2017-07-07 14:39:00

Viongozi wa G20 shikamaneni ili kupambana na changamoto za kimataifa


Kuna haja kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuthamini rasilimali muda katika kupambanana na changamoto ya umaskini, vita na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji. Ili kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano katika utekelezaji wake. Umefika wakati wa kutekeleza sera na mikakati inayoamriwa na Jumuiya ya Kimataifa kwa vitendo zaidi kwani maneno matupu hayavunji mfupa! Nchi za G20 zinapaswa kujisikia kuwa ni sehemu ya familia kubwa ya binadamu, kumbe, zinapaswa kuonesha umoja na mshikamano na mataifa mengine duniani!

Haya ni mambo msingi ambayo Baba Mtakatifu Francisko amewandikia viongozi wakuu wa G20 wanaoshiriki katika mkutano wao huko Hamburg, Ujerumani, kama mwendelezo wa Mapokeo ambayo yameanzishwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI tangu mwaka 2009, viongozi hawa walipokutana huko London, Uingereza. Baba Mtakatifu katika ujumbe huu ambao amemwandikia Chancellor Angela Merkel wa Ujerumani ambaye ndiye mwenyeji wa mkutano huu, anapenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza wajumbe wa mkutano huu ambao wanaendelea kusimama kidete kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na utawala wa sheria, ukuaji wa uchumi mintarafu soko la fedha kimataifa, biashara, changamoto na matatizo ya kodi pamoja na kuhakikisha kwamba, uchumi wa dunia unakuwa ni endelevu!

Mambo haya hayana budi anasema Baba Mtakatifu Francisko kuangalia pia changamoto ya vita na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani, ili kujenga jamii inayosimikwa katika udugu, haki na amani. Baba Mtakatifu anapenda kuchambua baadhi ya vipengele vinavyoweza kusaidia kutafakari na hatimaye, kupanga mbinu mkakati wa utekelezaji wa maamuzi yatakayokuwa yamefikiwa!

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, wimbi la wakimbizi na wahamiaji kamwe haliwezi kutenganishwa na baa la umaskini, vita, ghasia na mipasuko ya kijamii, changamoto kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa ni kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema rasilimali muda ili kuzipatia changamoto hizi suluhu ya kudumu kwa kuwa na mbinu mkakati makini unaoweza kutekelezwa kwa wakati muafaka. Kuna haja kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, wakimbizi,  watu wanaoteseka, wanaotengwa na kunyanyaswa bila kujali: utaifa, rangi, dini au tamaduni. Umefika wakati wa kuachana na vita!

Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee kabisa, anapenda kutoa angalisho kwa viongozi wakuu wa G20 pamoja na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake kuangalia kwa makini hali ya mateso na mahangaiko ya wananchi wa Sudan ya Kusini, Ukanda wa Ziwa Chad, Nchi zilizoko Pembe ya Afrika na Yemen ambako zaidi ya watu milioni thelathini wanakabiliwa na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha sanjari na ukame. Hawa ni watu wanaopaswa kusaidiwa haraka iwezekanavyo kwa kuwa na malengo ya muda mrefu na mfupi kama sehemu ya mchakato wa mageuzi ya kiuchumi duniani pamoja na kuhakikisha kwamba, uchumi wa dunia unakuwa katika kiwango kinachoridhisha!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kuna haja ya kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa ili kuondokana na vita isiyokuwa na tija wala mvuto kwa ustawi na maendeleo ya wengi. Nchi za G20 zinapania pamoja na mambo mengine kuhakikisha kwamba tofauti za kiuchumi zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu ili utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030 uweze kupata ufanisi mkubwa zaidi. Ndoto hii haitaweza kufikiwa ikiwa kama bado kuna vita na kinzani za kijamii; biashara ya silaha inaendelea kupamba moto kila kukicha. Ukweli na uwazi, vitasaidia kumaliza tofauti hizi msingi, ili kwamba, mchakato wa utekelezaji wa maendeleo endelevu unaweza kushika kasi na kusonga mbele zaidi. Jambo la msingi ni kujenga na kukuza umoja katika masuala ya kiuchumi, kijamii na kukataa katu katu kukumbatia migogoro ya kivita kwa masilahi binafsi.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kushikamana dhidi ya itikadi zinazopingana na dola, ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha mafao ya wengi yanayotekelezwa kwa uthabiti mkuu badala ya kukumbatia sera za watu wachache kwa mafao yao binafsi. Viongozi wa G20 wanaowakilisha nchi chache sana duniani ambazo zinazalisha kiasi cha asilimia 90% ya bidhaa na huduma, wanapaswa kufanya tafakari makini sana, kwa kusikiliza sauti ya mataifa maskini zaidi duniani, kwani wao ndio waathirika wakubwa wa mtikisiko wa uchumi kitaifa na kimataifa, hata kama wao si wachangiaji wakuu. Hapa, changamoto ni kuhakikisha kwamba, watu wote wanakuwa ni sehemu ya mchakato wa maendeleo endelevu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Sera za maendeleo za Umoja wa Mataifa na Mashirika yake ya misaada Kimataifa na Kitaifa inapaswa kuangaliwa zaidi sanjari na kuheshimu Itifaki na Sera za kimataifa zilizokwisha kutiwa sahihi, ili kweli sera na mikataba hii iweze kudumu na kuwafaidia wengi. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, viongozi wa G20 wataweza kutekeleza dhamana na majukumu yao kwa uwajibikaji wa mshikamano, ili kuleta mwanzo mpya wa mageuzi ya kiuchumi yenye mwonekano mpya; yanayoshirikisha, endelevu na kwamba, yanalinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Huu ni wajibu unaowakumbatia na kuwaambata watu wote pasi na ubaguzi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.