2017-07-13 15:33:00

Janga la karne ya 21: Dini bila Roho Mtakatifu; Ukristo bila Kristo!


Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, Katika Zaburi 50,7 tunasoma hivi: – sikia ewe taifa langu, ninasema nawe, Israeli, nataka kukushuhudia; ndimi niliye Mungu, Mungu wako.  Katika taifa la Israeli – neno lililotamkwa au kuandikwa lilikuwa na nguvu kabisa ya kiutendaji. Neno lilisimama badala ya aliyelitamka – kasema fulani au mamlaka fulani na likishatamkwa kinachofuata ni utekelezaji. Kama neno la mtu au kutoka mamlaka fulani lilipewa uzito kiasi hiki, fikiria juu ya nguvu ya Neno la Mungu. Kinachoweza kuzuia tu neno la Mungu ni sikio lililokufa. Kinyume chake tunaambiwa kuwa aliyesikia neno la Mungu anapata uzima wa kimungu. Inaeleweka kuwa mwanadamu mwenye masikio atadaiwa pia matumizi mazuri ya kiungo hiki cha mwili. Kinyume chake chake ni sawa na kinyago. Katika Zaburi 115 – tonaona hili – vinyago vina midomo lakini havisemi, vina masikio lakini havisikii …… wenye masikio tunaonywa tusiishie kuwa kama vinyago.

Tunaweza kusema ili watu wasikie habari njema ni lazima kuelewa na pia kinyume chake kwamba watu hawawezi kuelewa neno la Mungu bila kumkubali na kumpokea Mungu katika maisha yao. Hivyo ipo wazi katika somo la 1. Nabii Isaya anaamini katika Neno la Mungu na imani hiyo anawashirikisha watu wa Mungu. Naye Nabii Yeremia anashududia upendo wake kwa neno la Mungu akisema - Yer.15;16 – palipopatikana maneno yako, niliyatafuna; neno lako lilikuwa furaha yangu na shangilio la moyo wangu. Maana nimeitwa kwa jina lako,  ee Bwana, Mungu wa majeshi.

Tunaendelea kuona katika somo hili la kwanza kuwa Neno la Mungu ni kama mvua, inaboresha maisha. Katika sura 40-55 ya kitabu cha Nabii Isaya – Isaya wa pili – mwandishi anaandika neno hili – taifa la Israeli likiwa utumwani – katika somo hili la leo tunaona habari juu ya ujumbe wa furaha na matumaini kwa walio utumwani, katika nchi ya kigeni. Anatumaini kuwa neno hili litaleta faraja kwao. Ndiyo matumaini yake. Na kweli taifa lilitoka utumwani baada ya kusikia maneno na kilio cha manabii. Wakamgeukia Mungu, wakaacha uasi wao, wakawa huru tena. Hapa inaonekana wazi haja ya mtu wa Mungu, atakayesema neno la Mungu ili watu waamini, wasikie. Katika waraka wa Mtume Paulo kwa Rum. 10: 14-15 – tunasoma kuwa injili haina budi kutangazwa na wote. Katika sehemu hii ya maandiko tunaona kuwa ili wamwite : ni lazima wamwamini ; ili wamwamini ni lazima kusikia; ili wamsikie lazima awepo muhubiri; ili wahubiriwe ni lazima wapelekwe.

Neno la Mungu ni lazima litangazwe na kushuhudiwa kwa wote. Katika Injili ya leo tunasikia habari ya mpanzi na mbegu. Mbegu zimeanguka njiani, mwambani, katika miiba na kwenye udongo mzuri. Katika maeneo matatu ya kwanza hakuna matunda ila katika eneo la nne mavuno mengi yanapatikana. Hapa tunapata kiini cha ujumbe wa Yesu ambao ni habari ya ujio wa ufalme wa Mungu, yaani mavuno mengi. Maisha ya Kanisa na wanakanisa – yanapitia katika maeneo mbalimbali. Sisi tulioko hapa yafaa kujiuliza maisha yetu yako eneo gani sasa. Mbegu ndo ujumbe wa Neno. Ni Neno la Mungu lililokuja kwetu kwa njia ya Kristo.

