2017-07-14 15:56:00

Vigogo wawili wa Hospitali ya Bambino Gesù wapandishwa mahakamani


Mahakama ya Vatican chini ya uongozi wa Professa Giani Pietro Milano na Professa Roberto Zannotti imewafungulia mashitaka Professa Giuseppe Profiti, aliyewahi kuwa Rais wa Hospitali ya Bambino Gesù pamoja na Massimo Spina aliyewahi kuwa ni mhasibu mkuu wa Mfuko wa Bambino Gesù mashitaka ya ubadhirifu wa mali ya Kanisa. Kesi yao itaanza kusikilizwa kwa mara kwanza, Jumanne tarehe 18 Julai 2017. Wahusika wanatuhumiwa kuidhinisha kiasi cha Euro 422, 000 nje ya taratibu, kanuni na sheria za mfuko kwa ajili ya kugharimia ukarabati wa makazi ya Kardinali Tarcisio Bertone, aliyekuwa Katibu mkuu wa Vatican, wakati alipokang’utuka kutoka madarakani kunako mwaka 2013. 

Kiasi hiki cha fedha kililipwa kwa kampuni ya ujenzi ya Bwana Gianantonio Bandera, kosa ambalo lilitendwa mjini Vatican kati ya Mwezi Novemba 2013 hadi tarehe 28 Mei 2014. Professa Profit tangu awali amekuwa akikanusha shutuma hizi kwa kusema kwamba, fedha hii ilikuwa imewekezwa katika majengo haya kwa ajili ya kusaidia kuhamasisha watu kuchangia katika Mfuko wa Bambino Gesù.  Itakumbukwa kwamba, Professa Profit alikuwa ni Rais wa Hospitali ya Bambino Gesù kuanzia mwaka 2008 hadi mwezi januari 2015 alipojiuzuru kutoka madarakani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.