2017-07-07 14:59:00

Yesu Kristo anakupenda jinsi ulivyo anataka ushiriki utume wake!


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 7 Julai 2017 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya wafanyakazi wa Kituo cha Viwanda mjini Vatican pamoja na kumwombea Marehemu Luigi Mariotti, Baba yake na Bwana Sandro Mariotti, mmoja ya wasaidizi wa mahali anapoishi Baba Mtakatifu, aliyefariki dunia, Jumatano, tarehe 5 Julai 2017. Mzee Luigi alikuwa pia ni mfanyakazi katika Kituo hiki cha viwanda. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia kwa namna ya pekee umuhimu wa  kazi kama utimilifu wa maisha ya binadamu na kwamba, Yesu alithamini sana kazi katika maisha na utume wake.

Injili inamwonesha Yesu akimwita Mathayo mtoza ushuru, moja ya watu waliodhaniwa kwamba, walikuwa ni wadhambi kuliko watu wote. Hawa waliwatoza watu kodi na kuipeleka kwa Warumi, lakini uzoefu unaonesha kwamba, hawa pia hawakuwa waaminifu sana katika kazi yao, kwani walikuwa wamezoea kujichotea sehemu ya fedha ya kodi na kuigeuza kuwa ni mali yao! Bila kupepesa pepesa macho watoza ushuru walikuwa ni wezi na wasaliti wakuu ndiyo maana hawapendwi sana na watu! Yesu anamwona Mathayo mtoza ushuru anamwita na kumtaka amfuate.

Mathayo kwa heshima hii mbele ya umati wa watu, akaamua kumwandalia Yesu chakula, hali ambayo ilileta zogo kubwa kwa watu kutahamaki kwamba, Yesu alikuwa anakula na wadhambi. Lakini, Mathayo hakuangalia makunyanzi ya watu, ataonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake, akaitwa ili naye aweze kushiriki katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Hapa Yesu anaonesha utume wake wa kuwakomboa watu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, ili kuwashirikisha furaha ya maisha ya uzima wa milele.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, binadamu wote wametenda dhambi na kutindikiwa neema ya utakaso. Kila mtu anafahamu udhaifu na mapungufu yake ya kibinadamu, jambo la msingi ni kwa waamini kumfungulia Kristo Yesu, malango ya maisha yao, ili aweze kuwaganga na kuwaponya na dhambi zao. Anataka rehema na wala si sadaka; amekuja kuwaita wakosefu na wadhambi ili waweze kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu anayesamehe, anayeponya na kuganga daima. Waamini wanapoanguka dhambini wawe na ujasiri wa kumwita Yesu ili aweze kuwaokoa, kuwaganga na kuwaponya, kwani Yesu anawapenda jinsi walivyo! Waamini waoneshe ujasiri wa kumwalika Yesu ili aweze kuwaondolea dhambi zao.

Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha mahubiri yake kwa kukumbusha kwamba, Ijumaa ya kwanza ya Mwezi inatolewa kwa ajili ya Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, chemchemi ya neema, baraka na Sakramenti za Kanisa. Hii ni hazina ya huruma ya Baba wa milele na kwamba, Yesu anasamehe yote kabisa na kuwajalia waja wake chemchemi ya furaha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.