2017-07-04 14:36:00

Majadiliano ya kiekumene! Miaka 50 mengi yamefanyika!


Shirikisho la Makanisa ya Kiluteri Duniani linaendelea kuadhimisha Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani kwa kuangalia yaliyopita kwa toba, ili kuweza kuyaambata ya leo kwa imani, matumaini na mapendo. Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, mchakato wa majadiliano ya kiekumene umechukua kasi kubwa na kupata sura mpya zaidi inayojikita katika ushuhuda wa pamoja miongoni mwa wafuasi wa Kristo! Ikumbukwe kwamba, Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ni msingi wa mapambazuko ya majadiliano ya kiekumene ambayo yanaendelea kuboreka siku hadi siku kwa matumaini kwamba, siku moja kadiri ya Roho Mtakatifu, Makanisa yote yatakuwa chini ya Kristo mchungaji mkuu.

Haya ni matumaini yaliyooneshwa hivi karibuni na Dr. Martin Junge, Katibu mkuu wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani wakati alipokuwa anachangia hoja kwenye  kongamano la kiekumene kuhusu taalimungu lililofanyika kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Saramanca. Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita anasema Dr. Junge, kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika mahusiano miongoni mwa wakristo, changamoto na mwaliko kwa Makanisa kusoma historia na matukio mbali mbali ya maisha kwa mwanga mpya hata kama bado kuna tofauti kubwa sana za mawazo kuhusu: Urithi wa kiti cha kitume; dhana na maana ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu pamoja na Daraja Takatifu kwa Wanawake.

Dr. Junge anakaza kusema, Hati ya Kiekumene kati ya Kanisa la Kiinjili la Kiluteri na Kanisa Katoliki “Kutoka katika kinzani kuelekea umoja” inatoa changamoto kwa Makanisa haya mawili kutokatishwa tama na vikwazo, magumu na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, bali wao, waendelee kujielekeza zaidi katika majadiliano yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Majadiliano ya kiekumene katika maisha ni chemchemi ya furaha na matumaini ya watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia.

Dr. Junge anakumbusha kwamba, historia iliyopita kwa Makanisa mengi, iligubikwa na chuki, vita na ghasia za kidini zilizobebwa na matamanio ya kisiasa na kiuchumi pengine kuliko hata na imani ya Kanisa. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Mtakatifu Yohane Paulo II na Papa Mstaafu Benedikto XVI wamechangia sana katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene. Lakini, kwa mshangao mkubwa, Baba Mtakatifu Francisko ameweka majadiliano ya kiekumene kama moja ya vipaumbele vya maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro na matunda yake yanaonekana katika mahusiano na mafungamano ya Wakristo katika medani mbali mbali za maisha.

Dr. Junge  anasema, ni mwelekeo, mtazamo na hisia tofauti kabisa zilizowawezesha waamini wa Kanisa la Kiluteri kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuungana na Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani! Miaka kadhaa iliyopita, ndoto ya namna hii, isingeweza kuwepo! Kumbe, majadiliano ya kiekumene yanafumbatwa katika uhalisia wa maisha, kwa kuthubutu kusonga mbele kwa imani na matumaini pasi na kukatishwa tama na magumu pamoja na changamoto za maisha! Makanisa yanahamasishwa kujikuta katika uekumene wa sala na maisha ya kiroho; uekumene wa huduma na ushuhuda wa damu, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha imani kwa Kristo na Kanisa lake. Majadiliano ya kekumene katika masuala ya kitaalimungu yataendelea ili kuwasaidia waamini kutambua imani, maisha na utume wa Kanisa. Ni mchakato ambao unapaswa pia kuyahusisha Makanisa ya Kiinjili ya Kipentekosti ambayo kwa miaka mingi yalitelekezwa pembezoni mwa majadiliano ya kiekumene kimataifa!

Itakumbukwa kwamba, ilikuwa ni tarehe 5 Julai 1517 Martin Luther akiwa mjini Witenberg, nchini Ujerumani aliamua kujitenga rasmi na Kanisa Katoliki na huo ukawa ni mwanzo wa mchakato wa kuundwa kwa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani. Tamko kuhusu “Kuhesabiwa Haki ndani ya Kanisa” lililotiwa mkwaju kunako mwaka 1999, limesaidia sana kupunguza mpasuko miongoni mwa Wakatoliki na Waluteri duniani. Tangu wakati huo, kumekuwepo na Makanisa kadhaa ambayo yameridhia “Tamko la Pamoja Juu ya Mafundisho ya Kuhesabiwa Haki”

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.