2017-07-08 09:07:00

Wazee washirikishwe katika mchakato wa maendeleo endelevu!


Maboresho ya afya yanaendelea kusaidia watu kuishi kwa muda mrefu zaidi ikilinganishwa na miaka kadhaa iliyopita. Idadi ya wazee duniani inaendelea kuongezeka siku hadi siku, kiasi hata cha kusababisha hali hii kuwa ni kati ya changamoto zinazoikabili Jumuiya ya Kimataifa. Haki msingi za wazee, utu na heshima yao ni mambo yanayopaswa kupewa msukumo wa pekee. Baba Mtakatifu Francisko anamshukuru Mungu kwa maboresho katika huduma ya tiba ya mwanadamu, lakini kwa bahati mbaya sana, sehemu kubwa ya jamii haijajiandaa kuwapokea na kuwaenzi wazee. Umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kuweka sera na mikakati itakayosaidia kuenzi maisha, utu na heshima ya wazee duniani!

Haya yamesemwa hivi karibuni na Askofu mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, alipokua anachangia mada kuhusu mambo msingi yanayopaswa kutendeka ili kuenzi mchango wa wazee katika ustawi na maendeleo ya jamii. Wazee ni watu wanaokabiliwa na: umaskini, hali mbaya ya afya, ulemavu; hali ya kutengwa na jamii. Ni watu ambao wanafanyiwa ghasia sana; hawana mawasiliano thabiti na kwamba, huduma ya afya wanayopewa ni hafifu sana, hali ambayo wakati mwingine inagumishwa na ukosefu wa lishe bora.

Wazee pia ni waathirika wakubwa wa majanga asilia, vita, kinzani na mipasuko ya kijamii; athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa na kwamba, si rahisi sana kuweza kufikiwa na huduma za dharura kutokana na masuala mtambuka! Askofu mkuu Bernardito Auza anaendelea kufafanua kwamba, kutokana na changamoto zote hizi, kuna haja ya kutoa kipaumbele cha pekee cha huduma kwa wazee, kwa kuwapatia fursa ya kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ustawi na maendeleo endelevu. Hii inatokana na ukweli kwamba, wazee kwa kiasi kikubwa wanatengwa na jamii na wala hawapewi nafasi ya kushirikisha hekima, ujuzi na maarifa yao, kwani wazee ni amana ya hekima na busara kwa watu wao!

Wakati mwingine, sera, maamuzi mbele na mitindo ya maisha inaweza kupelekea kwamba, wazee wakajikuta wanatengwa, ingawa wakati fulani walikuwa ni kitovu cha familia na jamii katika ujumla wake. Kumbe, kuna haja ya kufanya tafakari ya kina, ili kuhakikisha kwamba wazee wana husishwa kikamilifu  kuchangia katika mchakato wa maendeleo endelevu ya watu wao na kamwe tija na mchango wao visilinganishwe na uwezo wao wa kimwili. Wazee wanapaswa kuhusishwa katika mchakato wa kupanga, kwani wanaendelea kuchangia katika masuala ya kiuchumi, soko la ajira pamoja na kufurahia maisha ya uzeeni kwa kuwa na uhakika wa usalama wa afya, malezi na majiundo endelevu.

Askofu mkuu Bernardito Auza anasema, kuna haja ya kuangalia kwa karibu zaidi kuhusu mchango wa wazee katika mchakato mzima wa maendeleo ya binadamu sanjari na kuzingatia mahitaji yao msingi. Wazee wagonjwa, walemavu, wapweke na waliopungukiwa ufahamu hawana tena nafasi ya kuzalisha na kutoa huduma, lakini ni kundi ambalo linahitaji kuangaliwa kwa umakini mkubwa. Wazee wanapaswa kupendwa na kuheshimiwa kwani hata katika mapungufu yao ya kibinadamu, bado wanaendelea kubaki ni binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wenye utu na heshima yao ambayo kamwe haiwezi kupungua kutokana na udhaifu wa kimwili.

Utandawazi wa kutowajali watu ni hatari sana anasema Baba Mtakatifu Francisko. Kumbe, kuna haja kwa wazee kuheshimiwa na kuthaminiwa na jamii inayowazunguka, kwa kuwajali na kuwaonesha mshikamano wa dhati. Utamaduni wa kifo unaokumbatiwa kwa njia ya kifo laini ni hatari sana kwa maisha ya jamii mamboleo, kwani dhana inayokumbatiwa hapa ni kuwaona wazee si mali kitu katika mchakato mzima wa maendeleo ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.