2017-07-03 09:21:00

Papa Francisko: Wakristo jengeni mahusiano thabiti na Kristo Yesu!


Kristo Yesu baada ya kuwachagua na kuwafunda wafuasi wake, anawatuma kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu katika vijiji vya Galilaya na Yuda, huku akikazia mambo msingi ambayo mitume wake watatakiwa kuyazingatia kama wafuasi wamissionari. Jambo la kwanza kabisa lazima wajenge uhusiano wa nguvu na Kristo Yesu kuliko mahusiano na mafungamano mengine yote; pili ni kutambua kwamba, kama wamissionari wanapaswa kumbeba na kumpeleka Kristo Yesu kwa watu na wala si wao kujipeleka kwa watu! Kwa njia yake pamoja naye na ndani yake, upendo na huruma ya Baba wa milele, viweze kuwafikia watu wa Mataifa. Mashari haya mawili yanakwenda pamoja kwani Kristo Yesu ndiye kiini na maisha ya wafuasi wake wanaopaswa kuwa wazi kwa njia ya uwepo wake.

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 2 Julai 2017, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, mahusiano na mafungamano yanayoweza kudhihirishwa kwa njia ya wema na upendo wa wazazi, ndugu na jamaa, hata kama ni mazuri kiasi gani, hayawezi kamwe kupita mahusiano na Kristo Yesu kwani mahusiano kati ya mfuasi na Mwalimu wake, hayana budi kupewa kipaumbele cha kwanza. Mahusiano haya hayajalishi hali, wito wala maisha ya mwamini ndani ya Kanisa.

Jambo la msingi kama Wakristo, anasema Baba Mtakatifu, wanapaswa kujiuliza ikiwa kama wanajitaabisha kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao ya kila siku? Je, wamejenga ari, moyo na utamaduni wa kusali mara kwa mara kama njia mbashara ya kukutana na kuzungumza na Yesu katika maisha yao? Hapa lengo ni kujenga na kuimarisha mafungamano na Kristo Yesu, anayewaita, akawafundisha na hatimaye, kuwatuma kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Kristo Yesu pamoja na wafuasi wake, wanapaswa kushibana na kuwa wamoja kama ambavyo inafafanuliwa katika Kitabu cha Mwanzo. (Rej. Mwa. 2:24).

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kwa mfuasi ambaye anavutwa kwa kiasi hiki katika upendo na maisha, anageuka kuwa ni mwakilishi na “Balozi” wake mwaminifu, kwa mtindo wake wa kuishi na kuwa shuhuda wa uwepo endelevu wa Mungu katika Kristo Yesu kwa njia ya maisha yao. Ushuhuda wenye mvuto na mashiko, uwawezeshe watu kumtambua “Kristo Yesu” kati ya wafuasi wake anayekuwa ni kiini, lengo na hatima ya maisha yao! Hapa haijalishi udhaifu na mapungufu ya kibinadamu ambalo ni jambo la kawaida kabisa, lakini Baba Mtakatifu anakaza kusema, lazima watambue hali yao kwa moyo wa unyenyekevu, kwani hakuna jambo baya kuwa na maisha ya unafiki kama Mkristo!

Wafuasi wa Kristo hawana budi kushikamana na Mwalimu wao, ili kuwa na roho moja na moyo mmoja! Wakristo wajitahidi kuwa waaminifu mbele yao wenyewe na mbele ya jirani zao, kwani unafiki hauna tija wala mashiko katika maisha ya Kikristo! Kutokana na hatari iliyoko mbele yao, ndiyo maana Kristo Yesu aliwaombea wafuasi wake ili wasije wakaangukia majaribuni na hatimaye kumezwa na malimwengu! Haiwezekani kuwatumikia Mabwana wawili! Hapa anasema Baba Mtakatifu Francisko kwamba, uzoefu na mang’amuzi ya maisha na utume wa Kipadre unawafundisha kwamba, ukarimu unaooneshwa na watu wa Mungu kama ambavyo umebainishwa katika Injili ya Jumapili ya XIII ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa, unapotolewa kwa imani na upendo, unawawezesha kuwa ni mapadre wema.

Baba Mtakatifu anawakumbusha mapadre wenzake kwamba, ikiwa kama watajisadaka bila ya kujibakiza na kuendelea kushikamana na Kristo Yesu katika maisha na utume wao, kwa hakika watu wa Mungu watatambua uwepo wa Kristo katika maisha yao; hii inageuka na kuwa ni chachu ya toba na wongofu wa ndani, safari ambayo mapadre wanapaswa kuifanya kila siku ya maisha yao. Hii ni changamoto kubwa kwa mapadre kupyaisha maisha yao kila siku na kuendelea kujitakasa kutoka katika malimwengu yanayoweza kuwazonga zonga kiasi cha kupoteza dira na mwelekeo wa maisha na hatimaye, kuanguka vishawishini!

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwa kina kwamba, kwa padre anayejisikia kuwa karibu sana na watu wa Mungu, vivyo hivyo, ataweza kujisikia kuwa karibu sana na Yesu na anapojisikia karibu na Yesu, atakuwa karibu sana na watu wa Mungu! Mwishoni, Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, Bikira Maria kwa namna ya pekee kabisa katika maisha yake, ameonja maana ya kumpenda Kristo Yesu, kwa kuwa na mahusiano mapya yanayobubujika kutokana na imani kwa Yesu. Sala na maombezi yake ya kimama, yawasaidie waamini kuwa huru na wamissionari wa Injili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.