2017-07-13 14:51:00

Malezi na majiundo endelevu ya Kipadre ni muhimu sana!


Baba Mtakatifu Francisko anasema,  majiundo ya awali na endelevu kwa ajili ya wakleri ni muhimu sana ili kuwawezesha kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa upendo na huruma ya Mungu kati ya watu wanaowahudumia. Anakazia umuhimu wa maisha ya sala tangu mwanzo ili hatimaye, Mapadre waweze kuchota nguvu ya kutekeleza dhamana na wajibu wao barabara, katika maisha na utume wa Kanisa. Wawe ni viongozi wanaojitaabisha kusoma Neno la Mungu, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha katika uhalisia wa maisha na utume wao. Maandiko Matakatifu yasomwe na kueleweka kwa msaada wa Roho Mtakatifu na chini ya uongozi wa Ualimu wa Kanisa, kwa kuzingatia yaliyomo katika Maandiko yote katika umoja wake; kwa kuheshimu Mapokeo hai ya Kanisa na mwishoni kwa kujali ulinganifu wa imani, yaani mshikamano wa kweli zote za imani!

Maaskofu wanahamasishwa na Baba Mtakatifu kuhakikisha kwamba, wanakuwa karibu sana na Mapadre wao vijana, hasa wanapoanza maisha na utume wao. Mapadre wawe ni watu wa sala, wanaotembea pamoja katika umoja, upendo na mshikamano, ili kutekeleza dhamana na wajibu wao katika maisha na utume wa Kanisa. Daima wajitahidi kujitakatifuza kwa njia ya maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Mapadre vijana waoneshe kipaji cha ubunifu katika mchakato mzima wa uinjilishaji, kwa kutumia vyema maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano, daima wakiwa tayari kusoma alama za nyakati!

Mapadre wanahimizwa na Mama Kanisa kuonesha ushuhuda wa: utii na uhuru kamili unaobubujika kutoka katika undani wa sakafu ya mioyo. Mapadre wawe tayari kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa ajili ya watu wa Mungu. Majiundo awali na endelevu ni muhimu sana kwa Wakleri katika maisha na utume wao, ili kuweza kutoa kipaumbele cha kwanza cha uwepo wa Mungu katika maisha yao; kwa kumpokea na kujenga uhusiano thabiti na Kristo Yesu.

Hii ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Maaskofu wanaotoka katika nchi zinazozungumza lugha ya Kiingereza kama sehemu ya malezi endelevu katika maisha na wito wa Kipadre. Yesu anawataka wafuasi wake kujisadaka bila ya kujibakiza ili kujenga pamoja naye mahusiano ya nguvu yanayoshinda mahusiano na mafungamano ya udugu wa damu na familia. Imani inapaswa kumwilishwa katika maneno na matendo yanayojikita katika kanuni maadili na utu wema, lakini zaidi kwa njia ya mafungamano ya dhati na Kristo Yesu.

Mwelekeo huu utawawezesha wakleri kuwa ni vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Maaskofu katika maisha na utume wao, watambue kwamba, wao ni walezi wanaopaswa kuwasaidia watu wa Mungu kujenga na kudumisha uhusiano wa dhati na Mwenyezi Mungu katika maisha yao: kiroho na kimwili. Mafungamano yote haya yapanie kujenga na kudumisha ari na moyo wa huduma kwa Kanisa la Kristo, tayari kujimimina kama kimiminika kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo.

Kardinali Beniamino Stella, anawataka Wakleri kujenga na kudumisha maisha yao mintarafu mantiki ya Fumbo la Msalaba, kwa kujisadaka bila kujibakiza kila siku ya maisha; kwa kushinda kishawishi cha kutaka kumezwa na malimwengu na badala yake, kutumia nguvu ya upendo ulioko ndani mwao kwa ajili kuwahudumia jirani zao. Hapa kuna haja ya kuwafunda wakleri watakaojisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo; Mapadre wenye huruma na mapendo, wanaotaka kuwatibu na kuwaganga waamini wao kwa njia ya mafuta ya faraja na divai ya matumaini. Kwa njia hii, Wakleri watakuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili kwa watu wanaowahudumia!

Kardinali Stella anawataka Wakleri kumjifunza Kristo Yesu kwa ukamilifu zaidi kutoka katika shule yake, ili waweze kuguswa na mambo msingi aliyopatia kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wake! Yaani upendeleo kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Hii ni huduma inayomwilishwa katika ukarimu, ukweli na upendo dhabiti! Haya ndiyo mambo msingi ambayo Maaskofu wanapaswa pia kuhakikisha kwamba, wanawarithisha majandokasisi wanaojiandaa kujisadaka kama Mapadre. Msisitizo huu umebainishwa kwa kina zaidi katika Mwongozo wa Malezi ya Kipadre uliochapishwa hivi karibuni na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri unaojulikana kama “Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis” yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre”. Kumbe, mwongozo huu unapania kuboresha kwa kiasi kikubwa maisha na utume wa Kipadre. Wote wanahusika na wala hakuna mtu awaye yote anayetengwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.