2017-07-05 17:12:00

Askofu Mkuu Musa P. Filibus asema, mkazo: Umoja wa Kanisa na Huduma!


Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican yamekuwa ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Kanisa mintarafu mchakato wa majadiliano ya kiekumene miongoni wa wafuasi wa Kristo! Kumekuwepo na mafanikio makubwa katika kudumisha uekumene wa sala unaotoa nafasi kwa wakristo kusali kwa pamoja katika matukio mbali mbali. Kumekuwepo na uekumene wa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na kwa namna ya pekee kwa nyakati hizi ni huduma kwa wakimbizi na wahamiaji, ambao wanaangaliwa na wengi kana kwamba ni kero ya kimataifa, kwani “wanapigwa danadana” kiasi cha kuonewa huruma!

Kumekuwepo na uekumene wa maisha ya kiroho unaofumbatwa katika tafakari ya Neno la Mungu linalomwilishwa katika uhalisia wa watu. Mwishoni, katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, Kanisa limeshuhudia uekumene wa damu ukiendelea kuimarishwa na kudumishwa kila wakati kutokana na vita, nyanyaso na dhuluma wanazofanyiwa Wakristo sehemu mbali mbali za dunia. Haya ndiyo maeneo ambayo kimsingi, Wakristo wote wamejikuta wakiunganishwa nayo! Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani imekuwa ni fursa nyingine tena ya kuendelea kuimarisha majadiliano ya kidini katika sala na huduma makini kwa watu wa Mungu wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia!

Hivi karibuni, Askofu mkuu Musa Panti Filibus, kutoka Nigeria, amechaguliwa kuwa Rais wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani, linalounganisha Makanisa 145 kutoka katika nchi 98 duniani. Historia inaonesha kwamba, Askofu mkuu Filibus ni kiongozi wa ngazi ya juu kabisa kuwahi kuchaguliwa kutoka Barani Afrika. Bila shaka, wengi bado wanamkumbuka Askofu Josiah Kibira kutoka Tanzania aliyeliongoza Shirikisho hili kati ya mwaka 1977 hadi mwaka 1984.

Askofu mkuu Filibus anasema, katika kipindi cha miaka saba ya uongozi wake anapenda kukazia zaidi umuhimu wa mawasiliano ndani ya Kanisa na ushirikiano wa dhati kati ya Makanisa ya Kikristo, ili kwamba, kamwe, lisiwepo Kanisa ambalo linajisikia kutengwa katika Shirikisho hili. Uongozi huu umechaguliwa hivi karibuni na mkutano mkuu wa Shirikisho uliofanyika huko Windhoek, Namibia, kuanzia tarehe 10 – 16 Mei 2017. Ndoto yake ya dhati kabisa kutoka moyoni ni kuona Shirikisho hili linajikita zaidi katika mchakato wa huduma makini kwa familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna changamoto kubwa zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo!

Vita, ghasia, kinzani na mipasuko ya kijamii; athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa. Mambo yote haya yanapelekea ongezeko kubwa la umaskini duniani, linaloendelea kuzalisha wimbi kubwa ka wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi ughaibuni pamoja na jeshi la watu wasiokuwa na fursa za ajira! Haya ni mambo yanayotishia pia usalama, utu na heshima ya binadamu. Askofu mkuu Filibus mwenye umri wa miaka 57, ameoa na kubahatika kupata zawadi ya watoto watatu. Kabla ya kuchaguliwa kuliongoza Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani alikuwa anatekeleza dhamana na utume wake wa shughuli za kichungaji nchini Nigeria. 

Anachukua nafasi ya Askofu Munib Younan ambaye amekuwepo madarakani kuanzia mwaka 2010. Kuchaguliwa kwa Askofu mkuu Musa Panti Filibus, kutoka Nigeria kwa ushindi wa “Tsunami” wakati wa uchaguzi mkuu ni alama kwamba, wajumbe wameanza kutambua na kukiri ukuaji wa Kanisa Barani Afrika pamoja na utume wake kwa familia ya Mungu. Mambo makuu mawili yanaendelea kupewa msukumo wa pekee: umoja wa Kanisa na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Askofu mkuu Filibus amekuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yake kwenye Kanisa lake nchini Nigeria, hasa zaidi kwa kujipambanua katika huduma kwa waathirika wa vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kutekelezwa na Boko Haramu ambao umekuwa ni “mwiba mchungu” kwa wananchi wa Nigeria! Ni Saratani inayotishia: usalama, umoja na mafungamano ya kijamii ndani na nje ya Nigeria. Katika uongozi wake kama Katibu wa Idara ya utume na maendeleo ya Shirikisho hili kwa kipindi cha miaka kumi na moja, amefanikiwa kujenga na kudumisha uhusiano wa karibu sana na Makanisa ya Kiluteri sehemu mbali mbali za dunia.

Hii ni hija muhimu sana ya umoja na mshikamano hata miongoni mwa Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri, kwani yakiwa yameungana, tayaweza pia kushiriki kikamilifu katika mchakazo mzima wa uekumene, ili wote wawe wamoja chini ya Kristo mchungaji mkuu. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani, imekuwa ni fursa kwa Kanisa kugundua tena umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kati ya Mataifa. Hapa jambo la msingi ni kukuza na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa Makanisa ili yote yaweze kujisikia kuwa ni mamoja na wala hakuna Kanisa linalotengwa. Kwa njia hii, Makanisa yanaweza kujikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Askofu mkuu Musa Panti Filibus Anatambua kwamba, kuna changamoto kubwa hata ndani ya Makanisa ambazo zinagumisha kwa kiasi kikubwa umoja na mshikamano wa Kanisa, lakini jambo la msingi ni kukumbuka kwamba, kuna mambo mengine yanayowaunganisha Wakristo kuliko hata yale yanayowagawa kutokana na sababu mbali mbali. Wakristo wanayo amana ya Sakramenti ya Ubatizo, chemchemi ya neema ya utakaso, wanalo Neno la Mungu, lakini zaidi, ndani mwao wanazo karama mbali mbali zinazoweza kuwa ni ushuhuda wa imani tendaji kwa Kristo na Kanisa lake. Kuna haja ya kuendelea kushirikiana na kushikamana ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo.

Mkazo ni kudumisha mchakato wa ukomavu kutoka katika umoja wa Makanisa na kuendelea kujikita katika huduma makini kwa familia ya Mungu inayokabiliwa na matatizo na changamoto mbali mbali za maisha! Kanisa linatumwa kushuhudia kwa pamoja Injili ya matumaini na mapendo kwa watu wanaoteseka zaidi. Kanisa linapaswa kuwa ni chombo cha huduma ya upendo na mshikamano na kwamba, huu ndio utambulisho makini wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo! Shirikisho la Misaada ya Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani, ni chombo muhimu sana cha huduma ya Kanisa kwa maskini na wanyonge duniani. Askofu mkuu Musa Panti Filibus, Rais wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani anayapongeza Makanisa yote yanayoendelea kujielekeza zaidi katika huduma ili kukabiliana na changamoto kubwa zinazoendelea kuibuliwa katika ulimwengu mamboleo. Huduma ya  na umoja ni mihimili mikuu miwili inayopaswa kudumisha kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kansia la Kristo duniani mintarafu mahitaji ya watu mahalia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.