2017-07-15 07:16:00

Diplomasia ya Vatican inapania kudumisha: Haki, amani, utu na heshima


Diplomasia inayotekelezwa na Vatican sehemu mbali mbali za dunia inajikita kwa namna ya pekee, katika msingi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu! Ni diplomasia inayojipambanua kwa kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Tangu mwanzo wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu Francisko, amekazia kuhusu umuhimu wa diplomasia ya Vatican kufumbatwa katika amani, kwa kusimama kidete kupambana na baa la njaa na umaskini duniani; kwa kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote kwani kuna mamilioni ya watu wanaoathirika kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa fursa za ajira na maendeleo endelevu!

Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na Jumuiya ya Kimataifa kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kidugu, ili kuweza kukabiliana na changamoto katika ulimwengu mamboleo.Mataifa yatambue kwamba, yanategemeana na kukamilishana na kwamba, binadamu ni kiumbe jamii. Kwa njia, hii, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kuwa ni alama ya matumaini kwa wale waliokata tamaa ya maisha kutokana na sababu mbali mbali.

Hizi ni kanuni msingi zinazozifanya nchi kadhaa kuendelea kudumisha uhusiano wao wa kidiplomasia na Vatican kwa kuwa na Mabalozi wao wakazi kama ilivyojidhihirisha hivi karibuni kwa Afrika ya Kusini ambayo imeamua kumtuma Mheshimiwa George Johannes, Balozi wa kwanza mkazi kutoka Afrika ya Kusini. Hii inatokana na ukweli kwamba, Vatican ni mdau wa kuaminika katika masuala haki, amani, maridhiano, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Balozi George Johannes, hivi karibuni katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano amesema, Serikali ya Afrika ya Kusini imeamua kuwa na Balozi mkazi mjini Vatican ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani kama njia ya kupambana na changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza kila kukicha. Vatican ni wadau makini katika mapambano dhidi ya baa la njaa na umaskini sanjari na ukuzaji wa haki, utu na heshima ya wanawake. Haya pia ni mambo ambayo Serikali ya Afrika ya Kusini inataka kuyavalia njuga na hatimaye, kuyapatia majibu muafaka!

Itakumbukwa kwamba, Balozi George Johannes aliwasilisha hati zake za utambulisho mjini Vatican tarehe 3 Juni 2017 na kwamba, anaiwakilisha Afrika ya Kusini muda wote, ikinganishwa na ilivyokuwa miaka kadhaa iliyopita. Huu ni mchakato wa kisiasa ulionzishwa kunako mwaka 1994, Mzee Nelson Madiba Mandela alipoamua kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Vatican. Anakumbusha kwamba, kabla ya hapo, Wakristo walikuwa wanapambana na utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini kimya kimya, kwani walihesabiwa kuwa ni wakomunisti, watu hatari sana kwa ustawi na maendeleo ya nchi. Lakini, leo mambo yamebadilika sana kwani kuna uhusiano wa karibu kati ya Afrika ya Kusini na Vatican, kiasi hata cha kufikia uamuzi wa kuwa na Balozi mkazi mjini Vatican, jambo ambalo si rahisi sana, ikizngatiwa kwamba, nchi kadhaa zinawakilishwa mjini Vatican kwa mabalozi wasiokuwa na makazi yao rasmi mjini Roma. Ni wanadiplomasia wanaotekeleza dhamana yao kutoka katika nchi nyingine.

Balozi George Johannes anakiri kwamba, huu pia ni ushuhuda wa maisha na utume unaooneshwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama chombo cha amani, Baba wa maskini, sauti na mtetezi wa wanyonge duniani. Hata Kanisa Katoliki nchini Afrika ya Kusini limekuwa mstari wa mbele katika huduma kwenye sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya wengi! Huduma hii inatolewa kwa wananchi wote wa Afrika ya Kusini pasi na ubaguzi.

Ushuhuda huu ni kielelezo cha imani tendaji kama ilivyojionesha kwa Mwenyeheri Benedikto Daswa, baba aliyebahatika kupata watoto nane, lakini akapigwa kwa mawe hadi kufariki dunia kunako mwaka 1990 kwa kupinga imani za kishirikina. Kutokana na ushuhuda wa imani yake kwa Kristo na Kanisa, kunako mwezi Septemba 2015 akatangazwa kuwa ni Mwenyeheri, mfano bora wa kuigwa na familia ya Mungu ndani na nje ya Afrika kwa ushuuda na udumifu wake. Mashuhuda hawa wa imani, matumaini na mapendo, wameiwezesha Afrika ya Kusini kuendelea kucharuka katika maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili, licha ya changamoto nyingi zinazoendelea kujitokeza!

Balozi George Johannes anakiri kwamba, kiwango na ubora wa elimu unaotolewa kwenye taasisi za elimu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki ni cha hali ya juu, kwani elimu inalenga kumkoboa mwanadamu: kiroho na kimwili. Mfumo huu wa elimu unafikiwa na watu wengi ndani ya jamii; mazingira ya kufundishia na kusomea yanavutia sana na kwamba, kuna mitaala sahihi na watumishi wa elimu ambao wako tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Afrika ya Kusini. Mfumo mzima wa elimu inayotolewa na taasisi za Kanisa Katoliki unaleta matumaini kwa watu wengi.

Balozi George Johannes anaendelea kufafanua kwamba, Kanisa kweli limekuwa ni chombo cha haki, amani na upatanisho kati ya watu wa Mataifa. Vatican imepata mafanikio makubwa katika diplomasia ya usuluhishi kama ilivyojitokeza kati ya Marekani na Cuba, ingawa sasa kuna mwelekeo mwingine wa upepo. Afrika ya Kusini inaendelea kujifunza sera na mbinu za kupambana na migogoro, kinzani na mipasuko ya kijamii, ili hatimaye, kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upatanisho na mafungamano ya kijamii.

Afrika ya Kusini inaendeleza mchakato wa majadiliano ya kisiasa nchini Sudan ya Kusini ili kusitisha machafuko ya kisiasa yanayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao kama ilivyo pia huko Jamhuri ya Watu wa Afrika ya kati. Haya ni maeneo ambayo vita imekuwa ni chakula chao cha kila siku na kusahau kwamba, wanaweza kuweka silaha chini na kuanza kuandika kurasa mpya za matumaini, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Majadiliano haya yanafumbata pia majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kuishi kwa amani na utulivu; kwa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa, chachu muhimu sana ya maendeleo endelevu. Haya ni mambo msingi kabisa ambayo dini sehemu mbali mbali za dunia zinaweza kuchangia katika maisha ya watu wa Mungu. Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji inashughulikiwa vyema na viongozi wa kidini ikinganishwa na viongozi wa kisiasa.

Mheshimiwa George Johannes, Balozi wa kwanza mkazi kutoka Afrika ya Kusini anahitimisha mahojiano yake na Gazeti la L’Osservatore Romano kwa kusema, viongozi wa kidini wanapaswa kushirikiana kwa karibu sana na viongozi wa kisiasa ili kukuza na kudumisha jamii ambamo: haki, amani na upatanisho; umoja, udugu na mshikamano vinalindwa na kudumishwa na wengi. Serikali ya Afrika ya Kusini inapenda kushirikiana na Vatican katika diplomasia kwani ni nchi inayoaminika sana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.