2017-07-10 11:22:00

Jengo la ghorofa laporomoka na kusababisha watu 8 kufariki dunia


Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa nne huko Torre Annunziata, Napoli, Kusini mwa Italia, tarehe 8 Julai 2017 na kusababisha watu 8 kupoteza maisha. Katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Kardinali Crescenzio Sepe, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Napoli, Baba Mtakatifu anasema, anapenda kuwahakikishia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake, wale wote walioguswa na kutikiswa na maafa haya.

Anawaombea marehemu ili waweze kupata raha ya milele na mwanga wa milele uweze kuwaangazia, ili wapumzike kwa amani. Anawaombea huruma na faraja wale wote waliojeruhiwa katika tukio hili na mwishoni, anapenda kutoa baraka zake za kitume kama alama ya uwepo wake wa karibu kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Napoli, Italia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.