2017-07-14 14:29:00

Ukraine: Jengeni umoja wa kitaifa unaofumbatwa katika upatanisho!


Familia ya Mungu nchini Ukraine haina budi kujikita katika fadhila ya imani, matumaini na mapendo, licha ya changamoto nyingi zinazoikabili kwa wakati huu. Kuna haja ya kuendelea kujikita katika mchakato wa haki, amani na maridhiano, kwa kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa. Ni mwaliko ambao umetolewa hivi karibuni na Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki wakati huu wa safari yake ya kikazi nchini Ukraine, iliyoanza hapo tarehe 11 Julai na anatarajia kuikamilisha hapo tarehe 17 Julai, 2017.

Kardinali Sandri amehudhuria Liturujia Takatifu kwa ajili ya sherehe ya Mitume Petro na Paulo miamba wa imani, kwa kuwataka wananchi wa Ukraine kudumisha umoja na upatanisho wa kitaifa! Kardinali Sandri akiwa nchini Ukraine anaambatana na Askofu mkuu Claudio Gugerotti, Balozi wa Vatican nchini Ukraine pamoja na viongozi wa Kanisa nchini humo. Hawa ni pamoja na Askofu mkuu Sviatoslav Shevchuk, Kiongozi mkuu wa Kanisa la Kikatoliki, Madhehebu ya Kigiriki.

Kardinali Sandri amewakumbuka na kuwaombea wale wote wanaoteseka kutokana na mpasuko wa kijamii na kisiasa nchini Ukraine wakati huu wa vita. Amewahakikishia uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi kigumu cha maisha na historia ya wananchi wa Ukraine kwa hali na mali! Baba Mtakatifu anawashukuru kwa sala na sadaka waliyotolea wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Watakatifu Petro na Paulo, mitume na miamba wa imani; sanjari na maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 tangu Mtakatifu Josefati alipotangazwa kuwa Mtakatifu, mfano bora wa kuigwa na waamini wengine.

Ni mtakatifu aliyeyamimina maisha yake kama ushuhhuda wa hali ya juu kabisa wa upendo wake kwa Mwenyezi Mungu na kwa ajili ya umoja wa Kanisa. Amewataka waamini kuwa ni mashuhuda na vyombo vya umoja, upendo na mshikamano kati ya watu wa Ukraine.  Wawe ni mfano wa kuigwa katika imani, matumaini na mapendo, daima wakijitahidi kutafuta ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; mambo msingi ambayo yanaweza kukoleza na kudumisha umoja na upatanisho wa kitaifa, badala ya kukuza utengano na ghasia, mambo ambao kwa sasa yanaendelea kusababisha mateso na mahangaiko makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia.

Kardinali Leonardo Sandri ameungana na familia ya Mungu nchini Ukraine kwa ajili ya kusali na kumwombea Marehemu Kardinali Lubomyr Husar aliyefariki dunia hivi karibuni! Akizungumza na waandishi wa habari nchini Ukraine, Kardinali Sandri amekazia umuhimu wa kudumisha mchakato wa uekumene unaofumbatwa katika sala, maisha ya kiroho, huduma na ushuhuda wa damu; ili kujenga na kuimarisha umoja wa Kanisa na taifa katika ujumla wake. Ametembelea na kukagua shughuli mbali mbali zinazoendeshwa na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki, Madhehebu ya Kigiriki nchini Ukraine hasa miongoni mwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi, tangu vita ilipofumuka nchini humo kunako mwaka 2014. Hali ya uchumi inaendelea kuwa mbaya zaidi, gharama ya maisha imepanda wakati hali ya maisha inazidi kudidimia kutokana vita ambayo imesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Kardinali Sandri amewashukuru wafanyakazi wa Shirika la Caritas kwa majitoleo yao. Wananchi wa Ukraine bado wana kumbu kumbu ya “Holomodor” yaani, njaa kali iliyotokea nchini humo kati ya mwaka1929 na mwaka 1933 na kusababisha watu milioni saba kufariki dunia! Kardinali Sandri amewakumbuka watu hawa na kuwaombea usingizi wa amani na mwanga wa milele uweze kuwaangazia. Amewataka wananchi wa Ukraine kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu na wala si kuta na tamaduni za kifo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kisawahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.