2017-07-11 16:06:00

Misingi ya Umoja wa Jumuiya ya Ulaya inafumbatwa katika Ukristo!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, anaikumbusha familia ya Mungu Barani Ulaya kwamba, inao utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho na wapekee duniani; hii ni amana ambayo inapaswa kupyaishwa kwa ari na moyo mkuu. Huu ni utajiri unaofumbatwa katika maisha na utume wa Mtakatifu Benedikto mkuu, Abate na Msimamizi wa Bara la Ulaya, anayekumbukwa na wengi kwa kauli mbiu yake “Ora et Labora”, yaani Sala na Kazi; mambo msingi yanayompatia mwamini utimilifu wa maisha yake. Anakumbukwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 11 Julai.

Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE katika mahojiano maalum na Radio Vatican anawaalika viongozi wa Umoja wa Ulaya, kumsikiliza kwa makini Baba Mtakatifu Francisko na kuzifanyia kazi changamoto zinazotolewa naye kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ndani na nje ya Jumuiya ya Ulaya. Ni maneno yanayopaswa kubisha hodi katika sakafu ya mioyo na akili za viongozi wa Jumuiya ya Ulaya ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto pevu.

Amana na utajiri wa Jumuiya ya Ulaya vitumike kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, daima wakiongozwa na maono ya waasisi wa Jumuiya ya Ulaya, badala ya kuonekana kana kwamba, wamechoka na kuanza kujitafuta wenyewe hali inayoonesha mpasuko katika Jumuiya ya Ulaya kwa kutozingatia mambo msingi yanayowaunganisha zaidi. Kardinali Bagnasco anakaza kusema, hali hii ni matokeo ya Jumuiya ya Ulaya kukosa utambulisho, hali inayowakatisha tamaa wananchi wengi Barani Ulaya, kiasi cha kutaka kujitenga na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya. Utambulisho na mizizi ya Umoja wa Ulaya inapata chimbuko lake katika Ukristo na kwamba, hii si hotuba ya kisiasa au ya kitaaluma, bali ni ukweli wa mambo kwamba, Jumuiya ya Ulaya inaendelea kumong’onyoka na kupoteza dira na utambulisho wake unaofumbata mizizi ya Kikristo. Jumuiya ya Ulaya inaanza kumezwa mno na ubinafsi pamoja na uchoyo kinyume kabisa cha fadhila ya ukarimu, upendo na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mataifa.  Ulaya inapaswa kuendeleza majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Utambulisho wa Jumuiya ya Ulaya unafumbatwa katika majadiliano ya kitamaduni na maisha ya kiroho!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.