2017-07-04 13:50:00

Msaada wa maendeleo endelevu toka Baraza la Maaskofu Katoliki Italia!


Majiundo makini ya awali na endelevu; ujuzi na maboresho ya huduma ya afya, elimu, ustawi na maendeleo ya wengi pamoja na kuwajengea wanawake uwezo wa kukabiliana na changamoto za maendeleo ni kati ya mambo makuu yaliyopewa kipaumbele cha kwanza na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kwa ajili ya kusaidia  kugharimia mchakato wa maendeleo endelevu katika Nchi changa zaidi duniani. Kiasi cha Euro millioni 13 zitatolewa msaada ili kugharimia miradi ya maendeleo endelevu 89 Barani Afrika; 12 Amerika ya Kusini; 13 Barani Asia na Mradi mmoja huko Mashariki ya Kati.

Taarifa kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Italia inaonesha kwamba, nchi ya: Burkina Faso, Burundi, DRC na Togo ndizo ambazo zitanufaika na msaada huu wa maendeleo endelevu ili kuchimba kisima cha maji safi na salama kwa kutambua kwa maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Huduma ya maji kwa waathirika wa dawa za kulevya na ulevi wa kupindukia itatolewa nchini Bukrina Faso. Nchini Burundi, mradi unaofadhiliwa ni kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha haki na amani mjini Bujumbura, ili kuwafunda watu umuhimu wa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano kati ya watu, kama jambo muhimu sana la kukuza na kudumisha maendeleo ya kweli ya binadamu! Nchini DRC., fedha hii itatumika kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji wanaoendelea kuteseka kutokana na vita huko DRC.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linakumbusha kwamba, hii ni sehemu ya ukarimu wa familia ya Mungu inayotoa kama kodi kwa ajili ya mahitaji ya Kanisa Katoliki ndani na nje ya Kanisa. Maaskofu pia wamekuwa mstari wa mbele katika kuchangia huduma kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi Barani Ulaya. Mkazo kwa wakati huu ni kuweza kuwasaidia watu hawa huko huko waliko, kwa kuboresha mazingira ya maisha na huduma, ili kupunguza kishawishi cha kutaka kukimbilia Barani Ulaya, ambako kwa sasa hali si nzuri sana kama wengi wanavyodhani! Hii inatokana na ukweli kwamba, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji sasa ni changamoto inayoendelea kuligawa Bara la Ulaya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.