2017-07-11 15:45:00

Mh. Padre Jesùs Ruiz Molina, M.C.C. ateuliwa kuwa Askofu msaidizi


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Jesùs Ruiz Molina, M.C.C, kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bangassou, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Askofu mteule Jesùs Ruiz Molina kutoka Shirika la Wacomboni, alizaliwa tarehe 23 Januari 1959 huko La Cueva de Roa, Jimbo Katoliki la Burgos, nchini Hispania. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa, kunako tarehe 11 Julai 1987 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Na tarehe 24 Aprili 1988 akaweka nadhiri zake za daima kwenye Shirika la Wacomboni.

Tangu wakati huo, ametekeleza dhamana  na utume wake wa Kipadre kama mhamasishaji mkuu wa shughuli za kimissionari nchini Hispania tangu mwaka 1987 hadi mwaka 1989. Akateuliwa kuwa Paroko usu na baadaye Paroko kati ya mwaka 1990 hadi mwaka 1995 katika Parokia ya Immaculèè Conception, Bedjondo, Jimbo Katoliki la Sahr, nchini Chad. Kati ya mwaka 1996 hadi mwaka 2008 akateuliwa na viongozi wake wa Shirika kuwa mlezi wa wa wapostulanti wa Shirika la Comboni na mratibu wa waamini walei wenye kujishikamanisha na Shirika la Wacomboni.

Kati ya Mwaka 2002 hadi mwaka 2008 alichaguliwa kuwa Padre mkuu wa Kanda mpya ya Wacomboni nchini Chad. Mwaka 2008 akaenda kujinoa zaidi kwenye Chuo Kikuu cha Salamanca, Hispania. Mwaka 2009 akapelekwa kwenye Parokia ya Mtakatifu Anna huko Dekoa, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Baadaye akateuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Moungoumba, Jimbo Katoliki la M’Baiki, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Na kati ya mwaka 2013 hadi mwaka 2015 alikuwa ni mshauri wa Shirika la Wacomboni kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.