2017-07-15 13:50:00

Papa Francisko: Heshimuni na kuwajibika katika utunzaji wa mazingira


Kuna haja ya kuheshimu, kuwajibika sanjari na ujenzi wa mahusiano na mafungamano mema na mazingira. Hii ni changamoto kubwa iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa washiriki wa kongamano la kimataifa juu ya utunzaji bora wa mazingira kwa majiji na miji mikuu duniani, huku wakiongozwa na Waraka wa Kitume, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”, huko Rio de Janeiro, Brazil. Kongamano hili lilizinduliwa na Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu, tarehe 13 Julai na kuhitimishwa tarehe 15 Julai 2017.

Mada ambazo zimepembuliwa kwa wakati huu ni pamoja na maji safi na salama kama sehemu ya haki msingi za binadamu; umuhimu wa hewa safi; ukusanyaji na hifadhi ya taka za mijini. Lengo la kongamano hili ni kuhakikisha kwamba, kanuni maadili na utu wema, vinazingatiwa kwa ajili ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Laudato si”. Wajumbe, wamehimizana kuhusu umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kushikamana katika kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi kwani ni chanzo kikuu cha umaskini, maafa na mahangaiko ya watu wengi duniani!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Kardinali Lluis Martinez Sistach, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Barcellona, Hispania anakazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu wa kuheshimu, kuwajibika na kuhusiana kama mambo msingi yanayoiwezesha jamii kuishi kwa amani na utulivu. Kuheshimiana anasema Baba Mtakatifu ni dhamana ambayo binadamu anapaswa kuimwilisha katika mchakato wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, zawadi makini kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayopaswa kuendelea kumshangaza mwanadamu na kuitumia kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi.

Mtakatifu Francisko wa Assisi katika utenzi wake “Laudato si” anawahimiza binadamu kusimama kidete kulinda na kutunza maji ambayo ni muhimu sana kwa uhai na maendeleo ya binadamu. Maji safi na salama ni kielelezo makini cha upendo uliokusudiwa na Mwenyezi Mungu kwa kila binadamu! Hii ni haki msingi  inayopaswa kulindwa na kudumishwa na jamii ya binadamu. Maji yasipoheshimiwa yanageuka kuwa ni chanzo cha magonjwa na maafa makubwa kwa mamilioni ya watu duniani. Kumbe, hapa kuna haja ya kuhakikisha kwamba, watu wanajenga tabia ya kulinda na kuhifadhi mazingira, kwa ajili ya ustawi na mafao ya kizazi cha sasa na kile kijacho!

Baba Mtakatifu kuhusu wajibu anakaza kusema, binadamu anapaswa kuwajibika barabara katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Mwanadamu hawezi kuendelea kufumbia macho uharibifu, uchafuzi na uzalishaji wa takataka ambazo zinaendelea kuwa kero kubwa na chanzo cha magonjwa na maafa yanayomwandama binadamu. Zote hizi ni dalili zinazoonesha kwamba, binadamu ameshindwa kuwajibika barabara kwa ajili ya mafao ya wengi. Inasikitisha kuona kwamba, kuna watu ambao wanashindwa kabisa kuonesha upendo na mshikamano na watu wanaoathirika kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Hizi ni dalili za watu kushindwa kuwajibika na hivyo kutikisa msingi wa maisha ya kijamii. Serikali kwa kushirikiana na wadau mbali mbali zisaidie kuwahamasisha wananchi kujenga tabia na utamaduni wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, ili kudumisha afya bora. Kila mtu akiwajibika kwa kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake, kwa hakika Familia ya binadamu itajipatia mafanikio makubwa!

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, leo hii si mijini wala vijijini, mahusiano na mafungamano ya kijamii yanaendelea kuporomoka kutoka na ukweli kwamba, kumekuwepo na mwingiliano mkubwa wa watu, ambalo kimsingi ni jambo jema. Kuna kuwepo na utajiri mkubwa na ukuaji wa jamii na ongezeko la watu! Jambo la kusikitisha ni kuona kuwa Jamii ya namna hii haiguswi na mahangaiko ya wengine kwani imejifunga katika undani wake. Kuna baadhi ya watu wanakosa utambulisho na wengine wanatengwa katika jamii na kujikuta wanaishi katika mazingira duni sana.

Yote hii ni mifumo ya umaskini, ghasia na ukosefu wa haki msingi za binadamu, inayopaswa kushughulikiwa kwa njia ya mshikamano na mafungamano katika masuala ya kisiasa, kidini na kielimu, ili kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kibinadamu, yanayovunjilia mbali kuta za utengano. Mchakato huu unaweza kufanikiwa kwa njia ya vikundi, shule, Parokia na makundi mengine ya watu yanayoweza kujenga umoja, mshikamano na utambulisho utakaowasaidia watu kuishi kwa amani na utulivu hatimaye, kuvuka vikwazo na changamoto zinazowasibu, tayari kusukuma mbele mchakato wa maboresho ya maisha ya watu. Mwishoni, Baba Mtakatifu aliwaweka wajumbe wa kongamano hili chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Malkia wa mbingu na dunia, ili kwamba, ushauri wake uweze kuwaongoza wajumbe kusimama kidete, kulinda, kutunza na kudumisha mazingira nyumba ya wote; kwa kujenga na kusimamia utu wema na mshikamano wa kidugu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.