2017-07-05 07:39:00

Albania ni nchi yenye amana na utajiri mkubwa kwa ustawi wa watu wake


Monsinyo Dario Edoardo Viganò, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mawasilaino Vatican, siku ya Ijumaa, tarehe 29 Juni 2017, amepewa Tuzo ya heshima ya “Knight of Scanderbeg” nchini Albania. Tuzo hiyo ni kwa heshima ya kumbukumbu ya Giorgio Castriota Scanderbeg ambaye aliipigania nchi yake ya Albania karne ya 15, kutoka kwenye utawala wa waturuki ili wajenge nchi yao wenyewe katika umoja na udugu. Akipokea heshima hiyo Monsinyo Viganò amekumbusha kuwa matangazo ya Idhaa ya Kialbania ya Radio Vatican yalianza kuambaa hewani tarehe 3 Oktoba 1951, hii inaonesha ishara ya upendo na utayari wa Baba Mtakatifu na Vatican kwa ujumla kwa watu wa Albania. Itakumbukwa pia kwamba Baba Mtakatifu Yohane Paulo II aliitembelea nchi ya Albania mwaka 1993, naye Baba Mtakatifu Francisko alifanya hija hiyo ya kitume nchini humo mwaka 2014, ishara ya kudumisha mahusiano na mawasiliano mazuri kati ya Vatican na nchi ya Albania.

Nchi ya Albania katika udogo wake, imeteseka na kupitia magumu mengi katika historia yake, lakini kwa msaada wa Kristo imepambana, imesimama imara katika uaminifu, mizizi na utambulisho wake kiasi cha kuwa na mashujaa kama Giorgio Castriota Scanderbeg, ishara ya umoja, ujasiri na nguvu ya nchi ya Albania. Wakati wa harakati za kuipatia uhuru nchi ya Albania, Giogio Castriota alipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa Mababa Watakatifu kipindi hicho.

Albania ni kati ya nchi ambamo raia wake ni sehemu ya jumuiya za madhehebu na dini tofauti tofauti, lakini wanaishi kwa amani na udugu kati yao. Hii inawezekana kwa kuheshimu utambulisho na tofauti za kila mmoja. Albania pamoja na kupitia miaka ya utawala wa kikomunisti tangu miaka ya 1990, sauti za raia na umoja wao kutafuta mabadiliko ya demokrasia ya kweli vimekuwa vikisikika sana katika mawimbi ya Radio Vatican. Katika kipindi hicho kumekuwa na watu walioigusa historia ya nchi hiyo kwa namna ya pekee, mfano Watakatifu Yohane Paulo II na Mama Theresa wa Calculta, anasema Monsinyo Viganò. Radio Vatican, inarusha matangazo sio tu ya kumbukumbu au habari za maumivu, bali pia habari za upendo, matumaini na maendeleo ya watu. Mfano kwa sasa, nchi ya Albania imekuwa na habari nyingi za kujivunia utajiri, fadhila, udugu na umoja ambavyo ni sehemu ya nchi nyingi barani Ulaya. Monsinyo Viganò kawatia moyo waendelee kujiaminisha kwa Mungu katika safari yao ya matumaini kidemokrasia na kimaendeleo.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.