2017-07-08 15:41:00

Papa Francisko aridhia watumishi wa Mungu kadhaa kuendelea na mchakato


Baba Mtakatifu Francisko baada ya kukutana na kuzungumza na Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, ameridhia kwamba, waamini wanane ambao miujiza yao imetambuliwa rasmi na Kanisa waandikwe kwenye Kitabu cha Orodha ya Majina ya mchakato wa wenyeheri. Kanisa limetambua muujiza uliotendwa kwa maombezi ya Mtumishi wa Mungu Anna Chrzanowska, mwamini mlei aliyezaliwa kunako tarehe 7 Oktoba 1902 huko Varsavia, Poland na kufariki dunia tarehe 29 Aprili 1973 huko Cracovia, Poland.

Kanisa limetambua muujiza uliotendwa kwa maombezi ya Mtumishi wa Mungu Jesus Emilio Jaramillo Monslave, Askofu wa Jimbo la Arauca, aliyeuwawa kikatili kutokana na chuki za Imani mwaka 1989, huko Colombia. Mwingine ni Mtumishi wa Mungu Padre Pietro Maria Ramìrez Ramos aliyeuwawa kikatili tarehe 10 Aprili 1948 huko Colombia. Kanisa limetambua muujiza wa ushuhuda wa imani ulioneshwa na Askofu mkuu Ismaele Perdomo wa Jimbo kuu la Bogotà aliyezaliwa kunako tarehe 22 Februari 1872 na kufariki dunia tarehe 3 Juni 1950, huko Bogotà, nchini Colombia.

Mama Kanisa ametambua na kuridhia miujiza iliyotendwa na Mtumishi wa Mungu Luigi Kosiba, mwamini mlei aliyelizaliwa kunako tarehe 29 Juni 1855 huko Poland na kufariki dunia tarehe 4 Januari 1939 nchini Poland. Katika orodha hii, Kanisa limetambua muujiza uliotendwa kwa maombezi ya Mtumishi wa Mungu Paola wa Yesu Gil Cano, Muasisi wa Shirika la Watawa wa Wafranciscan wa Moyo Safi wa Bikira Maria, aliyezaliwa tarehe 2 Februari 1849 nchini Hispania na kufariki dunia tarehe 18 Januari 1913 huko nchini Hispania.

Katika orodha hii, Mama Kanisa ametambua na kuridhia muujiza uliotendwa kwa maombezi ya Mtumishi wa Mungu Maria Elizabeth Mazza, muasisi wa Shirika la Mitume wadogo wa Shule za Kikristo, aliyezaliwa tarehe 21 Januari 1886 huko Italia na kufariki dunia tarehe 29 Agosti 1950, huko Bergamo, nchini Italia. Kanisa linakiri muujiza uliotendwa kwa maombezi ya Mtumishi wa Mungu Maria Crocifissa wa upendo wa Mungu, muasisi wa Shirika la Mitume wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, aliyezaliwa kunako tarehe 23 Desemba 1892 na kufariki dunia tarehe 23 Mei 1973 huko Napoli nchini Italia.

Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 
All the contents on this site are copyrighted ©.