2017-07-05 08:15:00

Miaka 150 ya Uinjilishaji, Miaka 100 ya Upadre, Miaka 60 Jimbo Musoma


Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara, Miaka 100 ya Upadre Tanzania na Kumbu kumbu ya Miaka 60 ya Jimbo Katoliki la Musoma, Askofu Michael Msonganzila ameamua kuandika Barua ya Kichungaji inayoongozwa na kauli mbiu “ Upendo kwa utume” ili kufafanua kwa kina maana ya matukio yote haya katika maisha na utume wa familia ya Mungu Jimbo Katoliki Musoma na Tanzania katika ujumla wake! Katika barua hii, anachambua historia ya Uinjilishaji Tanzania Bara, Ukuaji wa Kanisa Mahalia yaani Jimbo Katoliki la Musoma; Umuhimu wa maadhimisho ya Jubilei katika maisha na utume wa Kanisa Jimbo Katoliki Musoma.

“Upendo kwa utume ni upendo kwa Kanisa na ni upendo kwa Kristo. Mkristo anapaswa kuguswa na kuwa tayari kuitikia mahitaji ya kiroho ya wale ambao bado hawajamjua Kristo” Kwa maneno haya Mwenyeheri Papa Paulo VI aliwahutubia wakurugenzi wa Mashirika ya Kitume ya Kipapa nchini Italia wiki chache kabla ya kifo chake mwaka 1978. Baba Mtakatifu huyu ambaye Kanisa linamkumbuka na kumuenzi kwa adhama kutokana na juhudi zake kubwa za kuhimiza moyo wa kimisionari katika kanisa, ametuachia katika maneno yake haya mwono wa pekee juu ya utume wa kila mkristo. Mwono huu unaojikita katika upendo unatualika kutambua kuwa upendo ndio msingi na nguzo madhubuti katika kuupokea, kuuishi na kuutekeleza utume wetu. 

Asili ya upendo huu ni Mungu mwenyewe. Mungu ni upendo (1Yoh. 4:8) na ni upendo wake unaoita na kutuma. Utume wa Mwana na utume wa Roho Mtakatifu, vyote huchipua kutoka undani wa Upendo wa Baba. Kristo mwenyewe alimtaka Mtume Petro kwanza awake ndani yake upendo huu ndipo ayatwae majukumu ya utume uliokuwa mbele yake. Mara tatu alimuuliza “Je, Simoni wa Yohane wanipenda…?” Naye akisha kuukiri upendo huo “ndiyo Bwana… wewe wajua yote; wewe umetambua kuwa nakupenda”, ndipo Kristo anamkabidhi utume “Lisha kondoo wangu” (rej. Yoh. 21:15 - 19).

Kwa kuwaka upendo huu, Kanisa limepokea na kuendelea kutekeleza agizo la Kristo “enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi…” (Mt. 28:19 - 20) kama wajibu wake wa msingi. Tangu enzi ya mitume hadi leo hii idadi isiyohesabika ya wanaume na wanawake wameubeba wajibu huu kiaminifu. Wakisukumwa na upendo kwa utume, wengi wao walilazimika kusafiri na kwenda mbali na mazingira yao, wakijikatalia mengi, wakivumilia taabu na magumu mbalimbali na baadhi yao kupoteza maisha ili kumtangaza Kristo katika maisha ya wasiomjua bado. Mwaka huu Kanisa la Tanzania tunafanya Jubilei ambazo ni matunda ya upendo huu kwa utume waliokuwa nao watangulizi wetu.

