2017-07-10 09:13:00

Papa Francisko: Nendeni nyote kwa Yesu atawapumzisha na kuwafariji!


Njooni kwangu ninyi nyote wenye kusumbuka na kuelemewa na mizigo nami nitawapumzisha, ni mwaliko unaotolewa na Kristo Yesu kwa kila mtu na wala hakuna mtu awaye yote anayeweza kujisikia kwamba, ametengwa. Yesu, mchungaji mwema, anatambua jinsi ambavyo maisha ni magumu na mazito kiasi cha watu kuteseka sana! Kuna watu ambao wamekatishwa tamaa ya maisha, wana madonda ya historia iliyopita; wanaelemewa na mambo mazito wanayopaswa kuyabeba katika maisha kwa wakati huu; wana wasiwasi na mashaka kwa ajili ya maisha yao kwa siku za mbeleni.

Katika magumu na changamoto zote hizi, Kristo Yesu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kupiga moyo konde na kuanza kuchukua hatua ya kumwendea! Kosa kubwa linalotendwa na watu wengi ni kubaki mahali ambapo wamekosea, kiasi hata cha kushindwa kuchukua hatua madhubuti na kuanza kutembea na kutoka katika hali kama hii! Changamoto hii si rahisi kuitekeleza, kwani yataka moyo kweli kweli! Pale mwanadamu anapoelemewa na giza moyoni anapata kishawishi cha kubaki peke yake na kuendelea kumeza moyoni mwake yale yanayomtesa na kumsumbua. Huu ndio ule muda wa kuwanyooshea watu wengine vidole na kuonesha jinsi ambavyo ulimwengu umegeuka kuwa ni tambara bovu!

Katika mazingira kama haya, watu wanajikuta wakiwa wanaogelea katika mazoea hata yale huzuni na simanzi moyoni, kiasi hata cha kujenga msingi wa maisha ya watu! Hili ni jambo baya sana katika maisha, lakini ndio ukweli wenyewe. Lakini, Kristo Yesu anataka kuwang’oa na kuwaondoa katika utelezi huu wa maisha na kuwaweka mahali salama, ndiyo maana katika Injili ya Jumapili ya XIV ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa anawaita watu wote akisema, “Njooni kwangu ninyi nyote”. Anaonesha dira na mwelekeo mpya wa maisha. Anataka kuanza kujenga tena mahusiano mapya kwa kushikamana na wale wote waliovunjika moyo, ili kuwaonjesha upendo wake usiokuwa na kifani!

Hii ni tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 9 Julai 2017 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican! Baba Mtakatifu anakaza kusema, haitoshi kutoka katika undani wa mtu, bali mtu mwenyewe anapaswa kufahamu mahali anapoelekea. Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna mambo ambayo yanatoa ahadi ya kutaka kuwapumzisha watu na mahangaiko yao ya kila siku; kwa kuwapatia amani na utulivu wa ndani; kwa kuwajalia faraja na burudani, lakini yote haya ni kama “moto wa mabua” anasema Baba Mtakatifu yanapita na kutoweka mara! Mtu anaendelea kubaki katika upweke wake wa maisha.

Kristo Yesu anawaalika kumwendea, ili aweze kuwasikiliza na kuwapatia faraja, kama ambavyo watu wengi wanafanya wanapokumbana na magumu ya maisha, kwa kuwaendea marafiki au hata wataalam jambo ambalo ni jema kabisa, lakini Baba Mtakatifu anakaza kusema, kamwe wasimsahau Kristo Yesu anayeweza kuwapatia utulivu na amani ya ndani kabisa! Jambo la msingi ni kujiaminisha kwake na kumsimulia historia ya maisha na kuwaweka watu na matukio mbali mbali katika ulinzi na tunza yake. Inawezekana kabisa katika hija ya maisha hapa duniani, kuna maeneo ambayo yamefichwa mbele ya Yesu na kuendelea kubaki katika giza la moyo na maisha, kwani hayajawahi kuona mwanga wa Kristo. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hapa kila mtu anayo historia ya maisha yake.

Kumbe, huu ni wito na mwaliko wa kumwendea Yesu ili kumshirikisha hayo yanayosumbua moyo; ni wakati wa kuwaendelea Wamissionari wa huruma ya Mungu waliowekwa na Mama Kanisa ili kuwaonjesha watu huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao; ni wakati wa kuwaendea Mapadre, lakini zaidi ni kumwendea Kristo mwenyewe na kumsimulia ana kwa ana pasi na kigugumizi! Yesu anawatia shime watu wote kutokatishwa tamaa na mizigo ya maisha, wasikate tamaa kutokana na woga, wasi wasi na mizigo ya dhambi, bali wote wamwendee kwani atawapumzisha.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, Yesu anawasubiri watu wote, si kuwapatia ufumbuzi wa matatizo kwa njia ya mkato, bali kwa kuwajalia nguvu na uthabiti wa moyo ili kukabiliana na changamoto zao za maisha, Yesu hawaondolei mizigo wala Misalaba ya maisha, bali anawasaidia kuibeba pamoja nao na hivyo mizigo na Misalaba hii inakuwa ni miepesi, kwani Yesu ni faraja na kimbilio la watu wake. Yesu anapoingia katika maisha ya mtu, amani na utulivu wa ndani vinapatikana hata kama mtu anakabiliana na mahangaiko makubwa kiasi gani!

Baba Mtakatifu anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwendea Kristo Yesu kwa kumpatia nafasi katika sakafu ya mioyo yao na muda wa kuweza kukutana katika sala, tafakari ya kina ya Neno la Mungu, ili kuonja na kugundua msamaha unaozima na kutuliza njaa ya maisha kwani Yesu mwenyewe ni mkate wa uzima, ulioshuka kutoka mbinguni! Kwa njia hii, watu watajisikia kweli wanapendwa na kufarijiwa na Yesu mwenyewe. Jifunzeni kutoka kwake ili kupata faraja katika maisha!

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, wakati huu, wa majira ya kiangazi, watu wengi wanakwenda likizo ili kujipumzisha, lakini Kristo Yesu ndiye anayeweza kuwapatia pumziko la kweli. Bikira Maria awasaidie waamini katika kukabiliana na changamoto hii, kwani daima anawapatia tunza yake ya kimama pale wanapojisikia kuwa wanaelemewa na mizigo, tayari kuwapeleka kwa Yesu. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewapongeza waamini na mahujaji waliofika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuungana naye kwa tafakari na sala ya Malaika wa Bwana licha ya jua kuwa kali kiasi cha kutishia maisha ya watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.