2017-07-08 16:45:00

WYD 2019: Wimbo rasmi wazinduliwa, vijana waanza kuufanyia mazoezi


Ilikuwa ni mwezi Julai, 2016 wakati wa kufunga rasmi maadhimisho ya Siku ya 33 ya Vijana Duniani sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa vijana, Baba Mtakatifu Francisko alipotamka rasmi kwamba,  maadhimisho ya Vijana kwa Mwaka 2019 yatafanyika nchini Panama kuanzia tarehe 22- 27 Januari 2019. Yataongozwa na kauli mbiu “Tazama mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema”.

Haya ni maneno kutoka katika Injili ya Luka ambayo pia yametumiwa na Katekista Abdiel Jimènez, mtunzi wa wimbo rasmi wa maadhimisho ya Siku ya 34 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019. Hivi karibuni, wimbo huu umezinduliwa rasmi na tayari vijana wa kizazi kipya wanaendelea kuufanyia mazoezi, tayari kuwashirikisha vijana wenzao kutoka sehemu mbali mbali za dunia furaha ya Injili katika maisha ya ujana!

Askofu mkuu Jose Domingo Ulloa Mendieta wa Jimbo kuu la Panama, anafafanua kwamba, wimbo huu unabeba maudhui yote ya maisha na utume wa Kanisa, ambamo waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria. Inafurahisha kuona kwamba, wimbo huu utaimbwa na vijana wa kizazi kipya, ili baada ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, waweze kutoka kifua mbele, tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa, kwa vile wamekutana na Kristo Yesu katika maisha yao kwa njia ya: Neno, Sakramenti na ushuhuda wa maisha ya Kikristo wenye mvuto na mashiko! Itakuwa ni changamoto kwa vijana wa kizazi kipya kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili aweze kuwafunda na kuwatumia kama vyombo na mashuhuda wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Katekista Abdiel Jimènez, mtunzi wa wimbo rasmi wa maadhimisho ya Siku ya 34 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 ni msomi kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Santa Maria la Antigua. Alipambanishwa na watunzi zaidi ya 50 na kati ya hizi, nyimbo tatu zikachaguliwa na hatimaye, wimbo mmoja uliobeba maudhui yote ukateuliwa baada ya kuchambuliwa “kama karanga” na Kamati tendaji ya Maadhimisho ya Siku ya 34 ya Vijana Duniani kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha wakauchagua wimbo wa Katekista Abdiel.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.