2017-07-14 15:02:00

Kumbu kumbu ya Miaka 6 ya Uhuru wa Sudan ya Kusini! Hali ni tete sana


Sudan ya Kusini ilijipatia uhuru wake tarehe 9 Julai 2011, ikawa ni kati ya mataifa machanga zaidi kujitawala baada ya kupiga kura ya maoni iliyowatenganisha na Sudan Kongwe! Lakini tangu wakati huo, hiki kimekuwa ni kipindi cha miaka sita ya mateso na mahangaiko ya wananchi wengi wa Sudan ya Kusini kutokana na vita ya wenyewe kwa wenywe inayosababishwa na uchu wa mali na madaraka; ukabila na udini usiokuwa na mashiko wala mvuto! Ni kipindi ambacho kumekuwepo na uvunjifu mkubwa wa haki msingi za binadamu na mauaji ya kutisha.

Askofu Barani Eduardo Hiiboro Kussala, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan katika barua yake ya kichungaji anasema, harakati ya kudai uhuru wa Sudan ya Kusini zilianza kunako mwaka 1950 na katika kipindi chote hiki watu zaidi ya milioni 2. 5 walifariki dunia na wengine milioni 4 kujikuta wakiwa ni wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum ndani na nje ya Sudan; hata baada ya uhuru, ukatili na unyama huu bado unaendelea.

Kumbu kumbu ya miaka 6 ya uhuru wa Sudan ya Kusini ziwe ni cheche za umoja na mshikamano wa kitaifa, kwa kuwakumbuka na kuwaombea mashuhuda wa taifa waliosadaka maisha yao kwa ajili ya kukoleza mchakato wa uhuru nchini Sudan ya Kusni kwa wakati huu na kwamba, uhuru ni zawadi ya kwanza kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa waja wake, zawadi inayopaswa kulindwa na kudumishwa na wote! Sudan ya Kusini inakabiliwa na ukata mkubwa wa fedha kwa ajili ya kuendeshea shughuli na huduma mbali mbali za Serikali kwa wananchi wake! Hakuna haki, amani wala matumaini.

Changamoto kwa familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini ni kujikita katika mchakato wa kutafuta na kujenga amani, ambayo kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu; amani inawajibisha na kwamba, wananchi hawana budi kuhakikisha kwamba, wanajikita katika mchakato wa kudumisha amani. Hii ni dhamana inayohitaji toba na wongofu wa ndani, kwani kuna Wakristo pia wanaoendelea kusababisha mateso na mahangaiko kwa jirani zao! Umefika wakati wa kuondokana na unafiki katika maisha kwa kuonesha upendo, umoja, udugu na mshikamano wa dhati kati ya wananchi wa Sudan ya Kusini. Waamini wawe ni mashuhuda na vyombo vya amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Umefika wakati anasema Askofu Barani Eduardo Hiiboro Kussala, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan: kusitisha mapigano na kuanza majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wote wa Sudan ya Kusini. Majadiliano haya yawe ni ya kitaifa yanayowaunganisha wote. Hali ya ukata ni kubwa sana nchini Sudan ya Kusini, Serikali iwe na ujasiri wa kutamka kwamba, imefilisika, ili kusaidia kuleta mageuzi makubwa yatakatoleta mabadiliko ya kiuchumi. Serikali ina deni kubwa sana ambalo haiwezi kulilipa kwa wakati. Wafanyakazi wake hawana mishahara. Kutangaza kufilisika kwa Serikali ni upendo na heshima kwa taifa, hata kama kuna fedheha ndani yake.

Familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini, haina budi kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Amani ni kikolezo muhimu sana cha shughuli za kilimo na uzalishaji mashambani na viwandani. Wananchi wa Sudan ya Kusini wajifunze kutatua migogoro na kinzani zao katika hali ya utulivu na amani. Imani kiwe ni kiungo muhimu sana kwa wananchi wa Sudan ya Kusini na kwamba, hii ni sehemu ya utambulisho wao kitaifa, inayoweza kuwaletea mabadiliko makubwa, kwa kujikita katika kulinda, kudumisha na kukuza haki msingi za binadamu; Injili uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida yanapomsibu kadiri ya mpango wa Mungu. Askofu Barani Eduardo Hiiboro Kussala, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan anahitimisha barua yake ya kichungaji kwa familia ya Mungu Sudan ya Kusini kwa kuwataka wananchi wawe na ujasiri wa kusimama kidete kulinda na kudumisha Injili ya familia; haki na amani; ukweli na uaminifu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Wananchi waendelee kusali kwa ajili ya kuombea haki, amani na utulivu, huko Sudan ya Kusini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.