2017-07-04 11:02:00

Makanisa yanaridhia Tamko Juu ya Mafundisho ya Kuhesabiwa Haki


Kunako mwaka 1917, Martin Luther alisherehekewa na kukumbukwa kama muasisi wa lugha ya Kijerumani, shujaa na mwana mapinduzi mahiri wa Kanisa, aliyetaka kulipyaisha Kanisa kutoka katika undani wa maisha na utume wake. Kwa bahati mbaya, Ulaya ikajikuta inatumbukia katika Vita kuu ya Kwanza ya Dunia iliyosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Mahusiano kati ya Wakatoliki na Waluteri yakawa na sura mbaya sana anasema Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha umoja wa Wakristo. Ulaya ikajikuta ikimeguka kutokana na kinzani za kivita, mipasuko ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Lakini, mchakato wa majadiliano ya kiekumene uliendelea kushika kasi pole pole na kwa namna ya pekee, baada ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Hapa, mchakato wa majadiliano haya ukaanza kuchukua sura mpya, kwa kushiriki katika furaha, mateso na matumaini ya Wakristo wengine duniani! Kumbe, maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani ni hatua muhimu katika majadiliano ya kiekumene kati ya Wakatoliki na Waluteri Duniani. Waamini wa pande zote mbili wameweza kujifunza ili kurejesha na kuimarisha imani ya waamini kwa Kanisa la Kristo lengo kuu lililokuwa moyoni mwa Martin Luther wakati akianzisha cheche za mageuzi ya Kiluteri!

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani yamelenga kukuza na kudumisha umoja wa kiekumene unaofumbatwa kwa namna ya pekee katika mchakato wa kulipyaisha Kanisa la Kristo mintarafu mwanga wa Injili. Maadhimisho haya yamekuwa ni muda muafaka wa kushukuru kwa mema yaliyojitokeza katika mchakato wa kulipyaisha Kanisa; kutambua dhambi na mapungufu yaliyojitokeza kati ya Makanisa haya mawili na kuwa tayari kujuta na kuomba huruma na msamaha wa Mungu, tayari kuchanja mbuga kwa imani na matumaini!

Kuanzishwa kwa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani anasema Kardinali Kurt Koch ni njama za kisiasa zilizoteka mchakato wa mageuzi ya Kiluteri kunako karne ya XVI, kumbe, hii ni sehemu ya mapungufu ya mageuzi haya, kwani yalisababisha Umoja wa Kanisa la Kristo kumeguka. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wakaona ile nia njema ya Mageuzi ya Kiluteri, wakalitaka Kanisa kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene ili kujenga tena Umoja wa Kanisa. Mwaka 2017 ni changamoto na mwaliko wa kurejea tena na tena katika wazo asilia la kutaka kulipyaisha Kanisa la Kristo, changamoto ambayo inapaswa kufanyiwa kazi na Wakatoliki na Waprotestanti ili kusuka tena ule uhusiano na umoja wa Kiekumene unaofumbatwa katika Sakramenti ya Ubatizo na ushuhuda wa Neno la Mungu. Hiki ni kipindi cha “kushukuru” kwa mchakato wa majadiliano ya kiekumene ulionzishwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani likawa la kwanza kujiunga na mchakato huu na matunda yake ni mweleko wa upatanisho baada ya Makanisa haya mawili kuchapisha hati ya pamoja juu ya “Tamko la Pamoja Juu ya Mafundisho Ya Kuhesabiwa Haki” iliyotiwa mkwaju kunako mwaka 1999.

Hii ni hati inayofumbata mambo msingi ya imani ya Kanisa, kumbe, hili ni jiwe la msingi la majadiliano ya kiekumene! Katika imani, twasadiki kwa pamoja kwamba kuhesabiwa haki ni kazi ya Mungu aliye Mmoja katika Nafsi tatu. Baba amemtuma Mwanae ulimwenguni kuwaokoa wenye dhambi. Umwilisho, kifo na ufufuko wa Kristo ni msingi na asili ya kuhesabiwa haki. Kwa hiyo, maana ya kuhesabiwa haki ndiyo hii: Kristo mwenyewe ni haki yetu, ambayo twaishiriki kwa njia ya Roho Mtakatifu, kulingana na mapenzi ya Baba. Kwa pamoja twakiri: kwa neema tu, katika imani kwa tendo la wokovu la Kristo, wala si kutokana na stahili yetu yoyote, tunakubaliwa na Mungu na kupewa Roho Mtakatifu, anayefanya upya mioyo yetu na kututayarisha na kutuita kwa ajili ya matendo mema.

