2017-07-06 16:38:00

Jifunzeni kutoka kwa Kristo kuwa wanyenyekevu wa moyo!


Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, Padre Munachi, mhubiri maarufu anatoa mfano huu katika mahubiri yake ambapo yaweza saidia tafakari yetu dominika hii. Anasema, mtu mmoja aliota ndoto usiku. Aliota kuwa alikuwa akitembea ufukweni pamoja na Bwana Yesu. Kutoka angani aliona picha nzima ya maisha yake. Kwa kila tukio la maisha yake aliona nyayo zake na zile za Bwana zikiwa pembeni mwake. Lakini aligundua kuwa sehemu nyingi za matukio ya maisha yake hasa wakati alipokuwa na shida kubwa, nyayo za Bwana hazikuonekana. Basi akamlalamikia Bwana kwa kumwacha mpweke wakati wa taabu. Jibu la Bwana likawa rahisi sana – hukuona nyayo zangu pembeni mwako wakati wa shida zako kwani huo ndio wakati nilipokubeba.

Ndugu zangu, tunaona katika injili ya leo, Yesu akisema njooni kwangu ninyi nyote mnaosumbuka na kuelemewa na mizigo kwani nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi. Hakika huu ni mwaliko mtakatifu na mwaliko ambao sote tunaomtafuta Bwana tunaalikwa kuukimbilia.  Padre Munachi anaendeleza mfano mwingine akisema, Albert Camus alijaribu kuelewa maana na mwenendo mzima wa maisha ya mwanadamu. Alitumia mfano wa Sisyphus, aliyekuwa mtu wa kufikirika katika hadithi za Kigiriki. Huyu alipata hukumu ya kusukuma kipande kikubwa cha jiwe kukipeleka kilimani. Ilikuwa shughuli kubwa sana na alifanya kazi hii kwa juhudi kubwa. Ila kila alipokaribia kilimani hakuweza kulifikisha jiwe kileleni kwani nguvu zote zilikuwa zimemwishia. Hivyo jiwe liliporomoka mpaka chini. Hali hii iliendelea hivvyo maisha yake yote na hivyo hakuweza kuitumikia adhabu yake. Hali hii inaakisi uhalisia wa maisha ya mwanadamu. Ni maisha toka chini kwenda juu.

Pengine haya ndo mahangaiko ya watu wengi wanaotamani kumtumikia Mungu kwa uaminifu. Huweza pengine kufanya vizuri kwa muda mfupi tu. Muda mwingi hushindwa kufika kileleni au kubaki waaminifu katika ahadi na maisha yao. Leo katika Mat. 11:28 Yesu anatupa mwaliko na jinsi ya kujinasua na haya mahangaiko akisema – njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao na kulememwa na mzigo, nami nitawapumzisha. Yesu atukumbusha kuwa katika harakati zetu za maisha, hatuna budi kuweka pia matumaini yetu kwa Mungu. Hakika peke yetu hatutaweza ila pamoja na Mungu yote huwezekana. Na Yesu anaendelea kusema katika Mat. 11:29 – mjitwike nira yangu na kujifunza kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu moyoni, nanyi mtazipatia roho zenu raha. Inaeleweka hapa kuwa Yesu anataka tutupilie mbali nira zetu na tubebe nira yake, kwa sababu tofauti na nira zetu, mzigo wake ni mwepesi.

Katika injili twaona habari ya ufunuo wa hekima ya Baba kwa Mwanae.  Tunasikia habari ya uhusiano uliopo kati ya Baba na Mwana na hitimisho la mwaliko wa Yesu kwa wasumbukao ili kupata faraja. Yesu Kristo ndiye njia na ufunuo wa hekima hii ya Mungu. Yesu anasema wazi kuwa anayo hekima kamili ya Mungu na kwa hiyo anaweza kusema anamfahamu Baba na mapenzi yake.

Hekima hii ya Mungu na kwa kadiri ya mapenzi yake ni kwa faida ya wanyonge. Tunasoma katika YBS. 24:18 – njooni kwangu mnaonitamani, na kutoka katika mazao yangu mshibishwe na wapumbavu wanahimizwa kujinyenyekesha katika shingo ya hekima na katika YBS 51:23,26 – tunasoma, nikaribieni enyi mlio wajinga, na hivyo mpate kukaa katika nyumba ya mawaidha. Mwinamishe shingo yenu chini ya nira, na nafsi zenu zitapokea mawaidha. Maneno haya yaonekana kutambua ukuu wa Yesu Kristo. Yeye anajifananisha na hekima iliyomwilishwa. Hivyo ye yote atakayeishi kadiri ya hekima hii ya Mungu atapata amani na faraja. Ni ipi hii nira ya Yesu? Hakika ni wajibu wetu na majukumu yetu kwa Kristo. Katika 1 Tim. 6:1… tunasoma hivi: watumwa walitakiwa kuwa katika nira ya bwana wao – wote walio chini ya nira ya utumwa wawajali mabwana zao kwa heshima yote wastahiliyo, kusudi jina la Mungu na mafundisho yetu yasipate sifa mbaya.

Kuchukua nira ya Bwana ni kujiweka katika mahusiano na Yesu na kuishi kadiri ya amri na maagizo yake. Hakika kufuata mafundisho ya Bwana, yaweza onekana kugumu sana kwani yadai sadaka kubwa. Hivyo tamaa ya kurudi katika hali zetu ni kubwa zaidi na mara nyingi imegharimu maisha yetu pale ambapo tumeenda peke yetu. Na mizigo yetu ikawa mikubwa zaidi. Katika mazingira ya Wayahudi, nira ilifungwa katikati ya shingo za ng’ombe wawili ili kuvuta jembe la kulimia. Ili nira ifanye kazi walihitajika ng’ombe wawili. Nasi pia ili tuweze kujibu vizuri mapenzi ya Mungu hatuna budi kufungamanisha maisha yetu pamoja na Bwana. Peke yetu hatutaweza ila pamoja na Bwana itawezekana. Nira ya Yesu ni tofauti na nira ya sheria, kwa maana watu wa kawaida walishindwa kuibeba. Wataalamu wanasema kuwa nira ya Yesu ni kukubali mapenzi ya Mungu. Ndicho kinachoonekana katika injili ya leo. Hakika nira ya Yesu ni ule upendo aliotujalia Mungu sisi waja wake.

Mtu mmoja aitwaye Richard Braunstein anasema kuwa unaweza kutoa bila kupenda, lakini huwezi kupenda bila kutoa. Mwaliko wa Yesu kujifunza kwake waonesha upole wake na unyenyekevu wake na zaidi sana upendo wake kwetu. Katika somo la kwanza, nabii anaelezea aina mpya ya mfalme, mfalme wa amani, anayepanda punda dhidi ya magari ya vita. Ni mfalme aletaye amani kwa mataifa yote. Huyu mfalme, kanisa latuambia kuwa ndiye Yesu Kristo. Yeye ataongoza kwa hekima ya Mungu na ataongoza kwa mwanga wa amani na nira ya upendo. Wote wakubalio ufalme huu watapata amani. Lakini ili kuupata huo ufalme, hatuna budi kuishi kadiri ya mapenzi yake Baba. Tunamshukuru Mungu kwani ametupatia Mwanae na kama tutaishi pamoja naye tuna uhakika wa kuupata ufalme wa Mungu. Hii kazi ya kuzipata mbingu imesharahisishwa.

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.
All the contents on this site are copyrighted ©.