2017-07-05 15:37:00

Papa Francisko asema: Jengeni umoja, udugu na mshikamano kati ya watu


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomtumia Dr. Luigi Contu, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Habari la ANSA, anasema, Bara la Ulaya lina dhamana na wajibu wa kuwasaidia wahamiaji. Baba Mtakatifu pamoja na mambo mengine anakazia umuhimu wa kuwashirikisha wahamiaji katika maisha ya wananchi mahalia ili kweli waweze kujisikia kuwa ni sehemu ya maisha yao.Wahamiaji wajenge tabia ya kuheshimu sheria, taratibu na kanuni za maisha ya watu wanaowapatia hifadhi na kwamba, watu wajenge na kudumisha madaraja ya watu kukutana: na utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kudumisha umoja, udugu na mshikamano kati ya watu wa Mataifa.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, yuko karibu na watu na taasisi ambazo zinaendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Wakimbizi na wahamiaji ni changamoto inayopaswa kushughulikiwa kwa njia ya mshikamano na ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo na Kiutu msingi wa utamaduni wa Ulaya. Ujumbe huu wa Baba Mtakatifu unapatikana katika tovuti kuhusu habari za wahamiaji inayojulikana kama: Infomigrants.net iliyotengenezwa na Shirika la Habari la ANSA kwa kushirikiana na vyombo vya habari kutoka Ufaransa “France Media Monde pamoja na Deutche Welle” la Ujerumani.

Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia wale wote wanaojisadaka na kujibidisha kwa ajili ya huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji uwepo wake wa daima kwa njia ya sala. Anasema, hawa ni watu wanaolazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na vita, vitendo vya kigaidi, majanga asilia, dhuluma na nyanyaso mbali mbali. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, wahamiaji na wakimbizi hawa wataweza kukutana na ndugu zao, watakowashirikisha chakula na matumaini katika hija ya pamoja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.