2017-07-06 07:17:00

Marehemu Kardinali Meisner alikuwa ni mtu wa imani na upendo thabiti!


Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa Kardinali Joachim Meisner, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 83 baada ya kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Kardinali Meisner anasema Baba Mtakatifu, ameitwa kutoka katika ulimwengu huu na Baba mwenye huruma. Katika salam zake za rambi rambi kwa Kardinali Rainer Maria Woelki, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kolon, nchini Ujerumani, Baba Mtakatifu anasema, yuko karibu na familia ya Mungu Jimboni humo kwa njia ya sala, katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya kifo cha Kardinali Joachim Meisner, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Kolon, nchini Ujerumani. Amerafiki dunia akiwa usingizini tarehe 5 Julai 2017, huko Bad Fuessing, Kusini mwa Ujerumani alikokuwa amekwenda kwa mapumziko!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ni kiongozi aliyekuwa na imani thabiti na upendo wa dhati kwa Kristo na Kanisa lake; akajitosa kimasomaso kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu anamwombea Marehemu ili Kristo, Hakimu mwenye huruma na haki, aweze kumlipa kwa dhamana, uaminifu na juhudi zake kwa ajili ya familia ya Mungu: mashariki na magharibi na hatimaye, aweze kumweka miongoni mwa ushirika wa watakatifu huko mbinguni. Mwishoni, Baba Mtakatifu anapenda kutoa baraka zake za kitume kwa wale wote walioguswa na msiba huu kwa sala na sadaka yao.

Itakumbukwa kwamba, Kardinali Joachim Meisner, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Kolon nchini Ujerumani amefariki dunia, Jumatano, tarehe 5 Julai 2017 akiwa na umri wa miaka 83. Alikuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kolon kuanzia mwaka 1988 hadi mwaka 2014 alipong’atuka kutoka madarakani! Itakumbukwa kwamba, alizaliwa tarehe 25 Desemba 1933 huko Breslau, Silesia, Ujerumani eneo ambalo kwa sasa ni Poland. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitaalimungu ambako alijipatia shahada ya uzamivu, kunako tarehe 22 Desemba 1962 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre.

Tarehe 17 Machi 1975 akateuliwa na Mwenyeheri Paulo VI kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Vina na Askofu msaidizi Jimbo Katoliki Erfurt, Ujerumani ya Mashariki na kuwekwa wakfu kama Askofu tarehe 17 Mei 1975. Tarehe 22 Aprili 1980, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu tarehe 22 Aprili 1980. Kuanzia mwaka 1982 hadi mwaka 1989 alikuwa ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Berlin. Tarehe 20 Desemba 1988 akateuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kolon nchini Ujerumani hadi alipong’atuka kutoka madarakani tarehe 28 Februari 2014. Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Kardinali tarehe 2 Februari 1983.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 
All the contents on this site are copyrighted ©.