Jubilei ya kwanza tunayoiadhimisha ni ya miaka 150 ya uinjilishaji katika Tanzania Bara. Wamisionari wa kwanza kufika Tanzania bara walikuwa ni Mapadre wa Shirika la Roho Mtakatifu. Hawa walifika Bagamoyo na kuanzisha Misioni tarehe 4 Machi 1868. Kitaifa Jubilei hii ilizinduliwa Rubya, Jimbo la Bukoba tarehe 01 Oktoba 2016 na itahitimishwa mwakani 2018 huko Bagamoyo. Jubilei ya Pili tunayoadhimisha ni Jubilei ya Miaka 100 ya Upadre katika Tanzania. Imetimia miaka 100 tangu mapadre wa kwanza wazalendo wa nchi hii kupewa Daraja Takatifu ya Upadre. Hawa walikuwa ni Pd. Angelo Mwirabure (Mzaliwa wa Kome - sasa Jimbo la Geita), Pd. Celestine Kipanda (Mzaliwa wa Kagunguli - sasa Jimbo la Bunda), Pd. Wilbard Mupapi na Pd. Oscar Kyakaraba (Wote wazaliwa wa Kashozi, Jimbo la Bukoba). Hawa wote walipadrishwa tarehe 15 Agosti 1917 huko Rubya, Bukoba. Jubilei hii ilizinduliwa tarehe 01 Oktoba 2016 Rubya sambamba na Jubilei ya miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara. Kilele chake kitakuwa ni tarehe 15 Agosti 2017 katika Jimbo Kuu la Dodoma.

Pamoja na Jubilei hizi, katika mwaka huu sisi familia ya Mungu ya Jimbo la Musoma tunaadhimisha miaka 60 tangu kuundwa kwa Jimbo letu. Jimbo la Musoma liliundwa tarehe 05 Julai 1957 kutoka katika iliyokuwa Prifektura ya Kitume ya Musoma. Tumependa kuyapa maadhimisho haya ya miaka 60 ya Jimbo hadhi ya Jubilei na kuyaunganisha na maadhimisho ya Jubilei mbili nilizozielezea hapo juu.Jubilei zetu hizi tatu, tulizizindua katika ngazi ya Jimbo tarehe 18 Februari 2017 kwa adhimisho la Misa Takatifu na kwa kuwasha Mshumaa wa Jubilei katika Kanisa Kuu la Kiaskofu. Kilele cha Jubilei hizi kitakuwa ni tarehe 05 - 08 Julai 2018. Nimependa niwaandikie barua hii ya kichungaji ili kufafanua mambo kadhaa kuhusu Jubilei zetu hizi tatu na kutoa mwongozo namna tutakavyoziadhimisha katika Jimbo letu hadi kilele chake.

II. Uinjilishaji Tanzania Bara katika Historia

Hatua za Uenezaji Injili Afrika

Mtakatifu Papa Yohane Paulo wa II, katika Mausia yake ya Kitume baada ya Sinodi ya Kwanza ya Afrika, alibainisha hatua tatu ambazo kwazo uenezaji wa Injili umefanyika katika Bara la Afrika. Hatua ya kwanza ilikuwa ni katika karne ya kwanza hadi ya nne ambapo uinjilishaji katika bara la Afrika umehusishwa kwa jina na mafundisho ya mwinjili Marko. Awamu hii ilijikita zaidi katika Afrika ya Kaskazini na ndiyo iliyochipusha watakatifu na waalimu mashuhuri wa Kanisa maarufu kwa mafundisho na maandishi yao. Miongoni mwao ni Orijeni, Mt. Athanasi, Tetuliani, Mt. Spiriani na Mt. Agostino, kwa kutaja wachache tu. Ni katika awamu hii pia wamepatikana Mababa Watakatifu kutoka Afrika. Hawa ni Papa Victori I (aliliongoza Kanisa kati ya mwaka 189 hadi 199), Papa Melkiades (311 - 314) na Papa Jelario I (492 - 496).

Hatua ya pili ya uinjilishaji Afrika ilikuwa ni katika karne ya kumi na tano na ya kumi na sita. Karne hizi zilishuhudia safari za wavumbuzi wa Kireno kwenye maeneo ya mwambao wa Afrika. Safari hizi zilifuatiwa na uinjilishaji wa maeneo ya karibu na jangwa la Sahara. Maeneo haya ni Benin ya sasa, Sao Tome, Angola, Msumbiji na Madagascar. Hatua ya tatu ya uinjilishaji Afrika ilianza katika karne ya kumi na tisa. Hii ilikuwa ni hatua ya ujio wa wamisionari mbalimbali kutoka bara la Ulaya. Ni katika hatua hii ambapo wamisionari walifika Tanzania, wa kwanza wakiwa ni Mapadre wa Shirika la Roho Mtakatifu.

