2017-07-05 15:54:00

Papa Francisko: Vijana tambueni na kusherehekea maisha!


Umoja, upendo, udugu na mshikamano miongoni mwa vijana wa kizazi kipya kutoka Israeli, Palestina na sehemu mbali mbali za dunia, ndiyo nguzo msingi iliyowakutanisha na kuwaunganisha vijana hawa kiasi cha kuweza kuonana ana kwa ana, katika ukweli na uwazi; ili kuambata na kuenzi Injili ya uhai inayotoa maana ya maisha ya binadamu hapa duniani. Kila mtu anayo thamani kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu na kila mara watu wanapokutana, thamani hii inapanuka zaidi, ili kuendeleza ile kazi ya uumbaji! Hii ni sehemu ya ujumbe kwa njia ya video uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika sherehe za ufungaji wa Kongamano la wanafunzi wa  Taasisi ya Kipapa ya“Scholas Occurentes” lililozinduliwa hapo tarehe 2 Julai hadi tarehe 5 Julai, 2017, huko mjini Yerusalemu.

Baba Mtakatifu anawataka vijana wa kizazi kipya kugundua maana ya maisha, ili waweze kuyasherehekea, kwani ujana ni mali, fainali iko uzeeeni! Vijana wanapaswa kuonja uzuri na utakatifu wa maisha, ili kuyaadhimisha kikamilifu, licha ya matatizo na changamoto mbali mbali zinazomzunguka mwanadamu. Shule ni mahali pa kuwafunda vijana maana ya maisha, kwa kujiweka wazi kwa wale wasiowafahamu, ili kuchanganyika na hatimaye, kufutilia mbali kabisa maamuzi mbele ambayo yamekuwa ni chanzo cha kinzani na mikwaruzo miongoni mwa jamii mbali mbali za binadamu. Baba Mtakatifu anawaalika wazazi na walezi kuwapatia vijana wa kizazi kipya fursa ya kuwa na ndoto ya kucheza, ili kujenga moyo wa shukrani na hatimaye, kukuza kipaji cha ubunifu.

Kongamano hili anasema Baba Mtakatifu Francisko imekuwa ni fursa kwa wazazi na walezi kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini, ili kuibua matumaini, ili hatimaye, ile ndoto iweze kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya vijana wa kizazi kipya. Shule pawe ni mahali pa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana; kushikamana katika umoja na kuthamini tofauti msingi zilizopo, ili kufikia usawa bila ya kulazimika wote kuwa sawa sawa! Hiki ndicho kilio cha walimwengu wa nyakati hizi.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kuna tabia ya watu wanaotaka kujenga kuta za utengano, kwa sababu ya woga na wasi wasio usiokuwa na mvuto wala mashiko! Ni watu wenye kuwaangalia wengine kwa jicho la kengeza na kuwapachika majina kuwa ni adui! Ulimwengu unawahitaji vijana makini na jeuri, watakaoweza kutoka kimasomaso kwa ajili ya kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana. Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru wanafunzi kutoka vyuo vikuu ndani na nje ya Israeli waliokuwa wamekusanyika katika kongamano hili. Ujuzi, maarifa na weledi walioupta uwasaidie kujenga na kudumisha huduma ya kusikiliza kwa makini. Anawataka vijana wa kizazi kipya kuendelea kuwa na ndoto, kutafuta maana halisi ya maisha, kushukuru na kuadhimisha Injili ya uhai, kwa kuzingatia utamaduni wa watu kukutana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.