2017-07-12 09:59:00

Kardinali Maung Bo: Dumisheni amani, ili demokrasia iweze kutawala!


Myanmar ni nchi inayopitia kipindi kigumu sana katika historia yake. Raia wa taifa hilo wana maumivu makali ya mkuki wa moyo kufuatia hali tete ya kuporomoka kwa demokrasia nchini humo, kiasi cha raia kujiona wakitumbukia kwenye giza totoro na kuhisi kukosa pa kukimbilia wala kujibanza. Kwa hali hiyo, nchi ya Myanmar inahitaji msaada wa kimataifa, ili kusaidia kuvuka hali hiyo tete ya kidemokrasia nchini mwao, anasema Kardinali Charles Maung Bo, Askofu mkuu wa Jimbo la Yangon nchini Myanmar.

Taarifa iliyotolewa na Kamati ya Haki msingi za Binadamu, ya Umoja wa Mataifa, mnamo tarehe 3 Februari 2017, inaonesha hali ya kusikitisha sana ya kukandamizwa kwa haki msingi za binadamu kwa raia wa nchi ya Myanmar. Vyombo vya ulinzi na usalama vimeonesha kuwatendea kwa ukatili sana raia wa nchi hiyo, hasa katika maeneo ya Rakhine, hali inayoonesha unyama mkubwa usioelezeka na ngumu hata kuamini kama mwanadamu anaweza kumtendea ndugu yake kwa namna hiyo. Kardinali Charles Maung Bo anasema, hiki ni king’ora kinachomwalika kila binadamu kwa nafasi yake kuingilia kati ili kutetea haki msingi za wananchi wa Myanmar.

Katika miaka mitano iliyopita Myanmar imeshuhudia mabadiliko makubwa ambayo yamekuwa ni chanya kwa maendeleo ya nchi hiyo na kwa mahusiano na nchi zingine. Imekuwa ni miaka ya mapambazuko ya matumaini makubwa katika nyanja za uchumi, uhuru wa habari, maendeleo ya kijamii, na ukuaji kidemokrasia. Mwito wa Kardinali Charles Maung Bo, ni kuhakikisha kwamba mapambuzuko ya miaka hii mitano yasiishie kuwa ni matumaini batili. Hivyo wanaopandikiza chuki dhidi ya watu wa kabila na dini tofauti na kupelekea ghasia na nyanyaso kati ya raia wa Myanmar, wanapaswa kusimamishwa mara moja, na hali hiyo isijirudie tena.

Hali ya uvunjwaji haki inaonekana pia katika maeneo ya Kachin na Shan, kwa namna ya pekee baada ya wachungaji wawili wa kabila la Kachini, Nawng Latt na Gam Seng kukamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi bila kufahamu uhalali wa tuhuma zao. Kardinali Charles Maung Bo, anaiomba serikali ya Myanmar kuwaachilia wachungaji hao, kusimamisha uonevu wa kijeshi dhidi ya wakazi wa Rakhine, Kachin na Shan, na kurejesha uhuru wa kujieleza katika mitandao jamii, haki za kufikia taasisi za huduma za binadamu na kamati za haki msingi za binadamu, kwani amani inawezekana pale tu panapokuwa na haki.

Kardinali Charles Maung Bo ametahadharisha pia kwamba, mauaji ya U Ko Ni, Wakili wa kiisalmu nchini Myanmar, yamekuwa hatua nyingine nyuma inayopingana na matumaini ya kutengeneza Myanmar yenye amani na demokrasia ya kweli. Ni mwaliko wa Kardinali Maung Bo: Jumuiya ya kimataifa iingilie kati ili kusaidia kutetea haki, kutafuta amani nchini humo, na kwamba Umoja wa Mataifa usichezeshe kope katika hili, bali uhakikishe jicho lipo makini ili kila mmoja atendewe haki na matumaini ya Myanmar yasizime moto. Kanisa nchini Myanmar limeuweka mwaka 2017 kuwa ni mwaka wa Amani, na linajitosa kuweka mchango wake ili kweli amani idumu nchini humo.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican. 
All the contents on this site are copyrighted ©.