2017-07-14 15:34:00

Maaskofu Katoliki Sierra Leone: Kuelekea kwenye uchaguzi wa amani!


Wananchi wa Siera Leone wameanza safari kuelekea mchakato wa uchaguzi mkuu unaopaswa kuwa kweli ni huru, wa haki, wazi na wa amani na unaoaminika, ili ifikapo tarehe 7 Machi 2018, wananchi waweze kufanya maamuzi makubwa kwa kuongozwa na dhamiri nyofu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi,  ili hatimaye, waweze kuwachagua viongozi watakaoonesha dira na njia ya kufuata. Huu ni uchaguzi wa Rais, Wabunge na Viongozi wa Serikali za mitaa.  Maamuzi makini yanahitajika ili kuweza kujenga na kudumisha utamaduni wa utawala bora, amani na utulivu sanjari na kuheshimu tofauti msingi zinazoweza kujitokeza.

Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Sierra Leone limeandika Barua ya Kichungaji kwa kuitaka familia ya Mungu nchini humo kuanza safari kuelekea uchaguzi wa amani na unaoaminika. Maaskofu wanawahimiza wanasiasa na wapambe wao kuhakikisha kwamba, wanalinda na kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa wakati wote wa kampeni, zinazopaswa kuendeshwa kwa ustaarabu, ili wakati na baada ya uchaguzi mkuu, waweze kuridhika na matokeo yakayotolewa ili kuondokana na utamaduni wa kisingizio cha wizi wa kura!

Maaskofu wanavihimiza vyama vya siasa, wagombea urais, ubunge na serikali za mitaa kuheshimu mchakato mzima wa zoezi la kupiga kura, yaani kwa kuanzia katika uteuzi wa majina, uzinduzi wa kampeni; uchaguzi mkuu na utangazaji wa matokeo na baadaye! Walinde na kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, haki msingi za binadamu na utawala bora. Watambue kwamba uongozi ni huduma kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wote wa Sierra Leone na wala si kwa ajili ya mafao ya mtu binafsi pamoja na familia yake.

Katika mtazamo wa jumla, wagombea nafasi mbali mbali za uongozi wazingatie kwamba, wote ni wadau wanaotaka kuwahudumia wananchi wa Sierra Leone kwa nafasi mbali mbali na wala si maadui! Uchaguzi ni tukio la mpito, kamwe lisiwe ni sababu ya kupasuka na kuporomoka kwa tunu msingi zinazowaunganisha wananchi wa Sierra Leone. Maaskofu wanawataka wakleri na waamini katika ujumla wao, kuwa kweli ni chachu ya umoja na mshikamano wa kitaifa; wawe ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Wayatekeleze haya yote kwa njia ya maneno, lakini zaidi kwa matendo na kamwe wasiwe ni sababu ya kashfa ya utengano!

Baraza la Maaskofu Katoliki Sierra Leone, linamshukuru na kumpongeza Rais Ernest Bai Koroma kwa kutangaza mapema kabisa tarehe ya uchaguzi mkuu, ili kuwapatia wadau mbali mbali nafasi ya kuanza kujiandaa kwa ajili ya kukamilisha sehemu hii muhimu sana ya demokrasia na utawala bora. Haya ni mawazo chanya yanayoweza kusaidia kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano sanjari na kusaidia kukuza na kukomaza demokrasia ya kweli nchini Sierra Leone.

Maaskofu wanapenda kuchukua nafasi hii kuishukuru Jumuiya ya Kimataifa kwa kusimama bega kwa bega na wananchi wa Sierra Leone katika mapambano dhidi ya ugonjwa Ebola ambao kwa hakika umekuwa ni tishio kubwa kwa usalama na maisha ya watu wengi duniani. Sierra Leone inaweza kuwa na nguvu ya kuamua, kupanga na kutekeleza sera na mikakati yake, ikiwa kama itakuwa imeshikamana na kufungamana kama taifa! Mlipuko wa ugonjwa Ebola na Vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone, ni matukio ambayo yaliwatikisa wananchi wengi wa Sierra Leone, lakini, wakati  wa mapambano ya Ebola, tofauti za kidini, kikabila, kisiasa na kitamaduni, ziliwekwa pembeni, ili kufikia malengo makuu ya nchi!

Maaskofu wanawataka wananchi wa Sierra Leone kushikamana na kuwajibika kwa pamoja katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2018. Kanisa litaendelea kufuatilia mchakato mzima wa uchaguzi mkuu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kanisa halina chama, lakini waamini wake ni wanachama wa vyama mbali mbali nchini Sierra Leone; Kanisa linataka kulinda na kudumisha umoja wa kitaifa, haki, amani na upatanisho wa kweli. Kamwe wananchi wasikubali kununuliwa kwa ahadi za uwongo, bali kila mwananchi apige kura kwa kuwajibika na kwa kutumia busara kubwa, ili taifa liweze kuwapata viongozi: waadilifu, waaminifu, wachapakazi na wachamungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.