2017-07-10 10:35:00

Angalisho juu ya utengenezaji wa hostia na divai kwa ajili ya Ibada!


Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko limewaandikia barua Maaskofu mahalia na viongozi wakuu wenye mamlaka kadiri ya kanuni na sheria za Kanisa kuhusu umuhimu wa kuhakikisha kwamba, maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yanatekelezwa kadiri ya mwongozo wa Mama Kanisa. Maaskofu ni waadhimishaji na wagawaji wakuu wa Mafumbo ya Kanisa; wao wanaratibu, wanaendeleza na kulinda maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa kadiri ya maeneo yao. Ni wajibu wao kuhakikisha kwamba, hostia na divai inayotumika kwa ajili ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu inakidhi viwango vinavyokubalika na Kanisa. Wanapaswa pia kuwa makini na wale wanaotengeneza hostia na divai kwa ajili ya maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa.

Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa linakumbusha kwamba, hadi hivi karibuni, kulikuwa na Jumuiya za kitawa zilizokuwa na jukumu la kutengeneza hostia na divai kwa ajili ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Lakini leo hii kutokana na biashara huria, hostia na divai zinapatikana hata katika maduka makubwa makubwa na kwa nchi zilizoendelea inaweza kununuliwa kwa njia ya mtandao.

Ili kuweza kuwa na uhakika wa ubora unaotumika kwa ajili ya kutengenezea hostia na divai kwa ajili ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Maaskofu mahalia hawana budi kutoa cheti cha ubora kwa wale wanaohusika, ili kuondoa wasi wasi unaoweza kujitokeza kwa waamini wakati wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Maaskofu mahalia watoe vigezo muhimu vinavyohitajika kwa ajili ya kutengeneza hostia na divai kwa ajili ya Ibada ya Misa Takatifu na kwamba, watengenezaji hawa wanapaswa kuheshimu maagizo haya kama yanavyofafanuliwa na Kanuni, Sheria za Kanisa na Mwongozo wa Maadhimisho ya Sakramenti ya Wokovu uliotolewa kunako tarehe 25 Machi 2004.

Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa linakumbusha kwamba, unga wa ngano unaotumika kwa ajili ya kutengeneza hostia ni ule uliotengenezwa hivi karibuni ili kutunza ubora wa Ekaristi Takatifu. Ni kosa kubwa kuchakachua hostia zinazotumika kwa ajili ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa kuongeza sukari au asali. Hostia za Ibada ya Misa Takatifu zitengenezwe na watu waaminifu, waadilifu na wenye ujuzi unaokubalika. Divai inayotumika kwa ajili ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu haina budi kuwa ni ile ya kawaida, isiyochakachuliwa na kwamba, inaweza kutunzwa kwa muda mrefu. Divai inayotumika kwa Misa ijulikane mahali inapotoka ili kuwa na uhakika wa divai inayotumika kwa ajili ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Mabaraza ya Maaskofu Katoliki yanahimizwa kufanya rejea tena kwenye barua iliyotolewa na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa ya Mwaka 2003 kuhusu kanuni na sheria zinazoongoza utengenezaji wa hostia na divai inayotumika kwa ajili ya maadhimisho ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Watengenezaji na wauzaji wa hostia na divai inayotumika kwa ajili ya maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa wanakumbushwa kwamba,  kazi yao ineelekezwa zaidi katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, Sadaka ya Mwili na Damu ya Kristo Yesu, kumbe, wanapaswa kuwa waaminifu, waadilifu na watu wanaowajibika barabara.

Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia yanaweza kutoa mwongozo utakaotumika katika maeneo yao kwa kuzingatia utakatifu wa Mafumbo yanayoadhimishwa na Mama Kanisa. Ikionekana inafaa, baadhi ya Mashirika ya kitawa yapewe dhamana na wajibu wa kutengeza hostia na divai kwa ajili ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi takatifu ili kuwa na uhakika wa mahali na ubora wa hostia na divai inayotumiwa na Mama Kanisa katika maadhimisho ya Mafumbo makuu ya Kanisa. Barua hii imetolewa na Kardinali Robert Sarah, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa pamoja na Askofu mkuu Arthur Roche, Katibu mkuu wa Baraza, wakati Kanisa lilipokuwa linaadhimisha Siku kuu ya Ekaristi Takatifu, tarehe 15 Juni 2017.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.