Watu wote wanaitwa na Mungu kupata wokovu katika Kristo. Tunahesabiwa haki kwa njia ya Kristo tu, tukipokea wokovu huo katika imani. Imani yenyewe ni kipawa cha Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu, atendaye kazi kwa njia ya Neno na ya Sakramenti katika jumuiya ya waamini, na wakati huohuo huwaongoza kwa upyaisho ule wa maisha ambao Mungu ataukamilisha katika uzima wa milele. Twashiriki pia imani kwamba ujumbe wa kuhesabiwa haki hutuelekeza, kwa namna ya pekee, kwenye kiini cha ushuhuda wa Agano Jipya juu ya tendo la Mungu la wokovu katika Kristo. [Ushuhuda huo] unatutangazia kwamba sisi, huku tukiwa wenye dhambi, maisha yetu mapya yanaitegemea tu huruma ya Mungu yenye kusamehe na yenye kufanya upya, ambayo Yeye atujalia kama kipawa, nasi twaipokea katika imani, bila kuweza kuistahili kwa namna yoyote.

Kwa hiyo mafundisho ya kuhesabiwa haki, yapokeayo na kufafanua ujumbe huo, si tu sehemu fulani ya mafundisho ya kikristo, bali yana uhusiano wa msingi na kweli zote za imani, ambazo hatuna budi kufikiria zihusiane kiundani zenyewe kwa zenyewe. [Mafundisho ya kuhesabiwa haki] ni kigezo cha lazima kinachofaa daima ili kumwelekezea Kristo ufundishaji wote na utendaji wote wa Makanisa yetu. Walutheri, wanapotilia mkazo umuhimu wa pekee wa kigezo hicho, hawakani umuhimu wa kweli zote za imani, wala kwamba zinahusiana. Wakatoliki, wakijifikiria wamefungamana na vigezo mbalimbali, hawakani dhima maalum ya ujumbe wa kuhesabiwa haki. Walutheri na Wakatoliki wanashiriki kwa pamoja lengo la kumkiri Kristo katika mambo yote, Yeye anayetakiwa kuaminiwa juu ya mambo yote kama Mpatanishi pekee (1 Tim 2:5-6), ambaye kwa njia yake, Mungu, katika Roho Mtakatifu, ajitoa nafsi yake na kumimina vipawa vyake vyenye kufanya upya [vitu vyote].

Kumbe, huruma na msamaha iwe ni dira na mwongozo katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene duniani!  Kardinali Kurt Koch anasema ”matumaini” yanayobubujika kutoka katika toba na wongofu wa ndani, tayari kuanza mchakato wa ujenzi wa Umoja wa Kanisa katika furaha na shukrani kwamba, licha ya mapungufu ya binadamu, Kanisa linaweza kusonga mbele ili kudumisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene katika ukweli na uwazi. Baada ya miaka 500 ya utengano, sasa ni wakati wa kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa Wakristo, ili kunako mwaka 2030, Kanisa litakapokuwa linaadhimisha Jubilei ya miaka 500 ya Baraza la Augsburg sanjari na Ilani ya Augustana, Wakristo wote waweze kukiri imani yao kwa Kristo Yesu. Kumbe, kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri ni mwanzo mpya katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika: shukrani, toba na matumaini.

Tarehe 5 Julai 2017 huko Wittenberg, Ujerumani, mahali ambako kunako mwaka 1517 Martin Luther alianzisha cheche za mageuzi ndani ya Kanisa kwa kuwasilisha  pingamizi 95  dhidi ya rehema zilizokuwa zinatolewa na Kanisa, kunafanyika tukio la kiekumene. Makanisa ya Upyaisho “Reformed Churches” yanajiunga na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani pamoja na Kanisa Katoliki katika Tamko la Pamoja Juu ya Mafundisho ya Kuhesabiwa Haki, lililotiwa mkwaju kunako mwaka 1999. Katika tukio hili muhimu na la kihistoria, Baraza la Kipapa la kuhamasisha umoja wa Wakristo linawakilishwa na Askofu mkuu Brian Farrel, Katibu mkuu wa Baraza pamoja na Padre Avelino Gonzalez, afisa anayeshughulikia Makanisa ya Magharibi katika Baraza hili.

Tukio hili ni muhgimu sana katika mchakato mzima wa majadiliano ya kiekumene ili kujenga na kudumisha umoja wa Kanisa la Kristo hata kama bado haujakamilika na kuonekana sana.  Tamko la Pamoja Juu ya Mafundisho ya Kuhesabiwa Haki na dhamana ya utekelezaji wa haki, amani na upatanisho ni mambo msingi sana yanayowahamasisha Wakristo sehemu mbali mbali za dunia kujenga na kudumisha uekumene wa sala, maisha ya kiroho, huduma na ushuhuda wa damu. Kwa kuwa na uelewa wa pamoja, Makanisa haya yataweza kushikamana katika kutoa huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Lakini, jambo la msingi ni kuishi katika umoja, upendo na mshikamano kama ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Injili ya Kristo kati ya watu wa Mataifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.