini cha furaha yao ya kweli ni Kristo Yesu, upendo wa Baba usiokuwa na kikomo! Kwa wale waamini ambao wanajikuta wakiwa na majonzi na wasi wasi moyoni, hapo Baba Mtakatifu anasema, kuna sehemu ambapo wamesigana na Kristo Yesu.

Kuna watu wengi leo hii wamekatishwa tamaa kutokana na matatizo na changamoto mbali mbali za maisha; kiasi kwamba, hawaoni tena sababu ya kuingia Kanisani na kusali; wanadhani kwamba, milango ya Kanisa imefungwa mbele yao na kamwe hawawezi kuingia tena! Lakini, Baba Mtakatifu anakaza kusema, matumaini ni fadhila ambayo waamini wanapaswa kushirikishana na jirani zao; kwa kuwaendea na kuwagusa wale waliokata tamaa; watu wanaoogelea katika shida na magumu ya maisha; hawa ndio wale wanaopaswa kushikwa mabegani, na kutiwa shime ya kusonga mbele kwa imani na matumaini.

Hawa ni watu wanaopaswa kuonjeshwa upendo na ukarimu na kamwe wasiachwe pweke katika mateso na mahangaiko yao ya ndani! Wakristo wawe mstari wa mbele kuwaonjesha imani na matumaini yanayobubujika kutoka katika uhuru na furaha ya kweli! Baba Mtakatifu anakamilisha ujumbe wake kwa njia ya video kwa sala ya nia yake ya jumla kwa mwezi Julai, kwa kusali na kuwaombea waamini ambao wamekuwa mbali na imani, ili kwa njia ya sala na ushuhuda wa Injili, waweze kugundua tena uzuri na utakatifu wa maisha ya Kikristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.