2017-07-04 14:09:00

Mshikamano wa Papa Francisko na waathirika wa tetemeko la ardhi Lesvos


Athari za mabadiliko ya tabianchi na majanga asilia ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kuwatumbukiza watu wengi katika umaskini wa hali na kipato! Ili kupambana fika na majanga asilia, Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna haja ya kujenga utandawazi wa mshikamano wa upendo, unaomwilishwa katika matendo ya huruma, kielelezo makini cha imani tendani! Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mahangaiko ya watu waliotikiswa na tetemeko la ardhi kwenye Kisiwa cha Lesvos, Jimbo Katoliki la Chios, nchini Ugiriki ameamua kuchangia kiasi cha Euro 50, 000, ili ziweze kuwasaidia waathirika wa tetemeko hili lililotokea tarehe 2 Juni 2017.

Askofu mkuu Nìkòlaos Printesis wa Jimbo Katoliki la Naxos, Tinos, Andro na Mykonos, ambaye pia ni msimamizi wa kitume wa Jimbo Katoliki la Chios aliowaomba maafisa wa Ubalozi wa Vatican nchini Ugiriki kumtaarifu Baba Mtakatifu Francisko kuhusu mahangaiko ya watu wake kutokana na tetemeko la ardhi pamoja na uwepo mkubwa wa wakimbizi na wahamiaji waliokuwa wanahitaji msaada wa dharura. Baba Mtakatifu baada ya kusikia taarifa hizi na kwamba, kuna kijiji ambacho kiliathirika vibaya sana kiasi hata cha kufutika katika ramani ya uso wa nchi. Kuna baadhi ya watu wamefariki dunia kwa kufukiwa na kifusi cha udongo na wengine wengi wamepata vilema vya kudumu na majeraha makubwa!

Akizungumzia kuhusu msaada huu ambao hivi karibuni watapelekewa walengwa na  Askofu mkuu Nìkòlaos Printesis, Monsinyo Massimo Catterin kutoka Ubalozi wa Vatican nchini Ugiriki anasema, msaada huu ni muhimu sana kwani unachukua pia mwelekeo wa kiekumene unaojikita katika uekumene wa huduma, kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Wakristo kushikamana katika uekumene wa huduma, kama kielelezo makini cha imani tendaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.