2017-07-06 14:17:00

Wafanyakazi katika sekta ya afya dumisheni Injili ya uhai!


Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordiae vultus” yaani “Uso wa huruma” anakumbusha kwamba, maisha ya binadamu ni hija na kuwa mwanadamu mwenyewe ni mhujaji hapa duniani; ni mtu anayesafiri kwenda nyumbani kwa Baba. Hija inapaswa kuwa ni nyenzo ya toba na wongofu wa ndani; huruma na mshikamano wa upendo na udugu, ili kuwa vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu.

Alhamisi, tarehe 6 Julai 2017 familia ya Mungu Jimbo kuu la Czestochowa, nchini Poland imeadhimisha hija ya 52 kitaifa kwa ajili ya wagonjwa, walemavu pamoja na wazee kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Jasna Gora “Yasina Gura”. Imekuwa ni nafasi pia kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Marehemui Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la huduma kwa wafanyakazi katika sekta ya afya ambalo kwa sasa ni kitengo cha Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya binadamu.

Ibada ya Misa imeongozwa na Askofu msaidizi Marek Szkudlo wa Jimbo la Katowice na mahubiri kutolewa na Monsinyo Jean-Marie Mupendawatu, Katibu mwakilishi, Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya binadamu ambaye aliwahi kufanya kazi kwa karibu sana na Hayati Askofu mkuu Zygmunt Zimowski aliyejisadaka bila kujibakiza hadi dakika ya mwisho wa maisha yake, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wagonjwa sehemu mbali mbali za dunia.

Hayati Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, ni kiongozi aliyeshuhudia Injili ya huruma na mapendo kwa wagonjwa, wazee na walemavu; akasimama kidete kulinda, kutetea utu na heshima ya wagonjwa dhidi ya utamaduni wa kifo. Alikazia umuhimu wa wahudumu katika sekta ya afya kuhakikisha kwamba,  wanaonesha upendo, huruma, utu wema, uvumilivu na majadiliano ili kuwasaidia wagonjwa katika mahitaji yao msingi: kiroho na kimwili! Monsinyo Jean-Marie Mupendawatu, Ijumaa asubuhi, tarehe 7 Julai 2017 anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumbu kumbu ya Marehemu Askofu mkuu Zygmunt Zimowski aliyefariki dunia tarehe 12 Julai 2016.

Madhabahu ya Bikira Maria wa Jasna Gora ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa wagonjwa, wazee na walemavu! Hapa waamini wanamkimbilia Bikira Maria Afya ya wagonjwa kwa ulinzi na tunza yake ya kimama; kwa faraja na upendo wake usiokuwa na kifani. Wafanyakazi katika sekta ya afya wanapaswa kukumbuka na kutambua kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa huduma ya huruma na upendo inayofumbatwa katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Dhamana na wajibu wa wafanyakazi katika sekta ya afya inawataka kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha uhai, utu na heshima ya binadamu.

Wafanyakazi katika sekta ya afya wawe na ujasiri wa kujenga mahusiano mema na wagonjwa, ili wagonjwa nao wawe kujiamimisha kwao katika huduma ya upendo. Ni wahudumu wanaochangamotishwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutenda wema; na wagonjwa nao, waweze kuwa tayari kuishi kwa matumaini, shida na mahangaiko yao ya ndani, daima wakitafuta neema na baraka ya Mungu ili kustahimili mahangaiko haya. Hii ndiyo ile Njia ya Msalaba ambayo Mtakatifu Yohane Paulo II amewafundisha wengi katika maisha na utume wake!

Lakini, Msalaba wa Kristo ulikuwa ni nguzo ya maisha yake, mateso na mahangaiko yalikuwa ni sehemu ya tasaufi ya Mtakatifu Yohane Paulo II. Lakini, ikumbukwe kwamba, Bikira Maria aliteseka sana tangu mwanzo alipopashwa habari za kuzaliwa kwa Mtoto Yesu, hadi pale alipothubutu kusimama chini ya Msalaba na kupokea Maiti ya Mwanaye Mpendwa Yesu Kristo anakaza kusema Monsinyo Jean-Marie Mupendawatu. Huu ni mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujiaminisha mbele ya tunza na maombezi ya Bikira Maria kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko, ili kweli wagonjwa nao wakiwa imara katika imani, matumaini na mapendo, wawe kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu katika maisha yao, ni imani inayorutubishwa kwa njia ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo makini cha imani tendaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.