2017-07-06 13:52:00

Dr. Navarro-Valls, gwiji na nguli wa tasnia ya habari amefariki dunia


Gwiji na nguli wa mawasiliano, Dr. Joaquin Navarro-Valls amefariki dunia, Jumatano, tarehe 5 Julai 2017 akiwa na umri wa miaka 80. Mwamini mlei wa kwanza kuwa ni msemaji mkuu wa Vatican wakati wa uongozi wa Mtakatifu Yohane Paulo II yaani kuanzia Mwaka 1984 hadi mwaka 2006. Kwa muda wa miaka michache, amekuwa pia ni msemaji mkuu wa Papa Mstaafu Benedikto XVI. Ijumaa, tarehe 7 Julai 2017 Monsinyo Mariano Fazio anaongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Eugenio kwa ajili ya kumwombea Marehemu Dr. Joaquin Navarro-Valls.

Alizaliwa tarehe 16 Novemba 1936 huko Cartagena, nchini Hispania, akabahatika kupata masomo yake huko Cartagena, Granada na Barcellona katika masuala ya afya ya akili na kubahatika kufaulu vyema katika fani yake! Akiwa mwanafunzi, Dr. Joaquin Navarro-Valls alijiunga na Shirika la “Opus Dei”, yaani “Kazi ya Mungu”. Kutoka katika huduma ya afya ya akili, akajiendeleza zaidi katika masuala ya uandishi wa habari na kufuzu masomo yake kunako mwaka 1968! Akatambulika sana kutokana na juhudi, nidhamu, uadilifu na uwajibikaji wake katika kutengeneza habari, akaipika na kupikika, akaipakua na ikapakulika barabara!

Kunako Mwaka 1970 akahamia Roma na kushirikiana kwa karibu sana na Mtakatifu Josemaria Escriva katika sekta ya mawasiliano ndani ya Shirika la “Opus Dei”. Kwa miaka mingi  alikuwa ni mwandishi wa habari wa Jarida la Diagonal, Nuestro Tempo na Mwakilishi wa Gazeti la ABC nje ya Hispania kazi ambazo amefanya kati ya mwaka 1964 hadi mwaka 1984 alipoteuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa msemaji mkuu wa Vatican na mlei wa kwanza kuchukua dhamana hii nyeti katika maisha na utume wa Kanisa!

Ni Gwiji aliyebahatika kufanya kazi katika mazingira magumu na tete katika kipindi kigumu cha historia ya dunia; kati ya kinzani na mipasuko ya kisiasa. Akabahatika kuwakutanisha Yohane Paulo II na Rais  Mikhail Sergeevič Gorbačëv, (Mikhail Gorbaciov)  wa Urussi pamoja na Rais Fidel Castro wa Cuba. Dr. Joaquin Navarro-Valls katika maisha na utume wake, amebahatika kufanya kazi karibu sana na watakatifu yaani: Yohane Paulo II na Mtakatifu Josemaria Escriva. Alikuwa mlei ambaye maisha yake yalifumbatwa katika sala na tafakari.

Baada ya kifo cha Mtakatifu Yohane Paulo II, akatoweka kabisa kwenye luninga hadi mwaka 2006 aliporejea tena katika tasnia ya habari. Watu wengi wameona ushuhuda wa mwamini mlei aliyekuwa mwaminifu kwa Kanisa, maisha na wito wake kama mwanachama wa Opus Dei hadi dakika ya mwisho! Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu mstaafu wa Vatican ambaye kwa sasa ni Rais wa Mfuko wa Joseph Ratzinger-Benedikto XVI anasema, ni kiongozi aliyeweza kujenga na kudumisha Jumuiya ya watu wa tasnia ya habari, akajitahidi kutoa habari za Khalifa wa Mtakatifu Petro katika ukweli, uwazi na ubunifu mkubwa. Alikuwa na vipaji vingi katika mawasiliano, akavitumia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo ndani na nje ya Vatican. Habari zake zilisheheni uzito, zilikuwa zinavutia na kuhabarisha kwa undani.

Ni mwamini mlei aliyetekeleza dhamana na wajibu wake kwa uaminifu, uadilifu na moyo mkuu! Akajitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kanisa la Kristo, akashuhudia kwamba, kweli alikuwa mwaminifu. Atakumbukwa kwa weledi na udumifu wake kama Msemaji mkuu wa Vatican kwa muda mrefu katika historia ya Kanisa Katoliki. Mchango wake ni mkubwa sana, kiasi kwamba, hakuna mwanadamu anayeweza kumpatia haki yake barabara. Dr. Joaquin Navarro-Valls alikuwa gwiji wa mawasiliano aliyeacha urithi mkubwa katika tasnia ya mawasiliano mjini Vatican na wala hakuna mfano wake tena!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.