2017-07-03 09:37:00

Papa Francisko: Venezuela kunawaka moto!


Nchi ya Venezuela inaendelea kutumbukia katika hali tete sana ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Kuna watu wanaoendelea kuuwawa kikatiliki kutokana na vyombo vya ulinzi na usalama kutumia nguvu kupita kiasi. Haki msingi za binadamu, utu na heshima ya binadamu vinaendelea kukandamizwa, kiasi kwamba, ndoto ya wananchi wa Venezuela kuwa na demokrasia ya kweli, utawala bora na utawala wa sheria, vinaonekana kutoweka kila kukicha! Ghasia, vurugu na uporaji wa mali yamekuwa ni matukio ya kawaida nchini Venezuela.

Wananchi wanaoshiriki hata katika maandamano ya amani, wanashambuliwa na vikosi vya ulinzi na usalama bila hata ya huruma na wengi wao wanaishia kutupwa magerezani na huko wanakiona cha mtema kuni! Utawala wa sheria unaoheshimu mihimili mikuu ya dola unaanza kumong’onyoka kwa kasi ya ajabu kabisa, kwa kuwatia pingu wale wanaopaswa kusimamia sheria na utawala bora! Kutokana na hali kama hii, waendesha mashitaka wakuu kutoka Argentina, Brazil, Paraguay, Uruguay, Chile na Perù wameandika waraka ili kuonesha mshikamano wao wa karibu na wale wote wanaonyanyaswa kutokana na kupindishwa kwa utawala wa sheria unaozingatia haki msingi za binadamu na katiba ya nchi kama sheria mama!

Baba Mtakatifu Francisko, mara tu baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 2 Julai 2017 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amekumbushia kwamba, tarehe 5 Julai 2017, Venezuela inaadhimisha kumbu kumbu ya uhuru wake. Anapenda kuwahakikishia wananchi wote wa Venezuela uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala. Anazikumbuka na kuziombea familia zote ambazo zimewapoteza watoto wao kutokana na kushambuliwa wakati wa maandamano nchini Venezuela.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwataka wadau wote kusitisha ghasia na machafuko na kuanza kujikita katika mchakato wa amani na demokrasia unaopania kutoa suluhu ya kweli katika machafuko haya ya kisiasa. Baba Mtakatifu anamwomba Bikira Maria wa Coromoto, aweze kuwasimamia na kuwalinda wananchi wa Venezuela. Baba Mtakatifu ameungana na waamini pamoja na mahujaji waliokuwepo kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ili kusali kwa ajili ya nia hii njema!

Wachunguzi wa masuala ya kiuchumi huko Amerika ya Kusini wanasema, mgogoro na mpasuko wa kisiasa nchini Venezuela unaendelea kuleta athari kubwa kwa ustawi na maendeleo ya nchi jirani kutokana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaohitaji msaada wa dharura hasa nchini Colombia na Brazil. Kuna idadi kubwa ya watu wanaoomba hifadhi ya kisiasa nchini Brazil. Hali ni mbaya sana huko Brazil wanakokimbilia wananchi kutoka Venezuela kwani wanajikuta wakiwa kati kati ya maskini wenzao! Kanisa limekuwa likijitwika dhamana ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji hawa, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa watoto na wanawake kadiri ya taarifa ya Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini Brazil.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.