2017-07-13 14:31:00

Familia ni dawa madhubuti ya changamoto mamboleo!


Umuhimu wa maisha na utume wa familia katika ulimwengu mamboleo unafafanuliwa vyema na Maandiko Matakatifu sanjari na Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa kutambua kwamba ni katika familia ndipo mtu hujifunza upendo na uaminifu kwa Mungu na sababu ya kuupokea na kuumwilisha upendo na uaminifu huu kwa watu wengine! Familia ni Jumuiya ya kwanza katika jamii ya asili na kwamba, ina haki na wajibu wake katika jamii. Familia ni tabernakulo ya kwanza ya Injili ya uhai na utakatifu wa maisha; ni mahali pa malezi na makuzi ya watu: kiroho na kimwili; hapa watu wanajifunza kupenda na kupendwa; kusamehe na kusamehewa.

Familia ni mahali pa kukuza na kudumisha, utu, heshima na maadili. Kumbe, wadau mbali mbali wanapaswa kuziwezesha familia ili ziweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake ndani ya jamii kwani familia ni dawa madhubuti katika mchakato wa kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoibuliwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia! Jamii mamboleo inakabiliwa na changamoto kibao, zinazofumbatwa katika mmong’onyoko wa maadili na utu wema; ubinafsi na uchoyo pamoja na hali ya kukata na kukatishana tamaa ya maisha.

Kardinali  Josip Bozanic, mwakilishi maalum wa Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 650 tangu Papa Urbano V kunako mwaka 1367 alipowapatia mahujaji kutoka nchini Croatia, Picha ya Bikira Maria walipokuwa wanatembelea Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto, amekazia umuhimu wa familia kama dawa makini inayoweza kuganga na kutibu changamoto mamboleo, ikiwa kama familia itathaminiwa na kupewa uzito wa pekee kama inavyostahili. Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ni mfano bora wa kuigwa na familia sehemu mbali mbali za dunia.

Familia Takatifu ilikumbana na matatizo na changamoto mbali mbali pasi na kukata tamaa, changamoto kwa familia kuhakikisha kwamba, zinakuza na kudumisha fadhila za kikristo na utu wema; familia zijitahidi kuthamini na kufanya kazi kwa: bidii, juhudi na maarifa kwa kutambua kwamba, kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu! Mtakatifu Yosefu anawafundisha watu umuhimu wa kupenda na kuheshimu kazi. Matatizo, shida na magonjwa ni sehemu ya historia ya maisha ya familia! Kumbe, wanafamilia wajenge utamaduni wa kujiaminisha mbele ya Mungu kwa kukimbilia ulinzi na tunza yake ya kibaba badala ya mwelekeo wa sasa wa watu kukata na kukatisha tamaa, kiasi kwamba, wanajikuta wakitumbukia na hatimaye, kumezwa na malimwengu pamoja na imani za kishirikina!

Kardinali  Josip Bozanic amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanajenga ujasiri, amani na utulivu wa ndani kama nyenzo msingi za kukabiliana na changamoto mamboleo, kama alivyofanya Bikira Maria kwa kuyahifadhi yote katika sakafu ya moyo wake. Waamini wamwombe Bikira Maria ili aweze kuwasaidia kusoma alama za nyakati na kuitafsiri historia katika maisha yao katika mwanga wa Injili ya Kristo. Familia ya Mungu nchini Croatia ina utamaduni na mapokeo ya kujiaminisha kwa Bikira Maria wa Trsat, Madhabahu yanayoheshimiwa sana na familia ya Mungu nchini Croatia. 

Kardinali  Josip Bozanic amekazia umuhimu wa ukimya na sala katika maisha ya waamini; umuhumu wa familia kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao, bila kupiga makelele au kujitafutia umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko! Amewataka waamini kujenga na kudumisha ari na moyo wa sala; kwa kufanya tafakari ya kina ili kumsikiliza Mwenyezi Mungu anayezungumza nao kutoka katika undani wa dhamiri zao nyofu. Madhabahu ya Bikira Maria Trasat nchini Croatia ni kumbu kumbu muhimu sana kwa tafakari ya Fumbo la Umwilisho, yaani jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu anatenda kazi zake kwa kuwashirikisha binadamu.

Kimsingi, Mwenyezi Mungu anapenda kukutana na waja wake kila siku ya maisha yao, kumbe, waamini wajibidishe kukutana na Mungu kwa njia ya sala, Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na huduma makini kwa familia ya Mungu. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Mwenyezi Mungu ameingia na kufanya makazi katika historia na maisha ya binadamu, chachu inayopyaisha na kuboresha maisha ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.