Mfano wa mpanzi na mbegu katika Injili ya leo wahitaji pia ufahamu kama wa Isaya na watakatifu wote wa Mungu. Ujumbe huu wa Mungu ni mwaliko kwetu sisi tuishi mafundisho kwa imani, mengine yote tutayapata mbinguni. Hakika majibu ya maswali mengine hatutayapata hapa duniani. Jibu  kamili ni fundisho takatifu kama hili la leo alilotuachia Yesu, anatuhakikishia ujio wa ufamle wa Mungu na upatikanaji wa mavuno, sisi tufungue mioyo yetu kwa Mungu. Tukilinganisha maisha yetu na udongo twaona tofauti moja kubwa; udongo hauwezi kujibadilisha wenyewe; mtu anaweza kujibadili/kubadilikia. Swali kuu na la msingi: SASA TUTABADILIKAJE?

Mwandishi mmoja anatumia fundisho la Nabii Nathan  kwa Mfalme Daudi – 2Sam. 12,13 - kama fundisho tosha. Nathan anamweleza na kumkaripia Daudi. Daudi anatubu. Baada ya fundisho la Nathan, Daudi anakiri kumfanyia Bwana dhambi - anatubu. Tusiposikia neno la Mungu – halitatoa mavuno. Ili neno lipokelewe na ili litende kazi tarajiwa, sisi hatuna budi kuchukua nafasi ya ile mbegu iliyotoa mazao. Hatuna budi kuwa ule udongo mzuri. Jenerali William Booth alisema wakati fulani kuwa anadhani janga kubwa la karne ya 20 ni hili:

  1. Dini bila roho mtakatifu
  2. Ukristo bila Kristo
  3. Msamaha bila uongofu
  4. Maadili bila Mungu
  5. Mbingu bila motoni.

Ndugu zangu, Mungu hana mdomo – mdomo wake ni manabii wake na pia ndo sisi leo. Katika 2 Pt. 1:21tunasoma maneno haya – kwa maana unabii hautokei kwa hiari ya mwanadamu, bali watu wenye kuongozwa na Roho Mtakatifu husema juu ya Mungu. Na katika Yoh.. 8,43 – tunasoma hivi; mbona hamwelewi nisemayo? Ni kwa sababu hamwezi kusikiliza neno langu. 

Jibu la swali ni kwa nini wengine wanaelewa na wengine hawaelewi - ni kwa sababu hawataki kuelewa Neno la Mungu. Bila shaka tafakari ya leo inagusa wengi – wanaofundisha/wanaofundishwa na yale wanayofundisha. Mfano wa mpanzi leo katika somo la Injili unatoa changamoto kubwa kwetu. Tutafakari tena leo vizuri juu ya nguvu ya neno la Mungu – kile tukijuacho kuhusu neno la Mungu na jinsi tunavyofikisha ujumbe huo katika ulimwengu wetu huu. Hatuna budi kutafakari sana kile tunachotamka/kusema katika sala, matumizi sahihi ya maneno,  uzito wa kile tutamkacho, kama yanabeba ujumbe wa Mungu. Je, sisi wakristo maneno yetu tunayoyatamka yanabeba ujumbe gani? Tunaambiwa kuwa tukiamini tutakuwa kama ule udongo mzuri. Mbegu ni Neno la Mungu, Kristo ni mpanzi na mavuno ni wale waliolisikia hilo neno. Katika kuitika ujumbe wa Neno la Mungu leo, tutafakarishwe tena na ile sheria ya dhahabu ya Mtakatifu Paulo katika Efe. 4:29 – neno baya lisitoke midomoni mwenu. Maneno yenu yawe mema, yaweze kuwainua watu panapofaa na kuwapatia neema wenye kusikiliza.

Tumsifu Yesu Kristo.

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.
All the contents on this site are copyrighted ©.