Bagamoyo -  Mlango wa Uenezaji Injili Tanzania Bara

Wamisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu, wakitokea Zanzibar walifika Bagamoyo na kuanzisha misioni tarehe 4 Machi 1868. Tunaikumbuka na kuienzi kazi kubwa waliyoifanya waanzilishi wa misioni hii, Pd. Anthony Horner, C.S.Sp, Pd. Eduard Baur, C.S.Sp pamoja na wenzao. Mazingira ya utume wao hayakuwa rahisi. Magonjwa ya mara kwa mara, hasa Malaria yaliwashambulia sana. Ndani ya miaka tisa tu ya uwepo wao Bagamoyo, tayari mapadre kumi na wawili, masista saba na mabruda watano walikuwa tayari wamepoteza maisha. 

Upendo kwa utume uliyavuta mashirika mengine ya kimisionari kuja Tanzania Bara kueneza injili. Mwaka 1878 walifika Wamisionari wa Afrika, maarufu kama White Fathers. Hawa walitumia njia ya kati iliyowafikisha Tabora, Karema, Ujiji na Mwanza. Baadaye walienea katika maeneo ya kanda ya Ziwa. Ni wamisionari hawa waliofika hadi Nyakatende katika Jimbo letu la Musoma. Miaka kumi baada ya ujio wa Wamisionari wa Afrika, mwaka 1888, walifika Wabenediktini, Shirika la Mapadre la Mt. Benedikto. Hawa walishika njia ya kusini iliyowafikisha kwanza Mahenge, Iringa, Ndanda na Peramiho kabla ya kusambaa katika maeneo mengine ya ukanda wa kusini. Tunamshukuru Mungu kwamba kutoka kipindi cha watagulizi hawa hadi leo makundi yasiyohesabika ya wamisionari wake kwa waume wameendelea kuuitikia wito wa umisionari na kuja kuhubiri injili na kulijenga kanisa la Tanzania.

Uinjilishaji katika Jimbo la Musoma

Uinjilishaji katika Jimbo letu la Musoma unayo historia nzuri na inayotia moyo. Shirika la kwanza kueneza injili ndani ya mipaka ya Jimbo letu la Musoma ni la wamisionari wa Afrika - White Fathers. Hawa walifika kwa mara ya kwanza mwaka 1897 katika eneo la Nyakatende wakitokea Kagunguli, Ukerewe. Katika ujio wao huu mambo hayakuwaendea vizuri kwani walishambuliwa sana na ugonjwa wa malaria. Ugonjwa huu ulisababisha kifo cha mwenzao, Pd. Joseph van Thuet, na kwa sababu hii walilazimika kurudi Kagunguli. Mwaka 1909 waliamua kurudi tena. Katika awamu hii walipata misukosuko mingine mingi ikiwemo kukataliwa. Hata hivyo mwaka 1911 walipewa eneo Nyegina na hapo walianza  rasmi kujenga kanisa.  Ni katika mwaka huo huo mkristo wa kwanza alibatizwa. Kwa sababu hii tunauhesabu mwaka 1911 kuwa ndio mwaka ambao Ukristo umepokelewa katika mipaka ya Jimbo la Musoma. Mwaka 2011 tuliadhimisha kwa shukrani Jubilei ya Miaka 100 ya kuuishi Ukristo katika Jimbo letu.

Wamisionari wa Afrika walifanya kazi ya uinjilishaji hadi tarehe 11 Aprili 1946 ilipoundwa Vikarieti ya Musoma - Maswa. Vikarieti hii ilikabidhiwa kwa wamisionari wa Shirika laMaryknoll. Ni katika uongozi wa wamisionari hawa Musoma ilifanywa kuwa Prifektura ya Kitume tarehe 24 Juni 1950 na hatimaye kupewa hadhi ya kuwa Jimbo tarehe 05 Julai 1957.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, itaendelea kukushirikisha utajiri unaofumbatwa katika Barua ya Kichungaji ya Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma, Tanzania.

 All the contents on this site are copyrighted ©.