2017-07-07 16:58:00

Matunda ya Mwaka wa Padre Tanzania!


Kanisa linaendelea kujitahidi kutafakari kwa kina na mapana ukuu na utakatifu wa Fumbo la wito, maisha na utume wa Kipadre, ili kuweka bayana thamani yake isiyoweza kupimika kwa mizani ya kibinadamu, ili kulinda, kuhifadhi na kudumisha usafi na utakatifu wake kama wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa. Jambo la msingi kwa Mapadre ni kutambua kwamba, Kanisa linawahimiza kuwa kweli ni watumishi waaminifu, watakaomuakisi Kristo fukara, Kristo mtii na Kristo msafi katika useja! Kwa kutambua thamani, ukuu na utakatifu wa Daraja Takatifu la Upadre, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linaadhimisha Mwaka wa Padre Tanzania.

Mapadre wote wanaopewa Daraja Takatifu wakati huu, wanakuwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka wa Padre Tanzania. Askofu Isaac Amani Massawe wa Jimbo la Moshi, tarehe 6 Julai 2017 ametoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi 31 kutoka Jimbo la Moshi na Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume. Tarehe 7 Julai 2017, Askofu Msaidizi Eusebius Nzigilwa wa Jimbo kuu la Dar es Salaam ametoa Daraja takatifu la Upadre kwa Mashemasi tisa. Imekuwa ni nafasi pia kwa Padre Benedikto Shayo na Padre Paulo Haule wa Jimbo kuu la Dar es Salaam kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre, matendo makuu ya Mungu!

Askofu Msaidizi Eusebius Nzigilwa katika mahubiri yake, amewataka Mapadre wapya kumtanguliza Mwenyezi Mungu katika maisha yao: kwa kuanza na kumaliza siku kwa sala na tafakari ya kina ya Neno la Mungu. Watambue kwamba, mavuno ni mengi, lakini Bwana wa mavuno anataka watenda kazi wema, wachamungu, watakatifu na wachapaka kazi bila ya kujibakiza! Mapadre wapya wanatumwa kwenda kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa. Mapadre wapya watambue kuwa wametwaliwa kati ya watu kwa ajili ya watu wa Mungu katika mambo matakatifu, kumbe, wameitwa na sasa wanatumwa kwenda kufanya kazi ya Bwana, yaani kushiriki katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Huu ni mchakato unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Askofu Msaidizi Nzigilwa amewataka Mapadre wapya kumjifunza Kristo ambaye ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nira yake ni laini na mzigo wake ni mwepesi. Amewaonya Mapadre wasigeuke kuwa ni mabwana, watemi na watalawa! Watambue kwamba, wanaitwa kuwa watenda kazi waaminifu na waadilifu katika shamba la Bwana. Katika maisha na utume wao, huko duniani watakutana na watu wema, watakatifu pamoja na wadhambi! Wasiwabague wadhambi katika maisha na utume wao, wawaonjeshe huruma na upendo, ili wadhambi waweze kutubu na kumwongokea tena Mungu, kwani Mapadre kimsingi ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu. Askofu msaidizi Nzigilwa amewataka Mapadre kujenga na kudumisha umoja, upendo, udugu na mshikamano wa dhati katika maisha na utume wao ili kamwe wasitoe nafasi ya chuki, uhasama na utengano kuharibu maisha na utume wao kama Mapadre! Mapadre wapya ni kama ifuatavyo:

Padre Alfonce Ntakwezile.

Padre Danipaso Bitegeko.

Padre Francis Malele.

Padre Frank Mtavangu.

Padre Simoni Shija.

Mapadre kutoka katika Mashirika ya Kitawa ni kama ifuatavyo:

Padre  Conrad Mutayoba, OFM.

Padre Patrick Aidan Ngamesha, Shirika la Yesu (Jesuists).

Padre  Christopher Amoni Mapunda, Shirika la Yesu (Jesuits).

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.